Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-12 16:12:45    
Mafanikio yaliyopatikana mkoani Guangxi, China katika kuondoa umaskini yawavutia maofisa wa nchi za Afrika

cri

Mwezi Julai mwaka huu wageni kutoka Afrika walitembelea vijiji vya mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guangxi, China. Waafrika hao walizungumza na wakulima wa huko, kutembelea mashimo ya kuzalisha gesi ya kinyesi na kujaribu wenyewe kuwasha moto kwenye jiko linalotumia gesi ya kinyesi. Wao ni maofisa waandamizi 18 wanaoshughulikia kazi za kuondoa umaskini kutoka nchi 12 za Afrika, walioshiriki kwenye semina kuhusu sera na hatua za kuondoa umaskini iliyoandaliwa na serikali ya China, na safari hiyo walifanya ukaguzi katika mkoa wa Guangxi uliopo kusini magharibi ya China.

Bw. Kreshna N. Bunjun kutoka Mauritius alisema katika ziara hiyo mkoani Guangxi, alishuhudia jinsi vijiji vya China vilivyoimarisha ujenzi wa miundo mbinu, kutumia ipasavyo raslimali ya nguvu kazi na raslimali nyingine katika kubadilisha hali duni ya vijijini, na kueneza teknolojia ya matumizi ya gesi ya kinyesi ambayo imewanufaisha sana wakulima. Aliongeza kuwa kuna shughuli nyingi ambazo China na Afrika zinaweza kufanya ushirikiano.

Kama mnavyojua China ni nchi yenye idadi kubwa ya wakulima, na watu maskini wengi wanaishi vijijini. Katika miaka zaidi ya 20 iliyopita, China ilipata mafanikio makubwa katika kupunguza idadi ya watu maskini, na mkoa wa Guangxi uliopo kusini magharibi ya China ni mfano mzuri. Takwimu zinaonesha kuwa, katika kati ya mwaka 2000 na 2005 pekee idadi ya watu maskini mkoani humo ilipungua kutoka milioni 1.5 hadi laki 8.6.

Basi je, Guangxi ilitumia mbinu gani? Mkurugenzi wa ofisi ya uongozi wa kupambana na umaskini ya mkoa huo Bw. Hu Decai alieleza kuwa, ujenzi wa miundo mbinu ya vijijini zikiwemo barabara na zana za maji ulipewa kipaumbele. Alisema"serikali inatoa misaada na wanavijiji wenyewe wanashiriki kwenye ujenzi huo. Kwa mfano kwenye ujenzi wa barabara, serikali inatoa baruti, saruji na nondo, huku wanavijiji wanashiriki kwenye ujenzi."

Kutokana na hali duni ya elimu ya wakulima maskini, mkoa wa Guangxi uliimarisha kazi ya kuwapa mafunzo. Mafunzo hayo ni pamoja na teknolojia za kilimo na ufugaji, na ufundi wa viwandani.

Katika kupambana na umaskini kuna hatua moja yenye umaalumu wa China, yaani kushirikisha jamii ili watu wasaidiane na kupata maendeleo ya pamoja. Kwa mfano hivi sasa bado kuna vijiji yenye umaskini vipatavyo 4,060, kazi ya kuondoa umaskini kwenye kila kijiji kimoja inafuatiliwa na kada fulani wa serikali au idara fulani ya serikali, hata kila familia maskini inasaidiwa moja kwa moja na watumishi wa serikali.

Mbali na hayo Bw. Hu Decai alizungumzia suala la matumizi ya wazi ya fedha za misaada, akisema mkoa wa Guangxi umeandaa na kufuata kwa makini utaratibu mkali ili kuhakikisha kuwa fedha hizo zote zinatumika kuwanufaisha wakulima maskini.

Alisema  "Fedha za misaada ni fedha zinazoweza kuokoa maisha ya watu maskini. Idara za serikali zinabeba wajibu wa kusimamia matumizi ya fedha hizo, na hizi si pesa zetu."

Ofisa huyo alieleza kuwa, katika mkoa wa Guangxi fedha za misaada zinagawanywa kwa mujibu wa miradi mbalimbali ya kuondoa umaskini ambayo inaamuliwa na wakulima maskini wenyewe. Aidha fedha hizo zinahifadhiwa kwenye akaunti maalumu, na matumizi yake yanafanyiwa ukaguzi kwa makini kila mwaka. Matokeo ya ukaguzi yanatangazwa hadharani kwa jamii ili matumizi ya fedha za misaada yawe chini ya usimamizi wa wananchi.

Hatua hizo zimekuwa na matokeo mazuri. Bw. Hu Deguang alisema  "Katika miaka ya karibuni hakutokea kashfa za ufisadi au matumizi mabaya ya fedha za misaada katika mkoa wa Guangxi."

Mafanikio katika kupunguza idadi ya watu maskini na rekodi nzuri ya usimamizi wa fedha za misaada ililetea mkoa wa Guangxi misaada ya kigeni ya dola karibu milioni 20 za kimarekani tangu katikati ya miaka ya 90 mpaka hivi sasa.

Miaka 10 iliyopita, mkulima Lan Hualin alikuwa hana chochote isipokuwa nyumba moja iliyojengwa kwa nyasi. Wakati huo familia yake yenye watu watano iliishi katika sehemu ya milima ni yenye mawe, ambapo mbali na mawe hakuna shamba wala barabara au miundo mbinu mingine. Familia hiyo ilitegemea kulima mahindi kati ya nyufa za mawe. Kwa hiyo wakati serikali ilipowahamasisha wahamie kwenye sehemu nyingine yenye mashamba, Bw. Lan Hualin aliitikia mwito huo kwa furaha.

Kila familia iliyohiari kuhama ilipata misaada ya pesa na mashamba yenye ukubwa wa hekta 1.3 kutoka kwa serikali. Hivi sasa bwana huyo na mke wake pia wamekodi shamba lingine lenye ukubwa wa hekta 0.7, wakilima mahindi, mihongo na matunda. Aidha familia hiyo inafuga ng'ombe watano na nguruwe 30. Hivi sasa familia hiyo ina pato la Yuan zaidi ya elfu 30 kwa mwaka na kujenga nyumba mpya. Bw. Lan Hualin alifurahi na kusema  "Sasa maisha yetu yameboreshwa. Zamani tuliweza kula nyama mara moja tu kwa mwezi, lakini hivi sasa tunakula nyama kwenye kila mlo wa jioni na kunywa pombe kidogo. Sasa nimezoea sijisikii vizuri kama sijala nyama wala kunywa pombe hata kama ni kwa siku moja tu."

Kijiji cha Nawo wanakoishi Bw. Lan Hualin na familia yake kiliundwa na wakulima waliohiari kuhama kutoka sehemu zenye hali mbaya ya kimaumbile. Tangu mwaka 1995 wakulima 525 wa familia 52 walihamia huko, na hivi sasa wote wameondokana na umaskini, na familia nyingi zimejenga nyumba mpya. Katika nyumba ya familia moja kijijini humo, bendi iliyoundwa na wanakijiji inafanya mazoezi, ambapo mkulima mmoja wa kike anaimba wimbo unaojulikana sana nchini China uitwao "siku njema".

Idhaa ya kiswahili 2006-10-12