Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-10 17:16:09    
Kampuni za Zhejiang zilizoendea nje

cri

Mkoa wa Zhejiang ambao uko kwenye sehemu ya pwani ya mashariki ya China, ni moja kati ya mikoa ya China ambayo ina maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii. Maendeleo ya mkoa huo ni dhahiri, ukifika kwenye uwanja wa ndege wa Hangzhou na kuelekea mjini Hangzhou kwa gari, barabara za kisasa pamoja na madaraja utakayopita, nyumba utakazoziona kando ya barabara, na uzuri pamoja na usafi wa mji huo, vyote vitakuonesha kuwa umefika kwenye mkoa wenye maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Miaka 20 iliyopita mkoa huo ulikuwa hauna tofauti kubwa na mikoa mingine ya China, ambayo leo inatajwa kuwa iko nyuma kimaendeleo. Lakini sasa hivi mji wa Hangzhou na pamoja na miji mingine midogo ya Mkoa wa Zhenjiang, haina tofauti kubwa na mji mikubwa ya China kama Beijing na Shanghai, au miji mingine mikubwa ya Asia ya Ulaya. Miundo mbinu ya mjini kama barabara na simu, usafiri wa umma, mahoteli ya kisasa, mikahawa na hata mpango wa mji yote inakufanya usione tofauti kubwa ya mtu kuwepo kwenye miji mikubwa na miji ya Mkoa wa Zhejiang.

Pato la jumla la mkoa huo ni Yuan trilioni 1.124 (takwimu za mwaka 2004) linachukua nafasi ya kati ya mikoa yote ya China na pato la wastani kwa wakazi wa mkoa huo kwa mwaka ni dola za kimarekani 3000, pato hilo si kubwa likilinganishwa na mapato ya miji mikubwa ya China, lakini linatosheleza kuwafanya wakazi wa huko waishi maisha ya furaha.

Ukijionea hali hii kwa macho yako, na ukilinganisha na mikoa mingine ya China itakuwa ni jambo la kawaida kujiuliza ni kwanini mkoa huo umekuwa na maendeleo mkubwa namna hii? Kuna sababu nyingi zinazoufanya Mkoa huo uwe moja ya mikoa yenye maendeleo makubwa ya kiuchumi nchini China. Kwanza kabisa kuna ushirikiano mkubwa kati ya Chama na serikali ya mkoa huo, na wafanyabiashara wenyeji na wageni wenye nia ya kujiendeleza. Pili ni kuwa mkoa huo una watu wachapakazi, wanaopenda kufanya biashara na wanaopenda kujitafutia maendeleo kwa nguvu, na tatu ni ushirikiano kati ya mkoa huo na mikoa mingine na hata nchi za nje, pamoja na utekelezaji mzuri wa sera ya mageuzi na ufunguaji mlango.

Moyo wa kuchapa kazi na ushirikiano kwa watu wa mkoa huo unaweza kuthibitishwa na baadhi ya viwanda na makampuni yaliyomo mkoani humo. Mfano mzuri wa moyo wa kuchapa kazi kwa wananchi wa Mkoa huo ni kampuni ya Wangxian Group. Kampuni hiyo ambayo zamani ilikuwa ni karakana ndogo ya kukarabati baiskeli, sasa ni moja kati ya Kampuni kubwa 500 nchini China, inayojihusisha na utengenezaji wa vitu mbalimbali kama vipuri vya magari, zana za kilimo na pia inajihusisha na shughuli nyingine. Mkuu wa Kampuni hiyo Bw Lu Guanchiu ambaye ni mtoto wa mkulima, alisema pamoja na juhudi zake binafsi na wafanyakazi wenzake kuiendeleza kampuni hiyo na kufikia mafanikio iliyonayo sasa, Chama na serikali mkoani Zhejiang vimetoa msaada mkubwa na kuifanya kampuni hiyo iwe moja kati ya kampuni kubwa za China. Mwanzoni Kampuni hiyo ilikuwa inashughulikia mambo machache lakini baada ya kupata maendeleo kiasi Chama na serikali mkoani Zhejiang ilitoa msaada kwa Kampuni hiyo ili iweze kuendeleza shughuli zake kimataifa.

Kampuni nyingine kubwa ambayo ipo mkoani humo Hengdian Group, ilianzishwa mwaka 1975 na Bw Xu Weirong. Mwanzoni ilikuwa ni kampuni ndogo ilijihusisha na utengenezaji wa nguo za hariri. Lakini kutokana na juhudi za miaka zaidi ya thelathini, sasa kampuni hiyo ni moja ya Kundi la kampuni kubwa kabisa nchini China ambayo inajihusisha na mambo ya utengenezaji wa dawa, bidhaa za sumaku, vifaa vya umeme, nguo, vifaa vya ujenzi na utengenezaji wa filamu. Bila shaka sio tu kundi kubwa la kampuni kama hilo limesaidia kutoa ajira kwa wakazi wa mkoa huo na wengine kutoka sehemu mbalimbali za China, lakini pia limeweza kusaidia kubadilisha sura ya mji wa Hengdian kutokana na ujenzi wa majengo yanayohusiana na shughuli zake na pamoja na miundo mbinu ambayo pia inawanufaisha wakazi wa huko.

Kampuni hizi mbili ni mfano tu wa Kampuni zilizopo mkoani Zhejiang Kampuni nyingine inayotengeneza nguo nzito Eral, na kampuni nyingine ya kutengeneza soksi Meng Na, nazo ni baadhi ya kampuni ambazo zimefuata nyayo za kampuni hizo. Wakuu wote wa kampuni hizo, pamoja na kuonesha kuwa juhudi zao na moyo wao wa kuchapa kazi ni sababu muhimu ya wao wa kampuni zao kupata maendeleo, wote pia walikiri kuwa isingewezekana kwa wao kupata maendeleo makubwa bila msaada na uungaji mkono kutoka kwa Chama na serikali mkoani humo.

Miundo mbinu ya mawasiliano ya mkoa huo, na inayounganisha mkoa huo na mikoa mingine, miji, wilaya na vijiji kwa ujumla ni mizuri, ni rahisi kusafiri au kusafirisha bidhaa kutoka mji mmoja hadi mji mwingine kwa njia ya reli, barabara na hata kwa ndege. Hali hii inawawezesha wakazi wa mkoa huo waweze kufanya biashara baina yao, na hata kufanya biashara na watu wa mikoa mingine na wa nchi nyingine kwa urahisi. Sasa Bidhaa zinazozalishwa Zhejiang zinapatikana kwa urahisi katika sehemu nyingi nchini China. Hali hiyo pia ni moja ya sababu inayowavutia wawekezaji kutoka nje na wafanyabiashara wageni ambao wanaona miundo mbinu ya huko imeweka urahisi kwa wao kufanya biashara ya kimataifa.

Ushirikiano kati ya mkoa huo na mikoa mingine, na kati ya mkoa huo na nchi ni nyingine duniani, pia umechangia kuharakisha maendeleo ya kiviwanda na biashara ya mkoa huo. Bara la Afrika ni sehemu moja ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na mkoa huo, hadi kufikia siku za karibuni Mkoa huo umeanzisha mashirika na makampuni zaidi ya 195 barani Afrika, na thamani ya biashara kati ya mkoa huo na Afrika ni zaidi ya dola za kimarekani milioni 65.5, mkoa huo ukiwa umewekeza zaidi ya dola za kimarekani milioni 57.9 barani Afrika. Pia bidhaa nyingi za nguo, vifaa vya umeme, na mitambo myepesi kutoka Zhejing inauzwa barani Afrika. Kwenye soko la bidhaa ndogondogo la Yiwu tuliweza kuona duka moja la vinyago vya mpingo. Mmiliki wa duka hilo alituambia kuwa vinyago hivyo vinatoka Afrika.

Mbali na mfanyabiashara huyo anayeingiza bidhaa kutoka Afrika, pia kuna wafanyabiashara wengi kutoka Afrika wanaonunua bidhaa kwenye soko hilo na kusafirisha kwenda barani Afrika. Kwenye pitapita yetu kwenye soko hilo tulikutana na wafanyabishara kutoka nchini Mauritania ambao walituambia kuwa wananua bidhaa mara kwa mara kwenye Soko la Yiwu na kuzipeleka Mauritania. Bwana Mohamed ambaye ni mmoja kati ya wafanyabishara hao alisema sasa hivi anasafirisha makontena mara kwa mara kutoka Zhejiang kwenda nchini mwake, na bidhaa anazozisafirisha zinapendwa sana nchini Mauritania.

Mkoa huo umeweka mazingira mazuri kwa wageni na wenyeji kufanya biashara mkoani humo. Kwenye mji wa Yiwu ambao una soko maarufu la biashara ya bidhaa ndogondogo duniani, hali motomoto ya biashara inaonekana kwenye soko hilo na kwenye sehemu za mji huo. Tuliweza kuwaona watu kutoka mataifa na mabara mbalimbali wakiangalia bidhaa kwenye soko hilo, na jioni kwenye sehemu za burudani waarabu wengi wanaoishi na kufanya biashara huko wanaoneka, na kuhisi kama nimefika kwenye nchi ya kiarabu. Ofisa wa habari wa serikali ya mji wa Yiwu Bw Yu Wei Yi, alituambia kuwa kuna wageni zaidi ya 4,500 wanaoishi kwenye wilaya hiyo kwa muda mrefu, na kati ya hao wafanyabiashara kutoka Korea ya kusini ni zaidi ya 3000.

Kila siku makontena zaidi ya 1000 yenye bidhaa ndogondogo zinazonunuliwa na wafanyabiashara kutoka nje yanasafirishwa kupelekwa nje ya nchi.

Wafanyabiashara wawili, mmoja kutoka India na mwingine kutoka Pakistan walikuwa ni mashahidi wa hali halisi ya biashara mkoani humo. Mfanyabiashara kutoka India alisema India ni nchi yenye uwezo wa kuzalisha wanakampuni wengi hodari, lakini kwa bahati mbaya si nchi yenye makampuni makubwa hodari, na badala yake wanakampuni wa India wanakwenda kwenye nchi zenye mazingira mazuri zaidi kibiashara ambako wanaweza kuanzisha makampuni yao. Alisema yeye ameweza kuanzisha kampuni yake kubwa mkoani Zhejiang kutokana na sera nzuri za kibiashara na msaada mkubwa wanaoupata kutoka kwa uongozi wa Chama na serikali mkoani huo.

Pamoja na maendeleo makubwa yaliopatikana mkoani humo, hali ya kutokuwepo kwa uwiano wa maendeleo kwenye mkoa huo pia inaonekana wazi. Pamoja na kuwa hali ya baadhi ya miji ya Zhejiang inafanana na miji mikubwa ya China na hata ya nchi za nje, vile vile kuna miji ambayo iko ambayo bado iko nyumba kimaendeleo. Pengo la maendeleo kati ya miji iliyoendelea na vijiji mkoa ni humo ni kubwa sana, na kutokana na jinsi miji na wilaya zinavyozidi kuendelezwa kuwa za kisasa na za kimataifa zaidi, pengo hilo ndio linazidi kuwa kubwa zaidi.

Lakini hata vijiji hivyo ambavyo viko nyuma sana kimaendeleo kuliko miji ya mkoa huo, vinaonekana kuwa vinapata maendeleo taratibu na hata wakazi wake wanaonekana kuwa na matumaini makubwa ya kuwa na maendeleo katika siku za baadaye. Kwenye vijiji tulivyotembelea pamoja na kuona hali duni ya miundo mbinu, watoto wa vijiji hivyo wanaonekana wenye afya na wachangamfu, wanaonesha kuwa hawana tatizo la upungufu wa chakula, wanaweza kwenda shule, na wanaweza kupata huduma nyingine muhimu za kijamii karibu na maeneo wanayoishi. Hata baadhi ya watu tuliofanikiwa kufanya mahojiano nao, walionesha kuridhishwa na mwenendo wa maendeleo yao.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-10