Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-05 20:23:39    
Mfaransa Bw. Le Blainvaux anayefanya kazi nchini China

cri

Kampuni ya Shenlong ni kampuni kubwa ya kutengeneza magari hapa nchini China, ambayo ilianzishwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya Peugeot Citroen ya Ufaransa na kampuni ya Dongfeng ya China, pia ni mradi mkubwa kuliko mingine uliowekezwa na Ufaransa nchini China. Katika makala hii tunawaletea maelezo kuhusu Mfaransa Bw. Le Blainvaux, ambaye ni mkuu wa kiwanda cha kuunganisha magari cha kampuni hiyo.

Miaka 11 iliyopita kampuni ya Shenlong ilipoanzishwa, Wafaransa wengi walikuwa hawataki kuja kufanya kazi nchini China kutokana na umbali mkubwa kati ya China na Ufaransa na kuwa na ufahamu mdogo kuhusu China. Lakini Bw. Le Blainvaux aliyekuwa na hamu ya kupata maendeleo ya kikazi alifurahia kuja China, akapewa nafasi ya kuwa mkuu wa kiwanda cha kutengeneza injini na vipuri vingine vikuu vya magari huko Xiangfan, katikati ya China.

Bw. Le Blainvaux alikumbusha kuwa, mwanzoni alipofika kwenye kiwanda hicho alikuta eneo la ardhi iliyoachwa na wafanyakazi 60 tu, na yeye alikuwa Mfaransa pekee. Katika miaka mitatu iliyofuata Bw. Le Blainvaux na wafanyakazi wakishirikiana waliondoa matatizo mbalimbali na kuendeleza sana kiwanda hicho, ambapo idadi ya wafanyakazi pia iliongezeka kutoka 60 hadi 1,000.

Hapo awali kwa maoni ya Mfaransa huyo, China ilikuwa ni nchi ya mashariki yenye miujiza na maajabu iliyoko mbali sana. Katika miaka hiyo mitatu alishuhudia maendeleo ya China na kuvutiwa na China.

Alisema "Naona China ni nchi inayoendelea kwa haraka, ambapo mabadiliko mengi yalitokea nchini China katika miaka ya karibuni. Kwa mfano barabara zilipanuka, idadi kubwa ya barabara za kasi na madaraja ya barabarani yalijengwa, na kampuni na viwanda vya sekta mbalimbali vinajiendeleza kwa haraka, ikiwemo sekta ya utengenezaji wa magari."

Mwaka 1998 Bw. Le Blainvaux alimaliza muda wake wa kazi nchini China na kutakiwa kurudi nchini Ufaransa kwa mujibu wa utaratibu wa kampuni. Lakini bwana huyo, mke wake na watoto watatu walikuwa hawafurahii kuondoka China. Kabla ya kufunga safari, walinunua vitu mbalimbali vya Kichina, kwa mfano samani za mtindo wa Kichina na vitu vilivyotengenezwa na mikono. Vitu hivyo vilivyohifadhi kumbukumbu nzuri kuhusu China vilijaa kontena moja la mita 30 za ujazo.

Bw. Le Blainvaux akarudi nchini Ufaransa, lakini alionekana kuwa moyo wake bado ulibaki nchini China. Alikuwa anafuatilia habari kuhusu China kila siku, na kufurahia maendeleo yaliyopatikana nchini China, hususan maendeleo ya kampuni ya Shenlong aliyofanyia kazi.

Kadiri magari yaliyotengenezwa na kampuni hiyo yalivyouzwa vizuri katika soko la China, kupata nafasi ya kufanya kazi nchini China likawa jambo la kujivunia miongoni mwa waajiriwa Wafaransa. Lakini kwa mujibu wa utaratibu wa kampuni hiyo, kila mwajiriwa anapewa nafasi moja tu ya kufanya kazi nchini China.

Bw. Le Blainvaux alikuwa na bahati nzuri, kampuni yake iliamua arudi China mwaka 2005. Mwezi Mei mwaka huu, Bw. Le Blainvaux aliteuliwa kuwa mkuu wa kiwanda cha kuunganisha magari kilichoko mjini Wuhan, katikati ya China.

Ikilinganishwa na hali ya miaka 10 iliyopita, Bw. Le Blainvaux aliona kuwa hivi sasa kuna ushindani mkali zaidi kwenye soko la magari nchini China, kwani kampuni maarufu duniani za utengenezaji magari zote zimeanzisha kampuni za ubia nchini China.

Bw. Le Blainvaux alichapa kazi zaidi. Alianza kazi saa 2 asubuhi, ambapo alitembelea karakana moja baada ya nyingine, kutatua masuala mbalimbali pamoja na mafundi.

Ili kukidhi mahitaji ya wateja wa China, kampuni ya Shenlong inapaswa kutengeneza aina mpya za magari kila baada ya kipindi fulani. Hii ni changamoto kuwa kwa Bw. Le Blainvaux akiwa ni mkuu wa kiwanda cha kuunganisha magari. Hata hivyo alisema anafurahia kukabiliana na changamoto. Alisema "Ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwa watu wa sekta ya utengenezaji wa magari kuvumbua kitu kipya, sekta mpya au aina mpya ya gari. Niko hapa nashirikiana na wenzangu wa China kuanzisha karakana mpya, kutengeneza aina mpya za magari na kuyauza sokoni kuwafurahisha watu wa China, hili ni jambo linalonitia moyo sana."

Baada ya kazi Bw. Le Blainvaux anapenda kucheza karata na wafanyakazi wenzake. Bw. Wang Tong ambaye ni mkuu wa karakana moja alimsifu kuwa ni mgeni mwenye tabia nzuri ya kuwavutia watu. Alisema "Ni mpole wakati anakabiliwa na maswali, hali ambayo inaonesha uhodari wake katika uongozi, hivyo unapenda kufanya kazi kwa bidii kwa mara 10 zaidi."

Bw. Le Blainvaux ana uhusiano mzuri na wafanyakazi wenzake wa China, ambao wanamwita "Lao Le" kwa Kichina, maana yake ni Mzee Le. Bw. Le Blainvaux alisema anafurahia jina hilo, kwani Wachina wenyewe wanasalimiana kama Lao Zhang, Lao Li ili kuonesha urafiki.

Hivi sasa kampuni ya Shenlong ina wataalamu na mafundi wa Ufaransa zaidi ya 100, ambao sawa na Bw. Le Blainvaux, katika kipindi cha kuishi nchini China si kama tu wanajitahidi kutimiza matumaini ya kutengeneza magari ya kisasa duniani, bali pia wanapata ufahamu na upendo mwingi zaidi kuhusu China.

Idhaa ya Kiswahili 2006-10-05