Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-05 20:28:52    
Askari polisi wa China wanaoshiriki kwenye jukumu la Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini Afghanistan

cri

Bw. Qiu Chongwen mwenye umri wa miaka zaidi ya 30 ni askari polisi wa China. Mwezi wa Mei mwaka 2005, afisa huyo alitumwa na wizara ya usalama wa raia ya China nchini Afghanistan kushiriki kwenye jukumu la Umoja wa Mataifa la kulinda amani, kwa muda wa mwaka mmoja. Katika makala hii tunawaletea maelezo kuhusu maisha ya Bw. Qiu Chongwen nchini Afghanstian.

Bw. Qiu Chongwen si mrefu lakini ni mchangamfu, akivaa sare ya askari polisi wa Umoja wa Mataifa anaonekana ni mwenye nguvu sana. Alieleza kuwa aliwahi kushiriki kwenye jukumu lingine la Umoja wa Mataifa la kulinda amani, na kushuhudia uchungu mkubwa na umaskini uliosababishwa na vita, hata hivyo alipofika nchini Afghanistan alishtushwa na hali ya nchi hiyo iliyokumbwa na mateso ya vita vya miaka mingi.

Alisema "Niliiangalia Afghanistan kutoka kwenye ndege, kulikuwa hakuna chochote, mji wa Kabul ulikuwa umebomolewa kabisa, ambao ulinipa picha ya kwanza kuwa ustaarabu wa binadamu umerudi nyuma kwa karne kadhaa."

Akiwa afisa msaidizi kwenye kikosi cha askari polisi cha Umoja wa Mataifa, kazi ya Bw. Qiu Chongwen ilikuwa kuisaidia Afghanistan katika mageuzi ya idara ya polisi na kuunda upya kikosi cha askari polisi. Afisa huyo alisema "Mageuzi ya idara ya polisi ni sehemu ya ukarabati wa kisiasa wa Afghanistan, ambayo ni kama ujenzi mwingine wa Afghanistan, sekta zote zinasubiri kufufuka nchini humo. Afghanistan ilikumbwa na vita vilivyodumu kwa miongo kadhaa, tunaweza kusema kila kitu kimeharibiwa, mifumo kamili ya sheria na utekelezaji wa sheria imeharibiwa kabisa, hivyo kila kitu kinapaswa kujengwa upya."

Afisa Qiu Chongwen alisema ili kuandaa mazingira ya usalama kwa ukarabati wa Afghanistan, mageuzi ya polisi yalikuwa ni moja ya mambo muhimu ya kwanza. Ili kuanzisha mfumo wa polisi wenye ufanisi, inapaswa kuifahamu hali halisi ya hivi sasa ya sekta ya polisi nchini Afghanistan. Ingawa kulikuwa na hatari ya kutokea kwa mashambulizi ya kigaidi, afisa huyo alifanya uchunguzi kwenye mikoa yote minne ya Mashariki ya Afaghanistan alikopangiwa, ambapo alitembelea vituo mbalimbali vya polisi, baadaye alitoa mapendekezo kadhaa kwa serikali ya Afganistan na idara husika ya Umoja wa Mataifa. Pia alisaidia idara ya polisi ya Afghanistan kutoa mafunzo kwa askari polisi.

Kutokana na juhudi za Bw. Qiu Chongwen na wenzake wa Umoja wa Mataifa, maendeleo makubwa yamepatikana katika kazi ya polisi nchini Afghanistan, na baada ya kufanyiwa mageuzi na uundaji mpya kikosi cha askari polisi cha nchi hiyo kinafanya kazi muhimu katika ukarabati wa Afghanistan.

Afisa Qiu alitoa mfano wa uchaguzi wa wabunge uliofanyika mwaka 2005 nchini Afghanistan. Alisema katika mchakato wa upigaji kura, yeye na maafisa wasaidizi wenzake wa Umoja wa Mataifa walipelekwa kwenye vituo mbalimbali vya upigaji kura, ambapo wakishirikiana na polisi wa Afghanistan, watumishi wa idara za serikali na wanajeshi wa nchi hiyo, walishughulikia kwa ufanisi matukio ya dharura, na kuhakikisha mchakato wa upigaji kura unafanyika bila matatizo.

Kazi hodari ya Bw. Qiu Chongwen ilisifiwa na serikali ya Afghanistan na idara husika ya Umoja wa Mataifa. Mwezi Oktoba mwaka 2005, alipewa medali ya amani ya Umoja wa Mataifa.

Jambo linalomfurahisha zaidi afisa huyo ni kwamba, kutokana na kazi yake alipata heshima kutoka kwa watu wa Afghanistan na kuongeza urafiki kati ya watu wa China na Afghanistan.

Alisema "Afghanistan ni nchi jirani ya China. China kutuma askari polisi nchini Afghanistan kusaidia ukarabati wa nchi hiyo kunalingana na maslahi ya China, ya kanda hiyo na ya Afghanistan. Watu wa Afghanistan ni marafiki wa Wachina, wengi walinisalimia kwa kusema 'Qin', maana yake ni China, kuonesha urafiki na ukarimu wao."

Bw. Abdulhadi ni mhandisi wa Afghanistan anayeishi mjini Kabul. Alisema "Kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani kimekuja Afghanistan ili kuimarisha usalama wa huku. Ni hadi taifa letu litakapodumisha usalama, ndipo shughuli mbalimbali ikiwemo ukarabati zitakapofanyika bila matatizo. Kwa maoni yangu miongoni mwa askari polisi wa Umoja wa Mataifa, wale wanaotoka China ni hodari kweli, na wanafanya kazi muhimu."

Zikiwa nchi majirani zenye uhusiano mzuri, China pia inafanya kazi muhimu katika kusaidia ujenzi mpya wa Afghanistan. Balozi wa China nchini Afghanistan Bw. Liu Jian alisema, misaada ya dhati kutoka China inatambuliwa na kusifiwa na watu wa Afghanistan.

Alisema "China inashiriki kwenye ukarabati wa Afghanistan kwa njia mbalimbali, zaidi ya hayo sisi Wachina tunawasaidia Waafghanistan kwa kujitolea muhanga. Afghanistan inaona kuwa, misaada ya China ni ya muda mrefu na isiyo na masharti, China haina maslahi binafsi kwenye misaada hiyo. Waafghanistan wanasema, 'ni fahari kwetu kuwa na jirani mzuri, China.'."

Idhaa ya Kiswahili 2006-10-05