Huu ni mwaka wa 50 tangu uhusiano wa kibalozi kati ya China na Afrika uanzishwe. Ili kuimarisha urafiki wa jadi, China na Afrika zitafanya mkutano wa viongozi wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika mjini Beijing kuanzia tarehe 3 hadi 5 mwezi Novemba. Siku chache zilizopita, mwandishi wetu alizungumza na balozi wa China nchini Misri Bw. Wu Sike, ifuatayo ni ripoti aliyotuletea.
Tarehe 30 Mei mwaka 1956 Misri ilianzisha uhusiano wa kibalozi na Jamhuri ya Watu wa China iliyoanzishwa muda mfupi na kuwa nchi ya kwanza ya Kiarabu na ya Afrika kuitambua China mpya. Kuhusu historia hiyo Bw. Balozi Wu Sike alisema, "Kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya China na Misri ni jambo muhimu katika historia ya diplomasia ya China. Kuanzishwa kwa uhusiano huo pia kunamaanisha kuwa uhusiano kati ya China na Afrika na nchi za Kiarabu uliingia katika kipindi kipya, kwa hiyo maadhimisho ya miaka 50 tangu China na Misri zianzishe uhusiano wa kibalozi pia ni maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Afrika na vile vile ni maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na nchi za Kiarabu."
Katika miaka 50 iliyopita, urafiki kati ya China na nchi za Kiarabu unaendelea kwa kina siku hadi siku. Mwaka 1999 pande mbili ziliafikiana kimawazo kuanzisha ushirikiano wa kiwenzi na kimkakati. Wakati tunaposherekea maadhimisho ya miaka 50 waziri mkuu Wen Jiabao wa China kwa mara ya kwanza alifanya ziara nchini Misri na alipeleka uhusiano kati ya nchi hizo mbili kwenye kipindi kipya. Katika mambo ya siasa, China na Misri zinaaminiana, katika mambo ya biashara pande mbili zinashirikiana na kunufaishana. Balozi Wu Sike alitueleza kwa mfano kuhusu ushirikiano wa biashara, alisema, "Nakumbuka kwamba waziri mkuu Ahmed Nazif wa Misri alitaja mara kadhaa kwamba alipokuwa waziri wa mawasiliano ya habari alianzisha ushirikiano na mashirika ya China katika mambo ya upashanaji habari, lakini kutokana kutofahamu sana hali ilivyokuwa ya China watu wengi wa Misri walikuwa na wasiwasi. Nikiwa waziri wa mawasiliano ya habari nilishikilia ushirikiano huo, baadaye ukweli umethibitisha kwamba sikukosea kuchagua ushirikiano huo ambao umetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya upashanaji habari nchini Misri. Na ushirikiano huo pia umeyaletea manufaa mengi mashirika ya China. Kwa hiyo ushirikiano huo ni wa manufaa kwa pande mbili."
Ushirikiano katika nyanja ya utamaduni pia ni mkubwa. Bw. Wu Sike alisema, "China na Misri zote ni nchi zinazotilia maanani utamaduni na zinatetea maingiliano ya utamaduni wa aina tofauti na kupinga msimamo kuwa utamaduni wa aina tofauti huleta mgongano. Kwa hiyo maingiliano ya utamaduni kati ya nchi mbili yanaimarika sana. Pande mbili ziliwahi kufanya wiki ya filamu, utamaduni na maonesho katika kila nchi."
Bw. Wu Sike alisema, rais Hosni Mubarak wa Misri atahudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika. Akiwa kiongozi mwenye heshima kubwa katika Mashariki ya Kati na hata katika jumuyia ya kimataifa kushiriki kwake kutakuwa na umuhimu kwa mkutano huo. Balozi huyo pia alidokeza kuwa rais Mubarak atatembelea China kwa mara yake ya tisa. Kuhusu uhusiano kati ya China na Misri Bw. Wu Sike alisema, "Uhusiano kati ya nchi mbili una msingi imara kabisa, na uhusiano huo unaweza kuelezwa kuwa ni wa marafiki, wenzi na ndugu, na uhusiano huo unafaa kuwa mfano wa kuigwa katika ushirikiano kati ya China na nchi zinazoendelea."
Idhaa ya kiswahili 2006-10-17
|