Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-18 19:06:50    
Teknolojia ya tarakimu yarahisisha maisha ya wakazi wa Beijing

cri

Labda wakazi wengi wa Beijing walikuwa wanasubiri kwa muda mrefu kwenye foleni katika benki ili waweze kulipa bili mbalimbali, hivi sasa kama wanataka kulipa bili ya simu, hawana tena haja ya kusubiri kwenye foleni, wanapigia simu benki tu na kulipa bili hiyo kwa kutumia kadi za benki. Aidha, kuanzia mwezi Julai mwaka huu, huduma hiyo itapanuliwa zaidi, bili mbalimbali zikiwemo bili za simu, mtandao wa Internet, televisheni ya kebo na kodi za magari na meli zitaweza kulipwa kwa njia ya mtandao wa Internet, simu au kwenye vituo vya viunganishio vya moja kwa moja vya mtandao wa huduma hiyo vilivyowekwa kwenye sehemu mbalimbali za mijini na vijijini. Vituo zaidi ya 2300 vya huduma hiyo vimesambaa katika benki za vitongoji vya Beijing, maduka, majengo ya ofisi na sehemu za makazi kote mjini Beijing. Kwenye vituo hivyo, huduma hiyo ni ya saa 24 na inapokea kadi za benki mbalimbali. Mkazi wa Beijing Bi. Cao Feng alisema:

"huduma hiyo imetuletea urahisi sana, hatuna haja tena kwenda nje au kusubiri kwenye foleni kushughulikia mambo hayo, na inachukua dakika chache tu. Maisha yamekuwa rahisi zaidi."

Miaka minane iliyopita, makamu wa rais wa zamani wa Marekani Bw. Al Gore alifahamisha wazo la "dunia ya kitarakimu". Kutokana na kuendelezwa na nchi mbalimbali, wazo hilo linalohusisha fani mbalimbali za ujenzi wa miji linajumuisha kwa ufanisi taarifa kuhusu ujenzi wa miundo mbinu, uchumi, utamaduni, elimu, usalama na kutoa huduma ya jumla kwa sekta mbalimbali za miji. Hivi sasa, miji karibu 40 ya China imetoa mpango wa ujenzi wa miji ya kitarakimu, na miongoni mwa miji hiyo, Beijing ya kitarakimu inafuatiliwa zaidi.

Tovuti ya serikali ya mji wa Beijing inayoitwa E-Beijing inawakilisha umaalum wa mradi wa ujenzi wa Beijing ya kitarakimu. Kwa kupitia tovuti hiyo, serikali ya Beijing inaweza kutoa taarifa za kiserikali. Aidha, tovuti hiyo inaunganishwa na tovuti nyingine za huduma za umma ili kuwawezesha wakazi wa Beijing kushughulikia mambo mbalimbali kwenye mtandao. Mbali na matumizi ya mtandao wa Internet, serikali ya mji wa Beijing pia imejenga kituo maalum cha uongozaji na mfumo wa kukabiliana na hali ya dharura, ili kuinua ufanisi wa kushughulikia matukio ya dharura.

Wakati wa kutoa mapendekezo kwa ujenzi wa miji ya kitarakimu, mkurugenzi wa taasisi ya maendeleo ya miji na mambo ya kitarakimu mijini katika chuo kikuu cha Beijing Profesa Kou Youguan aliona kuwa, jambo muhimu na la msingi kwa mradi wa miji ya kitarakimu ni kuzifanya taarifa mbalimbali ziweze kutolewa kwa matumizi ya pamoja. Profesa Kou Youguan alisema:

"ujenzi wa miji ya kitarakimu unalenga kusimamia taarifa za habari mijini na kuzifanya taarifa hizo ziwe chini ya udhibiti, na tuweze kuzitumia kwa maendeleo mazuri. Kwa mfano, hospitali inahitaji taarifa kadhaa binafsi za wagonjwa, na taarifa hizo zinapatikana katika idara husika ya usimamizi wa ukazi katika idara ya usalama wa umma. Kama taarifa hizo zitaweza kutolewa na kubadilishana, zitaleta manufaa makubwa kwa jamii."

Mwaka 2002, mji wa Beijing uliweka vibanda kumi kadhaa vya huduma za taarifa za mijini, ili kuwawezesha wakazi watafute taarifa mbalimbali. Baada ya hapo, mji huu ulitumia yuan milioni kumi kadhaa kurekebisha vibanda hivyo viwe vya kisasa zaidi. Baada ya marekebisho hayo, vibanda hivyo vina sura ya kupendeza zaidi, pia vimeongeza uwezo wa kununua tikiti mbalimbali, zikiwemo tikiti za sinema na tikiti za simu.

Mbali na vifaa mbalimbali, sekta ya software ya China pia ilitoa uungaji mkono wa software katika maeneo ya udhibiti kwa kujiendesha, upashanaji wa habari, teknolojia ya mtandao wa internet na televisheni ya kitarakimu. Software ya Ezone yenye hakimiliki iliyotolewa na kampuni ya Qinghuatongfang inatoa chombo cha jumla kwa software mbalimbali katika mradi wa miji ya kitarakimu, software hiyo inaunganisha vifaa mbalimbali vya kielektroniki kwa njia mbalimbali za mawasiliano, na kutimiza lengo la usimamizi wa jumla na huduma kwa sekta mbalimbali mijini. Meneja wa idara ya ushirikiano wa teknolojia ya kampuni ya Qinghuatongfang Bi. Zhao Ying alieleza:

"siku hizi watu wanauliza kuwa software zinaweza kufanya nini na zinaweza kufanya nini kwa jamii? Na lengo la software yetu ya Ezone ni kujenga mji wa kitarakimu. Tunataka kutumia chapa hiyo cha Ezone na uwezo na njia za usambazaji wa bidhaa zake kuhudumia jamii vizuri zaidi."

Katika karne ya 21, teknolojia ya upashanaji wa habari imekuwa moja ya misukumo ya maendeleo ya uchumi na jamii ya mijini. Profesa Kou Youguan anaona kuwa, ujenzi wa miji ya kitarakimu hauwezi kuondokana na upashanaji wa habari, matokeo ya mwisho ya upashanaji wa habari ni kwa ajili ya kuhudumia umma. Profesa Kou alisema:

"ujenzi wa miji ya kitarakimu unaweza kusaidia na kutimiza maendeleo endelevu katika jamii ya kiuchumi na jamii ya binadamu na sekta ya raslimali, na mradi huo ni mkakati muhimu sana. Pia China bado iko kwenye mchakato wa maendeleo, ikilinganishwa na nchi nyingine kadhaa zinazoendelea, China inaendelea kwa kasi zaidi. Kutokana na hali ya hivi sasa ya vifaa na raslimali ya nguvukazi, katika miaka miongo kadhaa ijayo, sekta ya upashanaji wa habari wa miji ya China itapata maendeleo ya kasi zaidi."