Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-09 17:45:15    
Viongozi wa sekta ya utamaduni wafafanua Mpango wa Maendeleo ya Utamaduni nchini China

cri

Hivi karibuni viongozi wa Wizara ya Utamaduni, Idara Kuu ya Redio, Filamu na Televisheni pamoja na Ofisi Kuu ya Uchapishaji nchini China walifanya mkutano na waandishi wa habari, kwenye mkutano huo walifafanua Mpango wa Maendeleo ya Utamaduni katika miaka mitano ijayo nchini China, na walijibu maswali ya waandishi wa habari waliotoka nchini China na nchi za nje.

Tarehe 13 mwezi Septemba serikali ya China ilitangaza Mpango wa Maendeleo ya Utamaduni katika kipindi cha Mpango wa 11 wa Maendeleo ya Miaka Mitano. Mpango huo umetoa mwongozo wa ujenzi wa utamaduni, lengo litakalofikiwa na mambo muhimu yatakayofanywa katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Utangulizi wa mpango huo unaeleza kuwa katika dunia ya leo utamaduni umekuwa unachanganyikana zaidi na uchumi na siasa, na pia unafungamana zaidi na sayansi na teknolojia, utamaduni umekuwa na umuhimu zaidi katika ushindani wa nguvu ya taifa na ni moja ya vipimo vya nguvu za taifa. Ingawa ujenzi wa utamaduni umepata maendeleo dhahiri katika miaka zaidi ya 20 iliyopita tokea mageuzi ya uchumi yaanzishwe nchini China, lakini kiwango cha maendeleo hayo bado si kikubwa, na bidhaa za utamaduni bado haziwezi kukidhi mahitaji ya nchini kwa idadi, ubora na aina zake, nguvu ya ushindani wa kimataifa bado ni dhaifu. Waraka wa mpango huo wenye maneno zaidi ya elfu 30 una sehemu nane zikiwa ni pamoja na huduma za kiutamaduni, uchapishaji, mashirika ya shughuli za utamaduni, uvumbuzi wa kiutamaduni, hifadhi ya utamaduni wa kikabila na maingiliano na nchi za nje. Waziri wa utamaduni wa China Bw. Sun Jiazheng alisema mpango huo ni muhimu katika kuendeleza jamii kwa pande zote. Alisema,

"Huu ni mpango pekee kuhusu maendeleo ya utamaduni tokea China mpya ianzishwe, mpango huo unalingana na mahitaji ya kustawisha kwa pamoja uchumi, siasa, utamaduni na jamii, na ni hatua kubwa na ya muhimu katika kusukuma ujenzi wa jamii yenye masikilizano, na kutimiza lengo la kujenga jamii yenye maisha bora kwa pande zote."

Mpango huo umeonesha mkakati wa serikali ya China wa kujenga jamii yenye kutanguliza mbele maslahi ya umma na jamii yenye masikiliano. Katika miaka ya karibuni, vyombo vya habari na wananadharia wametoa maoni yao kuhusu sera za serikali za ngazi mbalimbali ambazo zinatilia mkazo kupita kiasi ukuaji wa uchumi, wakisema mkazo unaotiliwa kwenye ongezeko la mapato ya taifa tu utasababisha matatizo mengi ya kijamii. Katika mpango huo, serikali ya China imeunganisha pamoja kuendeleza utamaduni na kujenga jamii yenye masikilizano kwa pande zote na imesisitiza kujenga mfumo wa kutanguliza mbele maslahi ya umma na kustawisha utamaduni wa umma, mfumo huo unalingana na mfumo unaoimarishwa na serikali ya China miaka ya karibuni katika mambo ya afya, tiba na uhakikisho wa maisha ya kimsingi.

Katika miaka ya hivi karibuni, uchumi wa China umekuwa unakua haraka, katika miji mikubwa huduma za utamaduni na bidhaa za utamaduni karibu ni sawa na nchi zilizoendelea, lakini katika sehemu za mbali za milimani na sehemu kubwa ya magharibi ya China, uchumi bado ni duni kutokana na mazingira ya maumbile na sababu za kihistoria, wakazi wa sehemu hizo hawajaweza kunufaika kama wakazi wa miji mikubwa. Mpango huo unasisitiza kuimarisha kazi za redio, televisheni na filamu. Naibu mkuu wa Idara Kuu ya Redio, Televisheni na Filamu Bi. Zhao Shi alisema, kwa upande mmoja serikali ya China itatilia mkazo kuendeleza kazi za redio, televisheni na filamu, na kwa upande mwingine serikali itawanufaisha wananchi kwa redio, televisheni na filamu, hasa watu wa vijijini. Alisema,

"Serikali itatekeleza miradi mitatu vijijini ili kutatua matatizo ya kusikiliza matangazo ya redio, kutazama televisheni na filamu. Miundombinu ya kupokea matangazo ya redio na televisheni katika sehemu za mbali na sehemu za makabila madogo madogo itaboreshwa ili kupanua maeneo ya kupata matangazo hayo. Hadi mwaka 2010 kila kijiji chenye familia zaidi ya 20 kitahakikishiwa kuwa linapata matangazo ya redio na televisheni."

Matumizi ya teknolojia mpya pia yamesisitizwa katika mpango huo yakiwa ni pamoja na kutumia tarakimu katika matangazo ya redio na televisheni, televisheni za kebo, maktaba, na uchapishaji wa vitabu vya kale kwa kupiga picha, na mtandao wa internet ufikie maeneo yote ya vijiji. Waziri wa utamaduni Bw. Sun Jiazheng amesema, kupunguza pengo kubwa kati ya sehemu zilizoendelea na zilizo nyuma kiuchumi ni suala muhimu katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa umma, na kuhusu suala hili serikali ya China imepata maendeleo kiasi. Alisema,

"Namna ya kupunguza pengo la tarakimu limekuwa ni suala linalofuatiliwa sana duniani. Ujenzi wa mradi wa kunufaika na habari kwa wote utasaidia kuondoa pengo hilo katika nchi yetu yenye watu bilioni 1.3 na kumfanya kila mmoja anufaike na maendeleo utamaduni."

Bw. Sun Jiazheng alisema, Mpango huo unaeleza kuwa China ni nchi yenye eneo kubwa, na kuna tofauti kubwa kati ya sehemu, serikali za mitaa zinapaswa kuimarisha ujenzi wa utamaduni kwa mujibu wa hali halisi ya sehemu zao. Alisema kwa mfano, kwa mujibu wa matakwa ya mpango huo, kabla ya mwaka 2010 kila tarafa ni lazima iwe na kituo cha utamaduni, na kila kijiji kinapaswa kuwa na chumba cha utamaduni, lengo lilo linaweza kutimizwa katika sehemu zenye watu wengi, lakini katika sehemu kubwa za wafugaji wanaohama hama, kituo cha utamaduni hakiwezi kukidhi mahitaji ya watu wote. Kutokana na hali hiyo inafaa idara ya utamaduni itumie njia ya kuwahudumia wananchi mambo ya kiutamaduni kwa gari.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-09