Tarehe 8 mwezi huu wabunge wawili wa India waliambukizwa homa ya Dengue, hadi sasa ugonjwa huo umegunduliwa katika majimbo 19, watu zaidi ya 3,400 wameambukizwa na wengine 56 wamekufa nchini India kutokana na ugonjwa huo. Katika siku hiyo waziri mkuu wa India Bw.Manmohan Singh alikwenda kwenye hospitali kuwatazama wagonjwa wa homa hiyo. Wizara ya afya ya India imethibitisha kuwa hali ya homa ya Dengue nchini India ni mbaya, lakini bado haijafikia kiwango cha kuenea haraka.
Tokea mwezi Oktoba idadi ya watu wanaoambukizwa homa ya Dengue nchini India inaongezeka kwa kumi kadhaa kila siku. Hivi sasa katika sehemu ya Delhi wagonjwa wamefikia 886 na watu 21 wamekufa, huko ni sehemu yenye wagonjwa wengi zaidi nchini India, na sehemu nyingine zenye wagonjwa wengi ni majimbo ya Kerala, Gujarat na Rajasthan. Kutokana na kuwa wagonjwa wengi wanapelekwa kwenye hospitali kubwa, hivi sasa limetokea tatizo la upungufu wa damu katika sehemu ya New Delhi, serikali ya mji wa New Delhi imetoa ombi la kutaka watu wajitolee damu kwenye hospitali za kiserikali, na baraza la serikali ya India lilifanya mkutano kujadili namna ya kutosheleza mahitaji ya dawa na damu, na limeunda ofisi maalumu kushughulikia mapambano dhidi ya ugonjwa huo nchini kote, na limetangaza hospitali 30 ziwe hospitali za kuwatibu bure wagonjwa wa homa hiyo.
Kuhusu hali hiyo mbaya vyombo vya habari vya India vinaona kwamba kuenea kwa ugonjwa huo kumekuwa ni hatari ya kitaifa, lakini serikali ya India inakataa ikisema kuwa, ingawa ugonjwa huo uko katika kipindi chake ya kuenea lakini bado haujafikia kiwango cha kutoweza kudhibitiwa, na baadhi ya maofisa wanashutumu vyombo vya habari kutangaza habari zenye kutia chumvi na kusababisha watu kuwa na wasiwasi. Mahakama kuu ya Delhi ililaumu serikali na tume ya mji kutochukua hatua za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
Homa ya Dengue inaambukizwa na mbu, na mbu huzaliana katika maji yaliyotulia kwenye sehemu za makazi, mpaka sasa bado hakuna chanjo, kwa hiyo kuua mbu ni njia muhimu ya kudhibiti ugonjwa huo. Dawa za kuua na kujikinga na mbu zinauzwa haraka katika sehemu zenye homa hiyo na hata ilitokea hali ya kutopatikana kwa dawa hizo, na kazi ya kusafisha mazingira imeimarishwa. Tume ya mji wa New Delhi imeongeza wafanyakazi 2,400 kuondoa maji yaliyotuama na kusafisha mazingira kwa kunyunyiza dawa, na kwenye sehemu zenye wagonjwa wengi kunyunyiza dawa nyumba hadi nyumba, na serikali za mitaa zinataka watoto wavae nguo zenye mikono mirefu.
Nchini India homa ya Dengue inazuka kila mwaka. Mwaka jana watu walioambukizwa walifikia elfu 12, na watu 157 walikufa. Mwaka huu ndugu watatu wa waziri mkuu wa India Bw. Manmohan Singh pia waliambukizwa ugonjwa huo.
Wataalamu wa WHO wanazingatia sana hali ya homa ya Dengue nchini India. Kwenye mkutano uliofanyika hivi karibuni kuhusu homa ya Dengue huko Geneva, wataalamu walisema mlipuko wa homa hiyo uliotokea mwaka huu unahusika na upanuzi wa haraka wa miji katika miaka ya karibuni nchini India. Wanaona kwamba kufuatia kupanuka wa haraka kwa miji, watu wanamiminika mijini na kusababisha matatizo ya huduma ya maji na kuleta takataka nyingi, watu wanalimbikiza maji na kuacha takataka nyingi, mazingira hayo yanafaa kuzaliana kwa mbu. Homa ya Dengue inaambukizwa haraka sana, kama hatua za haraka hazitachukuliwa hakika homa hiyo italeta shinikizo kubwa kwa idara za afya.
|