Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-20 17:08:29    
Mawasiliano ya elimu kati ya China na Afrika yapata maendeleo makubwa

cri

Mawasiliano na ushirikiano kwenye mambo ya elimu kati ya China na nchi za Afrika ni sehemu muhimu ya mawasiliano na ushirikiano wa kielimu kati ya China na nchi za nje, pia ni sehemu muhimu ya uhusiano kati ya China na Afrika.

Hadi leo China imeanzisha mawasiliano kwenye sekta ya elimu na nchi zaidi ya 50 za Afrika, mawasiliano hayo yameendelezwa katika ngazi mbalimbali, sekta mbalimbali na njia mbalimbali kutoka kutuma wanafunzi tu kama ilivyokuwa hapo awali. Naibu mkuu wa idara ya ushirikiano na mawasiliano ya kimataifa ya wizara ya elimu ya China Bwana Liu Baoli hivi karibuni alitoa makala kuhusu hali ilivyo ya mawasiliano na ushirikiano kwenye sekta ya elimu kati ya China na Afrika.

Bw. Liu Baoli alisema tokea miaka ya 50 ya karne iliyopita, ujumbe zaidi ya 100 wa elimu wa China umetembelea nchi za Afrika, na kupokea ujumbe zaidi ya 90 wa elimu kutoka nchi za Afrika. China na Misri zimeweka utaratibu wa kufanya kongamano la elimu la ngazi ya juu mara moja kwa mwaka, na baraza la mawaziri wa elimu kati ya China na Afrika limeweka mazingira mazuri kwa viongozi wa ngazi ya juu wa China na nchi za Afrika kukutana na kubadilishana maoni.

Kutoa udhamini wa masomo wa kiserikali ni hatua muhimu inayochukuliwa na serikali ya China kutoa mafunzo ya utaalamu wa aina mbalimbali kwa nchi za Afrika, hatua hiyo inaendana vizuri na kazi za kidiplomasia za China kwa nchi za Afrika. Baada ya kuasisiwa kwa Jamhuri ya watu wa China, serikali ya China ilitoa udhamini wa masomo kwa wanafunzi kumi kadhaa kutoka Misri, Kenya, Cameroon na nchi nyingine za Afrika. Ilipofika mwishoni mwa mwaka 2005, serikali ya China ilikuwa imetoa udhamini wa masomo wa kiserikali kwa wanafunzi elfu 19 wa nchi zaidi ya 50 za Afrika. Hivi sasa baadhi yao wameshika nyadhifa za juu kama vile spika wa bunge na mawaziri, wengine wanajishughulisha na mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Afrika, ambao wametoa mchango mkubwa katika kuzidisha uhusiano kati ya China na nchi za Afrika.

Jambo la kufurahisha ni kwamba, tangu China ianze kufanya mageuzi na kufungua mlango, mafunzo ya lugha ya kichina katika nchi za Afrika yamepata maendeleo mazuri. Ilipofika mwezi Julai mwaka2005, wanafunzi zaidi ya 6000 wa nchi za Afrika walikuwa wamejifunza lugha ya Kichina, somo la Kichina limeanza kufundishwa katika vyuo vikuu zaidi ya 60 katika nchi zaidi ya 10 barani Afrika, serikali ya China kwa nyakati tofauti imetuma walimu zaidi ya 200 wa lugha ya Kichina katika nchi za Afrika, na kufungua chuo cha Confucius nchini Kenya na katika nchi nyingine za Afrika.

Kutokana na kustawi kwa uchumi na kuinuka kwa hali ya viwanda, baadhi ya nchi za Afrika zinahitaji sana watu wenye ujuzi wa utaalamu wa aina mbalimbali, elimu ya kiufundi ya China inaweza kukidhi mahitaji ya maendeleo ya kiuchumi ya nchi za Afrika, hivyo ushirikiano wa elimu ya kiufundi kati ya China na nchi za Afrika una mustakabali mzuri. Katika miaka ya hivi karibuni China imekuwa ikiimarisha siku hadi siku ushirikiano kati yake na nchi za Afrika katika sekta ya elimu ya kazi za ufundi, kwa mfano imetuma walimu 87 wa ufundi nchini Ethiopia, ambao wamesambaa katika majimbo na miji mbalimbali ya nchi hiyo. Walimu hao kutoka China wametoa mchango wao ipasavyo katika kuhimiza maendeleo ya elimu, utafiti wa kisayansi na uchumi wa jamii wa huko.

Bw. Liu Baoli alisema kabla ya nusu karne iliyopita, serikali ya China ilianza kutuma walimu wanaofanya kazi katika vyuo vikuu na shule za sekondari za nchi za Afrika. Hadi leo serikali ya China imekwishatuma walimu zaidi ya 530 katika nchi 33 za Afrika, na kuanzisha miradi 60 ya misaada ya elimu katika nchi 25 za Afrika, kuzisaidia nchi hizo kujenga maabara 23 za utafiti kuhusu viumbe, kompyuta, kemikali, utunzaji na utengenezaji wa chakula, sanaa ya bustani na miradi ya majengo. Tokea mwaka 1998 serikali ya China ilipoandaa semina ya kwanza kwa nchi za Afrika, serikali ya China kwa nyakati tofauti imeandaa semina 39 kwa nchi za Afrika kuhusu usimamizi wa elimu ya juu, utoaji elimu kwenye mtandao wa internet, usindikaji wa mazao ya kilimo, kompyuta, utafiti wa mimea ya dawa na kadhalika, watu 747 wameshiriki katika mafunzo hayo.

Mbali na hayo mawasiliano na ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya China na nchi za Afrika yaliyoanza katika miaka ya 80 ya karne iliyopita yamekuwa sehemu muhimu ya mawasiliano ya elimu kati ya pande hizo mbili na njia muhimu ya kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa wanafunzi kutoka Afrika. Kutokana na takwimu zisizokamilika, vyuo vikuu 20 vya China vimeanzisha mawasiliano na vyuo vikuu 55 vya nchi 29 za Afrika.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-20