Vyombo vya habari vya nchi za magharibi vinapotoa ripoti kuhusu Afrika huwa vinazungumzia umaskini, vurugu na hali duni ya kimaendeleo. Lakini je, hayo ni kweli?
Mkurugenzi wa taasisi ya mambo ya Afrika katika Chuo cha Sayansi ya Jamii cha China Bi. He Wenping kwenye mazungumzo yake na waandishi wetu wa habari ameieleza Afrika iliyo tofauti na vyombo vya habari vya nchi za magharibi.
Bara la Afrika ambalo lilielezwa na mwananadharia wa maendeleo ya kimaumbile Bw. Charles Robert Darwin kuwa ni chanzo cha binadamu, lilikuwa na ustaarabu tangu zama za kale, lakini katika zama za karibuni liliachwa nyuma kwa sababu ya kutawaliwa na wakoloni kwa miaka mingi na vurugu za vita. Hata hivyo, Bi. He Wenping alisema, hali yake mbaya imeanza kubadilika tokea katikati ya miaka ya 90 ya karne iliyopita. Alisema,
"Tangu miaka ya 90 ya karne iliyopita, kutokana kuenea kwa demokrasia, migongano barani Afrika imeanza kupungua. Sudan, Liberia, Burundi, Angola, nchi ambazo ziikuwa na vurugu nyingi zimeanza kuwa tulivu. Kwa ujumla hali ya utulivu imepatikana kwa muda mrefu katika sehemu ya Afrika ya kaskazini na kusini, na migongano inaonekana zaidi katika Afrika ya kati na nchi ndogo ndogo."
Hali ya utulivu huleta maendeleo. Bi. He Wenping alisema, Afrika ya leo sio tena kama iliyoelezwa na vyombo vya habari vya nchi za magharibi kuwa ni bara maskini na hali duni ya kimaendeleo, bali ni bara linalojaa nguvu za uhai na limekuwa linaelekea kuwa na mustakbali mzuri. Alisema,
"Tokea katikati ya miaka ya 90 ya karne iliyopita, uchumi wa Afrika umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka. Vyombo vya habari vya nchi za magharibi vilieleza zaidi hali ya umaskini wa Afrika, lakini yeyote aliyefika barani humo atagundua hali ya kupigania maendeleo barani humo, watu na viongozi wa nchi za Afrika wote wamekuwa wakijitahidi kujiendeleza."
Mwezi Julai, makadirio ya Umoja wa Mataifa yalisema, kwa wastani uchumi duniani unaongezeka asilimia 3.6 kwa mwaka lakini katika muda wa miaka karibu kumi hivi uchumi wa bara la Afrika unaongezeka asilimia 3.7 kwa mwaka, na baadhi ya nchi hata zinafikia asilimia 6, hali ambayo inawafurahisha watu kwa kuona matumaini ya bara hilo. Bi. He Wenping alipotaja sababu za maendeleo ya Afrika alisema,
"Sababu ni mbalimbali, kwanza ni hali ya utulivu wa kisiasa. Pili ni sera mwafaka za kiuchumi. Na sababu nyingine ni kuwa katika miaka ya karibuni uchumi duniani umefufuka na bei ya malighafi inapanda haraka. Uchumi wa Afrika unategemea zaidi uuzaji wa malighafi katika nchi za nje, kwa hiyo hali ya kupanda kwa bei ya malighafi ni faida kwa Afrika. pamoja na hayo, biashara kati ya China na Afrika inastawi kwa kasi, huu vile vile ni msukumo wa maendeleo ya uchumi wa Afrika."
Maendeleo ya uchumi barani Afrika ni wazi kwa wote, hata hivyo kutokana na kuwa bara hilo lilitawaliwa na wakoloni kwa miaka 500, maendeleo yake hakika yatakabiliwa na matatizo mengi. Alisema,
"Katika upande wa kimataifa, bara hilo linakabiliwa mfumo usio wa haki wa kiuchumi, malighafi zinazouzwa katika nchi za nje zinazuiliwa na nchi zilizoendelea, na ruzuku za kilimo za nchi hizo, zaidi ya hayo katika miaka ya karibuni nchi zilizoendelea zimepunguza misaada kwa Afrika. Katika upande wa Afrika yenyewe, bara hilo linakabiliwa na changamoto ya miundo ya kiuchumi, madeni na utulivu wa kisiasa."
Lakini kutokana na mabadiliko ya hali nzuri ya kimataifa na mabadiliko mazuri yanayotokea barani humo watu wanaweza kuwa na matumaini kuhusu maendeleo ya bara hilo. Alisema,
"Viongozi wana matumaini makubwa ya kustawisha uchumi wa bara hilo na wanajitahidi kuboresha miundo na sera za kiuchumi. Katika mazingira ya kimataifa, jumuyia ya kimataifa imetilia maanani zaidi kuliko zama za vita vya baridi bara hilo kwa sababu ya mahitaji ya nishati, hadhi ya Afrika imeinuka."
Mwanzoni mwa mwezi Novemba Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika litafunguliwa, viongozi wa nchi za China na Afrika watakusanyika mjini Beijing na kujadili mpango kabambe wa maendeleo, China na nchi za Afrika ambazo zote ni nchi zinazoendelea hakika zitapata maendeleo makubwa katika karne ya 21.
Idhaa ya kiswahili 2006-10-23
|