Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-12 16:21:19    
Kijana aliyeendesha baiskeli ya magurudumu matatu

cri

Tarehe 5 Julai mwaka 2006 ilikuwa ni siku maalumu kwa Bw. Chen Ping mwenye umri wa miaka 40, kwani katika siku hiyo alipata barua inayomwarifu kuwa amefaulu mitihani ya kusoma shahada ya pili. Bw. Chen Ping ambaye anafanya kazi ya kuendesha baiskeli ya magurudumu matatu inayobeba abiria, amekuwa akifanya bidii kutimiza lengo hilo katika miaka 20 iliyopita.

Siku moja mwezi Aprili mwaka huu, katika mtihani wa duru la pili wa kuingia chuo cha shahada la pili katika chuo kikuu cha Yunnan, China, mtu mmoja aliyeshiriki kwenye mtihani huo aliwavutia walimu kutokana na umri wake mkubwa zaidi kuliko wenzake. Profesa Lin Chaomin wa chuo kikuu hicho alikumbusha akisema "Nilimwuliza maswali kadhaa. Alionesha uhodari katika taaluma yake. Alionekana ni mtu mwenye matumaini, nilivutiwa na tabia yake hiyo pamoja na moyo wake wa kufanya bidii na ushujaa wa kukabiliana na hali ngumu."

Mtu huyo aliyesifiwa sana na profesa Lin ni Bw. Chen Ping. Baada ya mtihani huo wa mahojiano, Bw. Chen Ping alipata barua ya kujiunga kwenye masomo ya shahada ya pili katika chuo kikuu cha Yunnan. Lakini kabla ya hapo alikuwa anafanya kazi ya kubeba abiria kwa baiskeli ya magurudumu matatu kwa miaka 6 huko Jiutai, mji mdogo wa mkoa wa Jilin, kaskazini mashariki mwa China.

Mwaka 1986 Chen Ping alishindwa kwenye mitihani ya kujiunga na chuo kikuu. Tukio hilo lilikuwa pigo kubwa kwake, na kuanzia hapo alijiwekea lengo moja kubwa zaidi, yaani kufaulu mitihani ya kujiunga na masomo ya shahada ya pili.

Mchakato wa kutimiza lengo hilo ulikuwa mrefu na ulikuwa na matatizo. Familia ya Chen Ping ilikuwa haina uwezo mkubwa, ilimbidi aendelee na masomo na kufanya kazi kwa wakati mmoja. Ingawa alikuwa anafanya bidii sana, lakini ilikuwa si rahisi kufaulu mitihani ya kusoma shahada ya pili, kijana huyo alikuwa anashindwa mara kwa mara kwenye mitihani hiyo.

Wakati huo huo alikuwa anakumbwa na matatizo mengine. Mwaka 2000 Chen Ping alipoteza ajira yake kutokana na kufilisika kwa kiwanda alichofanya kazi. Aliamua kujipatia pesa kwa kuwa dereva wa baiskeli yenye magurudumu matatu inayobeba abiria. Mwanzoni alipojishughulisha na kazi hiyo, alikuwa anaona aibu. Katika siku hizi kijana huyo amekuwa akijaribu kutafuta nafasi nyingine za ajira nzuri zaidi, lakini aliamua kuziacha kutokana na kushindwa katika masomo. Siku nenda siku rudi, Chen Ping alikuwa anapata ufanuu wa kazi hiyo ya kubeba abiria kwa baiskeli ya magurudumu matatu kwamba, aliweza kuchuma pesa na kuwa na muda mwingi zaidi wa kusoma, ili atimize haraka lengo lake la kujiunga na masomo ya shahada ya pili.

Bw. Chen Ping alisema "Kama hakuna wateja waliopanda baiskeli yangu, nilikaa karibu na baiskeli nikisoma vitabu. Hatua kwa hatua nilianza kufuata utaratibu fulani, yaani wateja wakija niliwahudumia, ama sivyo nilisubiri kando ya baiskeli huku nikiishika baiskeli kwa mkono mmoja na mkono mwingine nikiwa na kitabu, ambapo baiskeli ikiguswa na wengine, nilifahamu kuwa wateja walikuja, hivyo nikawachukua."

Bw. Chen Ping alikuwa anasoma kwa bidii, hali ambayo ilijulikana miongoni mwa wenzake waliofanya kazi ya kuendesha baiskeli ya magurudumu matatu. Mwenzake Bw. Zhang Baoguo alisema "Nimemfahamu kwa miaka 6. Alikuwa anasoma huku akifanya kazi hiyo ya kuendesha baiskeli ya magurudumu matatu, alikuwa anasoma mahali popote alipokwenda na baiskeli yake. Siku nyingine hata kama wateja walikuwa wameshapanda baiskeli, yeye alikuwa akiendelea kusoma. Kwa kawaida alimaliza kazi saa 4 usiku, hivyo mara kwa mara alikuwa anasoma chini ya taa za barabarani."

Kutokana na makadirio ya Bw. Chen Ping mwenyewe, katika miaka hiyo 6 iliyopita alikuwa amewahudumia wageni elfu 30 hivi na kupata Yuan elfu 40 kwa ajili ya familia yake yenye watu watatu. Mbali na moyo wa ushujaa wa kukabiliana na hali ngumu, jamaa zake pia walimpa uungaji mkono mkubwa.

Hata hivyo mke wake Bibi Liu Jing alisema kuwa aliwahi kuwa na malalamiko. Alisema "Niliona kuwa siwezi kuvumilia. Alishindwa kwenye mitihani mara kwa mara, baada ya kujulikana kwa matokeo ya mitihani aliwahi kulia, ambapo nilimwuliza, kwa nini unashikilia njia hiyo tu?"

Bw. Chen Ping ana jibu lake kwa hoja ya mke wake, alisema  "Naona siwezi kufikiri mambo mengi. Niliposhindwa nilijiwaza kwa nyimbo. Kwa kawaida nilikuwa sina muda wa kulia na wa kufikiria kushindwa, bali nilikuwa nasonga mbele."

Watu walikuwa na maoni tofauti kuhusu Bw. Chen Ping. Baadhi ya watu walimkosoa kuwa miaka 20 ni muda mrefu unaothaminiwa, ni afadhali autumie vizuri zaidi. Watu wengine walieleza kumwunga mkono.

Licha ya maoni hayo, Chen Ping mwenyewe alikuwa tayari kwenda kujiandikisha kwenye chuo kikuu cha Yunnan. Alimwambia mwandishi wa habari kuwa, hakutarajia maisha yake yabadilike kutokana na kufaulu mitihani ya kujiunga na masomo ya shahada ya pili, alitaka tu kutimiza lengo aliloweka. Na baada ya kuhitimu masomo ya shahada ya pili, kama hataweza kupata nafasi nzuri ya ajira, atarudi nyumbani kuendelea na kazi ya kuendesha baiskeli ya magurudumu matatu inayobeba abiria.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-12