Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-23 14:33:11    
Waongoza filamu vijana wa China wavutia macho nchini China na nchi za nje

cri

Hivi sasa nchini China wameibuka waongoza filamu vijana ambao katika ushindani wa soko la filamu wanashikilia mtindo wao wa sanaa na kusogeza filamu zao karibu na watazamaji. Filamu zao zinavutia nchini China na nchi za nje.

Katika miaka ya karibuni, mapato ya soko la filamu nchini China karibu yote yanachukuliwa na filamu zilizoingizwa kutoka nchini za nje na filamu za nchini zilizowekezwa kwa fedha nyingi wakati filamu zilizowekezwa kwa fedha chache na kuongozwa na waongoza filamu vijana zilikuwa zinaoneshwa kwa nadra katika majumba ya filamu na hata zikioneshwa pato la tikti lilikuwa dogo. Lakini katika majira ya siku za joto mwaka huu, hali imebadilika filamu iitwayo "Hadithi ya Jade" iliyowekezwa yuan milioni nne tu ilipata pato la mauzo ya tikti yuan milioni 20. Mwongoza filamu hiyo anaitwa Ning Hao, ni kijana mwenye umri wa miaka 30. Filamu ya "Hadithi ya Jade" ni hadithi ya kuchekesha, ikielezea kiwanda fulani cha vitu vya sanaa za mikono mjini Chongqing kilikuwa karibu kufilisika, lakini wakati nyumba ilipobomolewa jade moja yenye thamani kubwa iligunduliwa. Ili kufufua kiwanda hicho uongozi wa kiwanda hicho uliamua kuuza jade hiyo kwa mnada. Lakini baada ya habari ya ugunduzi wa jade hiyo kuenea, majambazi kutoka nchi za nje na wezi wa nchini waliitamani na walitumia kila njia kujaribu kuiba wakiwa wanashirikiana na kugombana katika mapambano yao dhidi ya mkuu wa idara ya ulinzi ya kiwanda hicho. Baada ya mapambano ya wazi na ya kichini chini na udanganyifu wa jade ya kweli na ya bandia, majambazi na wezi hao walichezewa vibaya. Mhakiki mzoefu wa jarida la Variety la Hollywood Bw. Derek Eller alisema, "Nimestaajabishwa na filamu hiyo, muundo wa filamu ni mzuri na upigaji filamu hiyo si wa kawaida kama filamu nyingine za China."

Ning Hao ni mmoja tu kati ya waongoza filamu vijana nchini China. Waongoza filamu vijana ni wale waliozaliwa miaka ya 70, ambao wakati walipojihusisha na nyanja ya filamu ulikuwa ni wakati wa mwanzo wa soko huria nchini China, walichagua maisha ya namna nyingine tofauti na ya zamani ambayo waliacha kazi yenye mishahara ya uhakika na kuwa watu wa kujiajiri, waliwahi kufanya kazi za aina nyingi na hii imekuwa raslimali yao ya sanaa. Kutokana na maisha yao wana hisia tofauti na wengine, filamu zao zimeiletea uhai mpya nyanja ya filamu nchini China. Filamu zao mara nyingi zinaoneshwa katika matamasha ya kimataifa na kupata tuzo. Muda si mrefu uliopita, filamu iliyoongozwa na Jia Zhangke iitwayo "Raia Wema katika Sehemu ya Magenge Matatu ya Mto Changjiang" ilipata tuzo ya "Simba wa Dhahabu" katika tamasha la filamu la Venice. Filamu zilizoongozwa na Jia Zhengke huwa zinaonesha hali halisi ya jamii, watu wanaoelezwa katika filamu zake huwa ni akina yakhe, hisia za watu hao ndio hisia za watazamaji.

Filamu iitwayo "Korti kwenye Mgongo wa Farasi" iliyoongozwa na mwongoza filamu mwingine kijana Liu Jie pia ilipata tuzo katika tamasha la filamu la Venice. Filamu hiyo ilitengnezwa kwa mujibu wa mambo ya kweli ikieleza hakimu mmoja wa ngazi ya shina alivyoshughulikia kesi kwenye sehemu za mbali milimani wanakoishi watu wa makabila madogo madogo mkoani Yunnan. Hakimu huyo anasafiri kwa farasi aliyebeba nembo ya taifa kwenye vijiji vitatu visivyokuwa na barabara kushughulikia mashitaka ambayo yanaonesha mgongano kati ya maisha ya watu wanaoishi mbali na sheria ya kisasa na mila na desturi yao ya jadi. Katika filamu hiyo waigizaji karibu wote ni wenyeji, watazamaji wanajikuta wako ndani ya filamu hiyo. Mfanyabiashara wa filamu kutoka Sweden Bw. Willmar Andersson alisema, "Nimevutiwa sana na filamu hiyo, kwa sababu inatokana na maisha halisi na hadithi inachemsha ubongo. Filamu zinazoonesha utu ni muhimu sana kati ya filamu zote duniani."

Nia ya waongoza filamu vijana ni kuendeleza usanii wao wala sio kujipatia mapato ya filamu zao, hata mapato yakiwa makubwa waongoza filamu hao hawayamegi hata kidogo.

Hivi sasa filamu 300 zinatengenezwa kila mwaka nchini China, watazamaji wanatamani kutazama filamu zenye mitindo tofauti. Waongoza filamu vijana wameanza kuvutia macho katika nyanja za filamu nchini China na nchi za nje. "Mfuko wa waongoza filamu nyota barani Asia" uliowekezwa na mwigizaji nyota wa Hong Kong, Liu Dehua, umewapatia nafasi nzuri waongoza filamu vijana wa China. Msimamizi mkuu wa mfuko huo Bw. Yu Weiguo alieleza, "Mfuko huo umewekezwa dola za Hong Kong milioni 25 kwa ajili ya upigaji filamu, moja ya filamu zilizowekezwa ilikuwa ni filamu iliyoongozwa na Ning Hao. Tunatumai kuwasaidia waongoza filamu hodari barani Asia."

Ingawa matatizo fulani bado yapo katika soko la filamu nchini China, lakini Wachina ni wengi na watazamaji pia ni wengi, soko la filamu nchini China ni kubwa, uhuru wa utengenezaji wa filamu unavyokuwa mkubwa siku hadi siku, ndivyo utawapatia waongoza filamu vijana nafasi kubwa zaidi za kuonesha sanaa zao, na soko la filamu nchini China litaimarika kwa aina nyingi za filamu.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-23