Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-23 14:42:08    
Guilin

cri

Watalii wa China waliowahi kuja China kutalii wengi walisema, mjini Xian kuna vivutio vya mabaki ya kale, mjini Guilin kuna vivutio vya milima na mito. Guilin iliyoko kusini magharibi ya China ni sehemu maarufu yenye mandhari nzuri nchini China, ambapo ni sehemu yenye sura ya kijiolojia ya ki-karst. Zaidi ya miaka elfu moja iliyopita, mshairi mmoja wa China alipotembelea Guilin alivutiwa sana na mandhari nzuri ya huko akaandika shairi lake akisema, mandhari nzuri ya milima na mito ya Guilin inawavutia watu zaidi kuliko vivutio vingine duniani, shairi hilo linajulikana sana nchini China, hivyo vivutio vya Guilin huwapa watu taswira nyingi mbalimbali.

Wachina husema kama sehemu moja kuna mto, sehemu hiyo ni kama ina uhai na roho. Mto Lijiang ni kama roho ya milima na mito ya Guilin. Mto Lijiang wenye urefu wa kilomita 83 kutoka mjini Guilin hadi wilaya ya Yangshuo, ni kama mwakilishi wa milima na mito ya China. Maji safi ya mto huo, pamoja na milima yenye maumbo ya ajabu inayoegemeana kwenye kando mbili za mto huo pamoja na mandhari nzuri ya mashamba ya huko, mandhari ya kila sehemu ni nzuri ya kupendeza, ambayo ni kama picha moja moja yenye mtindo dhahiri wa kichina zilizochorwa kwa brashi ya wino mweusi. Hivyo sehemu ya Yangshuo pia ni vivutio dhahiri vya milima na mito ya Guilin.

Wasikilizaji wapendwa, wilayani Yangshuo, kila ifikapo usiku milima na mito ya huko ni kama jukwaa la kuonesha michezo ya sanaa, ambapo maonesho makubwa ya nyimbo na ngoma huoneshwa kwenye Mto Lijiang.

Katika usiku wenye giza totoro, wimbo wa kienyeji unasikika kutoka mbali ambao unawavutia sana watazamaji, kwa ghafla, mwanga wa taa ukaibuka, na milima 12 yenye maumbo ya ajabu iliyoko upande mwingine wa Mto Lijiang ikajitokeza kwa ghafla mbele ya watazamaji, mara watazamaji wakashangaa na kupiga makofi kwa furaha. Maonesho hayo ya michezo ya sanaa yanawashirikisha watu zaidi ya 600, na wengi kati yao siyo wasanii maalum, bali ni wakulima wa huko. Katika maonesho ya dakika 70, wasanii hao wanaonesha maisha ya kawaida ya wavuvi wanaoishi kando mbili za Mto Lijiang, pamoja na kazi za kuvua sama, kulima mashamba, kufuga ng'ombe, kusimulia hadithi na kuimba nyimbo za kabila la wazhuang wanaoishi sehemu hiyo, na maonesho hayo yanapatana vizuri kwenye mandhari ya kimaumbile ya milima na mito, na kuwapa watazamaji taswira nzuri sana.

Maonesho hayo yalianzia mwezi Oktoba mwaka 2003, kila siku yanafanyika huko na kila mara yanawavutia sana watazamaji.

Bwana Thomas na mkewe Martina Laubis kutoka Ujerumani waliotembelea Yangshuo na kutazama maonesho hayo, walivutiwa sana na kuyasifu sana. Walisema hiyo ni mara yao ya kwanza kutalii nchini China, walichagua Yangshuo. Walisema hapo awali hawakufikiri kwamba watafanya utalii barani Asia, baadaye walishauriwa na rafiki yao aliyeishi Hong Kong, wakaamua kutalii Guilin kwa siku moja ya wikiendi, lakini walivutiwa sana na vivutio vya huko hata walisahau kuondoka.

Bwana Thomas Laubis alisema: Guilin ina vivutio vizuri sana, hakika tutakuja tena kutalii nchini China na barani Asia.

Mkewe Bibi Martina Laubis alisema: Wakazi wa Guilin ni wenye uchangamfu na urafiki kwa wageni, waliongea kwa hiari na sisi, naona hao ni watu wanaoaminika. Hakika tutakuja tena China na kutembelea sehemu nyingine nchini China.

Kama walivyosema Bwana Thomas na mkewe Bibi Martina Laubis, vivutio pekee vya Guilin vimewavutia watalii wengi wa China na wa nchi mbalimbali, hata watalii kadha wa kadha kutoka nje wameng'ang'ania huko na kuishi huko Yangshuo. Kijana kutoka Australia Bwana Alfonso Exposito ni mmoja kati yao. Miaka mitano iliyopita alianza kuishi huko Yangshuo, akaoana na msichana mmoja wa huko, hivi sasa wamekuwa na mwana mmoja, kijana huyo na mkewe wanaendesha baa moja kwenye mtaa wa Xijie ambao ni mtaa maarufu wenye maduka mengi huko Yangshuo.

Bwana Alfonso Exposito alisema: Yangshuo ina mandhari nzuri sana, kuna Mto Lijiang unaopendeza, ukifika Yangshuo hakika utatembea kwenye mto huo. Mandhari ya sehemu hiyo ina mvuto wake pekee nchini China. Yangshou ni sehemu ndogo, ambapo kuna hali ya utulivu, watalii wengi kutoka nje wakifika huko huishi kwa wiki moja hata wiki mbili, ingawa hapo awali mpango wao ni kutembelea huko ulikuwa ni kwa siku 2 au 3 tu. Kwani tunaona kuwa sehemu hiyo inafaa kuishi maisha, watu wanaweza kupumzika vizuri hapa.

Takwimu zilizotolewa na Idara ya utalii ya Guilin zimeonesha kuwa, mwaka 2005 Mji wa Guilin uliwapokea watalii kutoka nchini na nje wapatao laki 7, na inakadiriwa kuwa kwa mwaka huu mzima, watalii zaidi ya milioni 1.1 kutoka nchini na nje watapokelewa mjini humo.

Naibu mkurugenzi wa idara ya utalii ya Guilin Bwana Chen Yunchun alijulisha kuwa, Guilin ni sehemu ya utalii duniani inayopendekezwa na shirika la utalii duniani. Katika sekta ya utalii duniani, utalii wa China una alama mbili za vivutio vya Ukuta mkuu wa kaskazini ya China na Mandhari nzuri ya Mto Lijiang wa Guilin.

Wageni wengi kutoka nchi za nje pamoja na wakuu wa nchi mbalimbali walipofika China hakika walikwenda Guilin kwa matembezi. Mpaka sasa Mji wa Guilin umewapokea marais 108 wa nchi za nje. Rais wa zamani wa Marekani Richard Nixon alipofanya ziara ya kwanza nchini China aliwahi kutembelea Guilin na kutazama mandhari nzuri ya milima na Mto Lijiang. Alisema nilitembelea zaidi ya nchi 80 duniani, na miji zaidi ya 100, naona Guilin ni yenye mandhari nzuri zaidi kuliko sehemu nyingine.

Bwana Chen Yunchun alisema hivi sasa kila mwaka watalii kutoka nchi za nje wanaotembelea Guilin, watalii wa nchi za Afrika bado ni wachache, lakini hivi sasa Mji wa Guilin unachukua hatua za kuwavutia watalii kutoka nchi za Afrika. Alisema katika miaka ya hivi karibuni, Mji wa Guilin umeshiriki katika shughuli za kutangaza vivutio vya utalii zilizofanyika nchini Afrika ya kusini, ili kuwawezesha watalii wa Afrika waijue zaidi China, na kuijua Guilin. Ameeleza imani yake kuwa, watalii kutoka barani Afrika wanaotembelea Guilin wataongezeka mwaka hadi mwaka.

Katika sehemu nyingi duniani, kutokana na maendeleo ya shughuli za utalii, na kuongezeka kwa watalii, mazingira ya sehemu hizo yanakabiliwa na shinikizo kubwa na hata uharibifu. Lakini ukitembea mjini Guilin utahisi daima hewa safi na kuona maji safi ya Mto Lijiang, ambapo majengo ya mjini humo yametapakaa katika sehemu hiyo inayopandwa miti, maua na majani mengi. Wataalamu wa wizara ya ujenzi ya China walisema, Guilin ni mji unaofaa sana kwa binadamu kwa kuishi.

Bwana Chen Yunchun alisema mazingira ya milima na mito ya Guilin ni ya pekee nchini China hata dunia nzima, ili kuhifadhi vizuri mazingira asili ya Guilin, shughuli za utalii za Guilin zinaendelezwa kwa msingi wa kuhifadhi kwanza mazingira. Ili kulinda Mto Lijiang, viwanda karibu 30 vilifungwa mwanzoni mwa miaka ya 80 mjini Guilin.

Bwana Chen alisema: Kila serikali ya awamu mpya ya Guilin huweka mkazo kwanza katika kulinda mazingira ya viumbe ya Guilin. Tunapoongeza miradi ya utalii, huzingatia kwanza kuhifadhi mazingira, kama miradi hiyo hailingani na vigezo vya uhifadhi wa mazingira, hakika tunaiacha.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-23