Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-13 16:18:47    
Meneja mkuu wa shirika la utangazaji wa Kenya KBC Bwana David Waweru afanya ziara katika CRI

cri
Kuanzia tarehe 25 hadi 30 Septemba mwaka 2006, meneja mkuu wa shirika la utangazaji wa Kenya KBC Bwana David Waweru anafanya ziara hapa Beijing China , hii ni mara yake ya kwanza kuja China kwa matembezi, na kuwa mgeni wa studio ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa CRI

CRI: Najua hii ni mara yako ya kwanza kufika China , unaweza kutuambia jinsi unavyoiona China . Kabla hujafika China ulikuwa na picha gani kuhusu China ?

Waweru: Kimsingi kabla sijafika China nilikuwa nafikiria pengine Beijing ni mdogo kama ule wa Nairobi, au mkubwa kidogo tu kuliko Nairobi, lakini nimeona maajabu kidogo ni mji mkubwa kweli, mji wa zamani, nimeona mambo ya zamani.

CRI: Umekaa hapa Beijing kwa siku chache tu, unaonaje vyakula vya hapa Beijing ukilinganishwa vyakula ambavyo umevizoea kule nyumbani?

Waweru: Kitu cha kwanza na mambo muhimu sana ni pilipili, kama wewe upendi pilipili ama spicis pengine hutafurahia chakula cha hapa China . Lakini mimi mwenyewe nimekuwa nikienda mikahawa ya kichina kule Nairobi na Dar es Salaam , kwa hivyo nimezoea kidogo mambo ya chakula cha kichina. Lakini nikija hapa siku moja nilikula chakula pilipili kabisa, nafikiri ilikuwa ni pilipili tupu, lakini nilifurahia hata hivyo.

CRI: Sasa tuzungumzie kidogo maswala ya utangazaji, nadhani wewe ndio mkurugenzi mtendaji wa KBC, na tuna ushirikiano wa kurusha matangazo na KBC, unaonaje ushirikiano kati ya KBC na CRI?

Waweru: Kabla niingie hapa China , mimi nilikuwa nauona tu ule mkataba kama ni kazi ya biashara, lakini nilipoingia hapa nikaona Kenya na Uchina kuna mambo mengi sana wanaweza kushirikiana, na pia ukienda mitaani hapa Beijing utaona watu wengi sana , hawafahamu Kiswahili. Na kulingana na ile biashara ya ulimwenguni, wakenya wanaweza kufaidika sana na biashara na utalii kutoka kwa China . Mimi nafikiria matangazo ya Radio China Kimataifa yataboreshwa zaidi ili watu wanaweza kufahamu mambo mengi ya China ya kibiashara, kitalii, na ya masomo, hata kujionea ulimwengu na mambo ya kiteknolojia. Watu walikuwa wakifikiria mambo ya China ni ya zamani na ya chini, lakini ukiangalia huku utaona vyombo vingi vya China vimeendelea sana kama vya nchi nyingine ulimwenguni, pengine bei yao ni nafuu kidogo. Kwa hivyo, mimi naona matangazo yenu ya pale tujaribu kuyaboresha, tujaribu kufuatilia watu wengi waweze kuyasikiliza. Na sisi KBC pia tutajaribu kutangaza na kuwaelezea wasikilizaji wetu ili waweze kutega matangazo yenu wakiwa wengi.

CRI: Sehemu moja ya ushirikiano kati ya CRI na Kenya ni kujaribu kuwafanya wakenya waifahamu China vizuri zaidi na kujaribu kuwafanya wachina waifahamu Kenya vizuri zaidi. Unadhani kwamba sasa hivi wakenya wanaifahamu China vizuri au bado wana mawazo ya zamani kuhusu China ?

Waweru: Ningeanza kusema kwamba mawazo ni yale yale ya zamani, lakini kwa sababu ya ushirikiano ule umekuwepo, naona watu kama wako mijini wameanza kujua mambo ya Uchina kidogo, hata ukienda kule vijijini ama miji midogo midogo pia watu wanaweza kununua bidhaa kutoka China . Lakini watu wengi bado wanafikiria Uchina ni vile vilikuwa zamani kutokana na propaganda kutoka nchi nyingine. Kwa hivyo uelewano unakuwepo, lakini bado unahitaji juhudi za serikali zetu mbili.

CRI: Ingawa wewe si mtu wa mambo ya biashara unaweza kuzungumzia kidogo kuhusu mambo ya biashara kati ya China na Kenya ?

Waweru: Nikianza kwanza kusema kwamba, watu wa Kenya wameanza kuja China hata kule Guangzhou , biashara imeongezeka,watu wengi wanapenda kuja hapa kuangalia biashara. Zamani walidhani bidhaa za China hazina ubora kama zile za nchi nyingine. Lakini ukija hapa utaona ni tofauti na vile watu walivyofikiria. Kwa hivyo mimi naona wale wakenya wanaweza kuingia hapa Uchina na kutafuta na kununua bidhaa ambazo zinaweza kuwaletea manufaa, lakini itawabidi pia waelimishwe kuhusu ubora wa bidhaa za China, kwa sababu watu wengi bado wanafikiria ubora wa bidhaa kutoka China ni chini.

CRI: na kutokana na hayo unaonaje matangazo yetu ya Radio China Kimataifa kama ni daraja la kuongeza maelewano, hata kuongeza ufahamu wa watu wa Kenya juu ya China ?

Waweru: Tumepata kuongea na wakurugenzi wa CRI kuhusu vile tunaweza kuboresha vipindi ili matangazo yenu yawe yanawalenga wengi wenye biashara, wenye kufuatilia masomo, na pia watu katika serikalini waweze kusikiliza na kuelewa vile Uchina inaweza kusaidiana na Kenya kuendeleza ushirikiano na pia biashara katika nchi hizo mbili. Mimi naona vile tutafanya nikirudi kule Nairobi ni kushirikiana na watangazaji wenu walioko huko Nairobi tuangalie vipindi vyenu, na tuone jinsi gani na mikakati gani tunaweza kuweka ili vipindi vyenu vionekane wakati tunavirusha hewani watu wengi wanaweza kuvisikiliza. Na mimi naona bila shaka tutafanikiwa, na mwaka ujao watu wengi zaidi watapendelea kusikiliza matangazo yenu.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-13