Mjumbe wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Bw. Jan Pronk tarehe 23 jioni aliondoka Sudan na kufika New York tarehe 25 ili kufanya mjadala na Bw. Kofi Annan. Kutokana na kuwa Bw. Jan Pronk aliondoka Sudan kutokana na amri ya serikali ya Sudan, jambo hilo linafuatiliwa sana.
Tarehe 22 serikali ya Sudan ilimwandikia barua Bw. Kofi Annan ikimtaka amwondoe Bw. Jan Pronk nchini Sudan kabla ya tarehe 25. Kabla ya hapo tarehe 14 mwezi huu Bw. Jan Pronk alitoa makala yake kwenye mtandao wa internet ikisema kwamba jeshi la serikali ya Sudan lilipata hasara kubwa kwenye mapambano dhidi ya vikosi vya upinzani na ari ya jeshi hilo ya mapambano imeshuka. Kauli hiyo ilikasirisha serikali ya Sudan na kusema kwamba kitendo chake kimekuwa tishio kwa usalama wa Sudan. Siku chache baadaye serikali ya Sudan ilitangaza Bw. Jan Pronk kuwa ni "mtu asiyekaribishwa", na tarehe 22 ilimwamrisha aondoke nchini Sudan.
Bw. Jan Pronk ana umri wa miaka 66, aliwahi kuwa waziri wa mazingira wa Uholanzi, na kuanzia miaka ya 80 amekuwa ofisa katika vyombo vya Umoja wa Mataifa. Kuanzia mwaka 2004 alikuwa mjumbe wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan. Kwa kuwa mjumbe wa katibu mkuu angesuluhisha pande mbili za serikali ya Sudan na vikosi vya upinzani kufanya mazungumzo ya amani, lakini ametilia mkazo katika kuvutia jumuyia ya kimataifa kwenye suala la Darfur.
Darfur iko katika sehemu ya magharibi ya Sudan. Mwezi Februari mwaka 2003 mgogoro mkali ulizuka huko kati ya wanamgambo na jeshi la serikali na kusababisha vifo vya watu wengi, hivi sasa watu milioni 2.5 wamepoteza makazi. Umoja wa Mataifa unaichukulia Darfur kama ni sehemu yenye wasiwasi mkubwa wa kibinadamu duniani, na unajitahidi kutoa msaada wa kibinadamu katika sehemu hiyo.
Mwezi Mei mwaka huu serikali ya Sudan na kundi kubwa la upinzani "Sudan Liberation Movement" zilisaini mkataba wa amani huko Abuja nchini Nigeria, lakini mgogoro haukusimama. Hatimaye Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio mwezi Agosti ambalo liliamua kutuma askari elfu 20 huko Darfur badala ya askari 7,000 wa Umoja wa Afrika ili kuhakikisha mkataba huo wa amani unatekelezwa, lakini azimio hilo linapingwa na serikali ya Sudan.
Katika hali kama hiyo, Bw. Jan Pronk alizidi kukosoa mambo mbalimbali ya serikali ya Sudan, na hasa alikosoa kuwa kulikuwa na udanganyifu wa serikali ya Sudan katika utekelezaji wa azimio, kutozuia wanamgambo kuwaua raia, kusalimisha silaha za wanamgambo, kushindwa kuchukua hatua za kuwaadhibu wauaji, matokeo yanaonesha kwa kiasi fulani serikali ya Sudan imechangia mauaji dhidi ya raia. Yote hayo yalifanya uhusiano kati ya Jan Pronk na serikali ya Sudan uwe mbaya. Mjumbe wa Sudan katika Umoja wa Mataifa Bw. Abdalhaleen Mohamad kwenye mkutano na waandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa tarehe 23 alisema, tokea Bw. Jan Pronk alipoanza kuwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan alikuwa anaingilia mambo ya ndani ya Sudan na kwenda kinyume na makubaliano kati ya serikali ya Sudan na kundi la Umoja wa Mataifa nchini Sudan, kwa hiyo serikali ya Sudan imepoteza uvumilivu naye.
Tukio la kuitwa kwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa limesababisha watu wengi kutafakari, kwamba je maofisa wa ngazi ya juu wa kimataifa inafaa watangaze makala zao kwenye mtangao wa iternet kuhusu masuala nyeti ya nchi fulani? Msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema, hilo ni suala jipya katika karne ya 21. Kabla ya hapo Bw. Kofi Annan alikuwa na msamaha kuhusu suala hilo akiona hili ni suala la uhuru wa kutoa maoni binafsi na Umoja wa Mataifa hauna sheria kuhusu suala hilo. Kwa hiyo kabla ya kujadili suala hilo kwa kina, kitendo cha Bw. Jan Pronk kinachukuliwa kuwa ni kitendo chake binafsi, na Umoja wa Mataifa haujatoa maoni yoyote kama Bw. Jan Pronk ataendelea na wadhifa wake na juhudi za Umoja wa Mataifa zitaathiri vipi utatuzi wa suala la Sudan. Yote hayo yatajulikana baada ya mjadala kati ya Bw. Jan Pronk na Bw. Kofi Annan.
Idhaa ya kiswahili 2006-10-24
|