Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-11 15:41:15    
Baraza la Usalama laendelea kujadili hatua gani zitakazochukuliwa dhidi ya Korea ya Kaskazini

cri

Nchu tano wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na mjumbe wa Japan tarehe 10 waliendelea kufanya mkutano wa faragha kujadili hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Korea ya Kaskazini. Mjadala huo unahusu mswada wa azimio uliotolewa na Marekani. Kutokana na kuwa mswada huo unahusisha vikwazo vingi, pande mbalimbali ziko makini kuhusu misimamo yao na hata zinataka kuwasiliana vya kutosha baina yao, kwa hiyo muda wa mjadala huo umekuwa mrefu, na bado haijafahamika lini mswada huo utapigwa kura.

Habari zinasema mswada huo ulioandaliwa na Marekani umekusanya mambo 13 yakiwa ni pamoja na kuweka vikwazo vya silaha kwa Korea ya Kaskazini na kupiga marufuku kwa biashara ya nyenzo zote zinazoweza kutengenezwa kuwa silaha kali, kuzuia akaunti zote zinazohusu miradi ya silaha za nyuklia na noti bandia, na kupiga marufuku kuiuzia Korea ya Kaskazini vitu vya anasa. Mswada huo pia unataka kukagua meli zote zinazoingia na kutoka nchini Korea ya Kaskazini ili kuzuia kusafirisha au kuuza nyenzo zinazohusu silaha za nyuklia.

Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Bw. John Bolton alisema kwa sababu hivi sasa mwakilishi wa Russia bado hajapata maagizo kutoka serikali yake, kwa hiyo pande mbalimbali hazijaweza kujadili vilivyo mswada huo. Lakini alisema China na Marekani zimebadilishana vizuri maoni, hilo ni jambo muhimu sana. Aliongeza kuwa Marekani inataka azimio liwe kali na litekelezwe haraka. Bw. John Bolton alisema pande mbalimbali zinatumai kuwa mjadala huo utaharakishwa na kuafikiana kwa azimio.

Mwenyekiti wa mwezi huu wa Baraza la Usalama ambaye ni mwakilishi wa Japan kwenye Umoja wa Mataifa Bw. Kenzo Oshima kwenye mkutano na waandishi wa habari alifahamisha kuwa, kitu kinachozungumzwa zaidi kwenye mdahalo huo, ni hatua ya kutumia nguvu za kijeshi kwa mujibu wa kipengele cha saba cha Katiba la Umoja wa Mataifa. Kuhusu hatua hiyo pande mbalimbali bado hazijaafikiana, lakini alisema kwa kufanya majadiliano misimamo na malengo ya pande mbalimbali yamekuwa wazi.

Kipengele cha saba cha Katiba la Umoja wa Mataifa kinasema, ili kulinda amani ya dunia Baraza la Usalama linaweza kuruhusu kutumia nguvu za kijeshi kwa vitendo vyote vinavyoleta tishio kwa amani na usalama. Kutokana na sababu hiyo, pande mbalimbali zimekuwa na makini sana kuonesha misimamo yao. Baada ya Korea ya Kaskazini kufanya majaribio ya makombora mwezi Julai mwaka huu Baraza la Usalama lilipojadili azimio dhidi ya Korea ya Kaskazini pia yalitokea maoni tofauti kuhusu kutumia kipengele cha saba, na baada ya pande mbalimbali kujadiliana vya kutosha mwishowe hatua ya kutumia nguvu za kijeshi ilifutwa kutoka kwenye azimio na zilibaki shutuma tu kwa Korea ya Kaskazini na kuitaka nchi hiyo isimamishe shughuli zote za kutengeneza silaha za nyuklia na kupiga marufuku kwa msaada wa nyenzo za kutengenezea silaha hizo kutoka nchi za nje. Wachambuzi wanaona matokeo ya azimio litalalopatikana katika Baraza la Usalama litafanana na lile la safari iliyopita, yaani kuweka vikwazo vya kiuchumi bila kutumia nguvu za kijeshi.

Mwakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa Bw. Wang Guangya siku hiyo kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema msimamo wa kimsingi wa China kuhusu hatua dhidi ya Korea ya Kaskazini ni kuiadhibu vikali, lakini hatua za adhabu ziwe mwafaka, na pia alisema mswada wa Marekani kimsingi ni mzuri na unafaa kutekelezwa, lakini unahitaji kujadiliwa vya kutosha na pamde mbalimbali.

Wizara ya mambo ya nje ya China katika siku hiyo pia ilisisitiza kwamba katika wakati kama huo pande mbalimbali zinapaswa ziwe na akili tulivu kukabiliana na hali hiyo ngumu, kitu muhimu ni kuhakikisha kutokuwa na silaha za nyuklia katika peninsula ya Korea na amani na utulivu wa sehemu ya Asia ya Kaskazini na Mashariki.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-11