Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-24 14:15:26    
Barua 1022

cri

Msikilizaji wetu Jasmine Abbasy wa Shule ya Sekondari Dakawa, Morogoro nchini Tanzania anatumai kuwa wafanyakazi wote wa Idhaa ya kiswahili ya Radio china Kimataifa ni wazima na anatoa pongezi kwa vipindi bora vinavyoelimisha. Kwa sasa Bi Jasmine anasema anaendelea na masomo yake kwenye shule ya sekondari Dakawa, ambayo iko umbali wa kilometa 253 kutoka Dar es salaam. Pia anasema huko alik hapati vizuri matangazo ya RadioChina Kimataifa na kwa vile hakuna huduma ya mtandao wa internet, kidogo inakuwa ni vigumu sana kwake kupata vizuri matangazo ya Radio China kimataifa, hivyo anaomba kukiwa na uwezekano Radio China iboreshe usikivu wa matangazo ili yeye pamoja na wasikilizaji wengine wa huko Dakawa waweze kuyapata vizuri mawimbi ya Radio China Kimataifa.

Msikilizaji wetu huyo pia anaomba ikiwezekana atafutiwe marafiki wa kalamu ili aweze kuwasiliana nao, wanaweza kuwa wanafunzi au watu wa kawaida. Anaomba sana suala na marafiki lipewe uzito unaostahili kwani anapenda wachina na watanzania wawe kama ndugu. Pia anaomba atumiwe majarida na pia aweze kujibiwa barua zake kwa muda.

Bi Jasmine anaendelea kusema kuwa kuna watu ambao wanapenda kujiunga na CRI kutoka Dakawa lakini hawafahamu ni kwa jinsi gani wanaweza kujiunga, hivyo anaomba kama kuna uwezekano wafahamishwe, na mwisho anapenda tena kutoa pongezi kwa matangazo mazuri na yanayoelimisha.

Tunamshukuru msikilizaji wetu Bi Jasmine Abbasy kwa barua yake ya kutuelezea mengi, kuhusu ombi lake la kutafutiwa marafiki wa kalamu, hapa tunapenda kumwambia kwamba, tunaomba atuelewe kuwa hii si kazi rahisi kwetu, kwani sisi tunatangaza kwa lugha ya Kiswahili kwa wasikilizaji wetu walioko Afrika ya mashariki, na watu wengi wa hapa China hawaelewi Kiswahili, hata hawajui matangazo yetu, si rahisi kumsaidia kupata marafiki wa kalamu kutoka China, kama tutaweza kupata wanafunzi wa China wanaosoma Kiswahili hapa hapa nchini tutajaribu kumsaidia.

Mskilizaji wetu Augustine Kabadi Michael wa S.L.B 1934, Tabora nchini Tanzania ana furaha kubwa kuandika barua hii kwa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, kwani amekuwa akiitafuta anwani kwa siku nyingi sana, ili aweze kuwa mmoja wa wanachama wa Radio China Kimataifa. Anasema yeye ni kijana wa mtanzania mwenye umri wa miaka 28 na elimu yake ni ya kidato cha nne, ambayo alihitimu mwaka 1999. Kwa sasa anajishughulisha na masuala ya ufundi wa magari madogo pamoja na udereva. Hiyo ndiyo ajira yake ambayo amaeajiriwa na shirika lisilo la kiserikali linajihusisha na mambo ya maendeleo katika kilimo, ufugaji pamoja na huduma muhimu za kijamii.Ikiwa ni pamoja na usambazaji wa vijarida vinavyoelimisha juu ya maisha ya vijana pamoja na jamii nzima ya kitanzania hasa katika suala la kupiga vita umaskini na ujinga vijijini.Shirika hilo linaitwa JIDA au Jikomboe .

Bwana Augustine anadhani kuwa ombi lake la kuwa mwanachama litakubaliwa na angependa kujua mengi zaidi kuhusu idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, ilianza lini, na kwa nini inatangaza kwa lugha ya kiswahili. Vilevile kwa nini haijafikiria kujiunga kurusha matangazo kupitia radio za nchini Tanzania kama ilivyo kwa radio zingine za kimataifa kama BBC,VOA, DW. Na pia anapenda kufahamu mipango ya baadaye kwa nchi zinazotumia lugha ya kiswahili za Tanzania, Kenya, Uganda na sasa hata Rwanda, Burundi na DRC.

Msikilizaji wetu huyu anaomba kama CRI ingejaribu kujiunga na na vituo vya masafa ya FM kwani vimeenea sana nchini Tanzania ili CRI iweze kusikika zaidi katika pembe za Tanzania. Anatumaini kuwa maombi na mapendekezo yake yatafanyiwa kazi na anaahidi kutafuta wanachama na wasikilizaji wengi katika mkoa wa Tabora. Mwisho anapenda kutuma salamu kwa Familia ya Mzee Michael wakiwa Berega Hospitali Morogoro, Rafiki zake: John Chodota akiwa Iringa, Jerome Ndonde akiwa Nzega i Tabora, Enock Lyoba Muuza magazeti posta Tabora, wanakwaya wa Familia Takatifu parokia ya Makolola, mtoto wake Kristina akiwa Shinyanga Tanzania, Agnetha Mbele na kaka yake Mathew Mbele wote kwa pamoja wakiwa Tabora

Tunamshukuru msikilizaji wetu Augustine kwa barua yake na maswali yake. Tunamkaribisha kuwa mwanachama wa CRI. Radio China kimataifa ilianzishwa mwaka 1940, mwanzoni ilitangaza kwa lugha chache tu kama vile Kiingereza na Kijapan, baadaye iliendelea kukuzwa na kutangaza kwa lugha mbalimbali, mpaka sasa Radio China kimataifa kila siku inatangaza kwa lugha 43 zikiwemo lugha 38 za kigeni. Na matangazo ya Kiswahili yalirushwa hewani kuanzia Tarehe 1 Septemba mwaka 1961. Madhumuni ya matangazo ya Radio China kimataifa ni kwa ajili ya wasikilizaji wa nchi mbalimbali waijue China na kuongeza maelewano na ushirikiano kati ya China na nchi mbalimbali duniani. Ni matumaini yetu kuwa Matangazo ya Kiswahili ya Radio China kimataifa yatakuwa kama daraja kati ya China na nchi za Afrika ili kuwawezesha watu wa nchi mbalimbali za Afrika waijue China, kuelewa zaidi kuhusu mambo yake mbalimbali ya siasa, historia, uchumi na utamaduni. Vile vile tunapenda kujiunga kurusha matangazo na radio za nchini Tanzania kama ilivyo kwa radio zingine za kimataifa kama BBC, VOA, DW, Lakini kazi si rahisi kufanikiwa tunaomba wasikilizaji wetu watuelewe. Lakini hakika tutaendelea na juhudi zetu ili kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu na kuwawezesha wapate usikivu mzuri zaidi.

Msikilizaji wetu Debra Barasa wa S.L.B 1042 Bungoma nchini Kenya anapenda kutoa shukrani na pongezi kwa bidii waliyo nayo wafanyakazi wa radio China Kimataifa. Ama kwa hakika anasema Radio China Kimataifa imejifunga kibwebwe kuhakikisha kuwa wasikilizaji wake wanapata habari za kutosha. Akiwa msikilizaji wa Radio China Kimataifa ameshapata kujumika pamoja nasi kwa muda mrefu na angependa kutoa pongezi kwa bidii hasa za kumfahamisha kuhusu Taiwan, ambacho ni kisiwa cha hazina cha China. Msikilizaji wetu anashukuru pia kwa kuweza kutuma salamu kwa wapendwa na marafiki zake.

Ombi lake ni kuwa yafanyike marekebisho katika muda wa matangazo katika baadhi ya sehemu, kwa mfano inamuia vigumu yeye na wasikilizaji wengine vijana kuyapata matangazo ya saa tisa mchana, kwa kuwa muda huo vijana wengi wanakuwa katika shughuri za kujiingizia kipato.

Na kwa upande wa wanafunzi wanapokea kadi na ujumbe kutoka Radio china kimtaifa wakati ambapo bado wanakuwa shule, na labda sanduku la barua litumiwalo ni lile la nyumbani, hivyo inawawia vigumu kurudisha majibu, kwa wakati, yeye kwa niaba ya wanafunzi anaomba radhi kwa hilo. Mwisho anamalizia kwa kututakia kila la kheri na kazi njema.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Debra Barasa kwa barua yake na pendekezo lake, siku hizi tunajitahidi kurekebisha mpango wetu ili vipindi vyetu viweze kuwafurahisha zaidi wasikilizaji wetu. Kama ikiwezekana saa za matangazo zitaweza kurekebishwa kwa mwafaka zaidi. Ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu watatuletea maoni na mapendekezo zaidi ili siku nyingine tuweze kurekebisha vizuri zaidi vipindi vyetu.

Msikilizaji wetu David D. Mangwesi wa S.L.B 284 Magu, mjini Mwanza Tanzania ametuletea barua akieleza mataumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa ni wazima na wanaendelea na shughuli katika idhaa ya kiswahili ya radio china kimataifa. Anasema dhumuni la barua yake ni kutoa shukrani kwa jinsi matangazo ya Radio China kimataifa yanavyosikika vizuri. Lakini pia anaomba apatiwe ratiba ya vipindi vya kila siku. Bwana David anaomba radhi kwa kutoshiriki katika chemsha bongo kwa sababu alichelewa kupata bahasha ya chemsha bongo. Pia anaomba atumiwe kalenda mpya na hata vitabu vya hadithi katika lugha ya kichina kwani anapenda sana kuijua lugha ya kichina.

Msikilizaji wetu Fesbeth Malima anayetunziwa barua na Mutanda Ayub wa S.L.B 172 Bungoma nchini Kenya, ameanza barua yake kwa kutoa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimatifa. Anasema yeye, dada yake pamoja na mama yake walifurahi sana wakati walipokuwa wakitazama Runinga na kumuona rais wa Jamhuri ya watu wa china bwana Hu Jintao akiwasili nchini Kenya.

Hali hiyo imeonesha upendo na urafiki mwingi uliopo kati ya watu wa Kenya na watu wa China. Anasema walishindwa tu kusafiri kwenda Naiorobi ili waweze kushuhudia moja kwa moja, lakini wanashukuru waliweza kupata vizuri habari kuhusu ziara hiyo kupitia matangazo ya Radio China Kimataifa. Anasema wana matumaini kuwa siku moja watamuona tena na Rais Hu Jintao au kuweza kupata nafasi ya kuja kusoma huko China, ili waweze kuelewa zaidi lugha ya kichina na utamaduni wa kichina.

Msikilizaji wetu Ali Hamis Kimani wa shule ya Msingi Alaro, Othoro nchini Kenya anatoa pongezi lukuki huku akiwa na wingi wa matumaini kuwa wote tu buheri wa afya, yeye pia ni mzima. Baada ya salamu na maamkizi anapenda kutoa shukrani zisizo na kifani kwa huduma nzuri za Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.Anasema Radio China kimataifa imemuwezesha kuwasiliana nasi, na marafiki na jamaa zake kote ulimwenguni kupitia kadi na bahasha zilizolipiwa anazozipata mara kwa mara. Anasema anashukuru sana na anaomba Mungu atubariki.

Mbali na hayo msikilizaji wetu huyo anapenda kutoa malalamiko yake kutokana na kuchukua muda mrefu kuzisoma kadi za salamu. Sasa ni karibu miezi mitatu tangu azisikie salamu zake hewani, anauliza kwa nini iko hivyo??

Mwisho anashukuru kwa kutumiwa nakala ya maswali ya chemsha bongo ya mwaka uliopita, lakini pia anauliza ni kwanini hatukuambatanisha na majibu sahihi ili aweze kutambua ni kwa nini alishindwa katika chemsha bongo hiyo na hivyo basi kukosa zawadi? Anatumai kuwa hakushindwa maswali yote na anadhani kuwa labda alistahili kupata zawadi japo kidogo.

Tunamshukuru Ali Hamis Kimani kwa barua yake. Siku za karibuni tumefanya matekebisho ya kutangaza salamu zenu, ambapo kadi nyingi zinasomwa. Kuhusu majibu ya chemsha bongo, wasikilizaji wengi walijibu karibu sahihi, lakini baadhi yao walieleza vizuri zaidi, kuchagua washindi hakutegemei majibu ya chemsha bongo peke yake, kwani majibu mengi ni sahihi ambayo ni rahisi kupatikana, hivyo pia tunazingatia makala au maelezo walizoandika wasikilizaji hao.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-24