Maofisa 18 wa kilimo kutoka nchi za Afrika wanaoshiriki kwenye semika ya teknolojia ya kilimo inayofanyika sasa mjini Beijing wanasema China imefanikiwa kutatua matatizo na masuala mengi ya kilimo yaliyoikabili Afrika, wakitumai China itatume wataalamu wengi zaidi kueneza maarifa barani Afrika.
Ukweli ni kwamba ushirikiano wa kilimo umekuwa sehemu muhimu katika ushirikiano wa mambo yote kati ya China na Afrika. Waraka wa "Sera za China kuhusu Afrika" uliotolewa Januari mwaka huu umesema, China na Afrika zitatilia mkazo kwenye ushirikiano katika kuongeza ardhi ya kilimo, kueneza teknolojia ya upandaji wa mimea ya chakula, ufugaji, usalama wa chakula, mashine za kilimo na usindikaji wa mazao. China imekuwa ikijitahidi kusaidia Afrika kuinua uzalishaji wa mazao, kuboresha maisha na kulikabili kwa pamoja tatizo la usalama wa chakula.
Kilimo kinapewa kipaumbele kati ya sekta zote za maendeleo ya uchumi barani Afrika, ni sekta muhimu katika uchumi wa nchi nyingi za Afrika, na ni msingi kabisa wa maendeleo yote barani Afrika. Lakini kutokana na teknolojia iliyo nyuma na maafa ya maumbile yanayotokea mara kwa mara hali ya kilimo ni duni barani humo. Miongoni mwa Waafrika milioni 860 watu zaidi ya milioni 350 wanaishi chini ya mstari wa umaskini wa kimataita kwa dola moja ya Kimarekani kwa siku.
Naibu mkuu wa Taasisi ya Sayansi ya Kilimo ya China Bw. Zhang Lijian alisema, mpaka sasa nchi nyingi za Afrika bado zinafuata kilimo cha jadi. China pia ni nchi ya kilimo, ina uzoefu mkubwa katika kilimo cha mpunga, ufugaji na kukinga maradhi na wadudu waharibifu, kueneza teknolojia ya China barani Afrika sio tu kunasaidia Afrika kuendeleza kilimo na kutatua tatizo la uhaba wa chakula bali pia kumeipatia China fursa nyingi za kutoa msaada wa kilimo duniani.
Imefahamika kwamba katika miaka ya karibuni kwa njia ya kuwaalika maofisa waje nchini China na kutuma wataalamu katika nchi za nje China imetoa msaada wa teknolojia ya kilimo kwa nchi nyingi za Afrika. Wizara ya kilimo ya China imefanya semina zaidi ya 30 kwa ajili ya maofisa wa kilimo wa Afrika, maofisa zaidi ya 1,000 kutoka nchi zaidi ya 40 za Afrika wamepata mafunzo kuhusu upandaji wa mpunga wenye kabila tofauti, mahindi, kilimo cha ardhi kavu, umwagiliaji usio na ubadhirifu wa maji, mazao ya majini, upimaji wa uwekezaji wa miradi ya kilimo, usimamizi wa mimea ya kilimo na maendeleo ya vijijini.
Isitoshe, kuanzia mwaka 1996, China inajitahidi kutekeleza mpango wa usalama wa chakula uliotolewa na Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa, na imesaini "Mkataba wa Pande
Tatu" wa ushirikiano wa kusini kusini na nchi za Moritania, Ghana, Ethiopia, Mali, Nigeria, Sierra Leone na kutuma wataalamu wengi wa kilimo katika nchi nyingi za Afrika ili kusaidia kuendeleza kilimo na kuwaandaa wataalamu wa kilimo, kwa jumla Chima imewatuma wataalamu karibu 700 barani Afrika.
Bw. Zhang Lijian alisema, China imetoa mchango mkubwa katika utatuzi wa tatizo la chakula barani Afrika. katika muda wa miaka mingi iliyopita China imeanzisha ushirikiano katika nyanja nyingi zikiwa ni pamoja na ufugaji wa funzi-hariri, ufugaji mazao ya majini, umwagiliaji usio wa ubadhirifu wa maji na usimamizi wa mmonyonyoko wa udongo na mabadiliko ya ardhi kuwa jangwa, matumizi ya gesi ya vinyesi, usindikaji wa mazao.
Kuanzia mwaka 1993 mkoa wa Gansu wa China umetoa msaada kwa nchi 19 za Afrika katika teknolojia ya kukinga na kuzuia kubadilisha ardhi kuwa ya mchanga, na teknolojia ya mmomonyoko wa udongo.
|