Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-26 14:51:01    
Kijiji cha kabila la Wadulong kilichopo milimani

cri

Wadulong wanaishi Katika eneo la mtiririko wa mto wa Dulong kusini magharibi mwa China. Kabila hilo sasa lina watu 5,800 tu, ni miongoni mwa makabila yenye watu wachache sana hapa nchini China. Wadulong ni watu wa kwanza walioanza kuishi kando ya mto Dulong, na hawana maandishi ya kikabila na kuna maelezo machache sana kuhusu kabila hilo kwenye nyaraka za historia. Mwaka 1949 China mpya ilipoasisiwa, Wadulong walikuwa wanaishi katika hali duni ya maendeleo kama ilivyo kuwa wanadamu kabla ya kuzaliwa kwa Kristo. Hivi sasa miaka zaidi ya 50 imeshapita, je, watu wa kabila hilo wanaendelea vipi? Mwandishi wetu wa habari alitembelea kijiji kimoja cha Wadulong na kutandia makala hii.

Asubuhi moja ambapo mvua ilikuwa ikinyesha, mwandishi wetu wa habari alifika kwenye wilaya iliyojiendesha ya Wadulong na Wanu mkoani Yunnan, kuanza safari ngumu ya kupanda kwa miguu mlima mmoja wenye mwinuko wa kilomita 1,800 kutoka usawa wa bahari, ambako kuna kijiji kimoja cha kabila la Wadulong kiitwacho Xiaochala.

Njiani kuelekea kijiji hicho mwandishi wetu wa habari alimkuta msichana mmoja wa kabila la Wadulong, dada huyo mwenye umri wa miaka 18 anaitwa Bai Yanjuan, anakaa wilayani na alipokutana alikuwa akirudi maskani kuwatembelea jamaa zake.

Kwa wakazi wa miji kupanda mlima huo kunawachosha sana, lakini dada huyo alionekana anapiga hatua nyepesi. Alisema "Narudi kwenye maskani yangu mara kwa mara katika siku za likizo. Inanibidi nipande mlima kwa kutumia saa moja. Sioni uchovu, nimezoea kupanda mlima."

Dada Bai Yanjuan amehitimu kutoka kwenye shule ya ngoma ya huko mwaka huu, na kupata ajira katika kikundi cha nyimbo na ngoma za kikabila huko wilaya. Alisema "Kabila letu lina watu wachache sana. Kikundi hicho cha nyimbo na ngoma za kikabila kinakwenda sehemu mbalimbali kufanya maonesho ili kuwafahamisha watu mila na desturi za kabila letu, uzuri wake na mavazi na mapambo zake."

Maongezi na msichana huyo yalisaidia sana kupunguza uchovu wa safari hiyo, ambapo baada ya saa 2 mwandishi wa habari akafika kijiji cha kabila la Wadulong.

Aliyemlaki mwandishi wetu wa habari ni mbwa wa Bw. Mu Guangming ambaye nyumba yake ipo kwenye mlango wa kuingia kijiji hicho. Familia hiyo ina watu wanne, Bw. Mu Guangming, mke wake na watoto wawili wanaosoma kwenye shule ya sekondari. Mwenye nyumba alimpokea mwandishi kwa ukarimu. Wadulong wanafurahi wanapotembelea na wageni, na idadi ya wageni wanaotembelea familia moja inachukuliwa kama ishara ya uzuri au ubaya wa tabia ya watu wa familia hiyo.

Bw. Mu Guangming ana nyumba ya mbao, haina samani nyingi isipokuwa televisheni moja mpya ilimvutia sana mwandishi wetu wa habari. Akizungumzia chombo hicho cha kisasa cha umeme, mwenye nyumba alionekana kuwa na majivuno makubwa. Alisema "Tunaweza kutizama programu za vituo 20 za televisheni. Awali hatukuwa na televisheni, niliinunua hii miezi mwili iliyopita tu. Kabla ya hapo hatukuwahi kutizama televisheni."

Bwana huyo aliongeza kuwa, alinuna jenereta ndogo inayozalisha umeme kwa nguvu ya maji ili kuipatia seti ya televisheni umeme. Alisema katika miaka ya karibuni wanakijiji wenzake wamepata uwezo hatua kwa hatua katika miaka ya hivi karibuni, kwa kutegemea kuuza mazao ya mlimani na sera ya serikali ya kuwapunguzia na kuwasamehe kodi za kilimo. Baadhi yao pia wamenunua televisheni.

Televisheni hiyo ilileta furaha nyingi katika familia hiyo. Binti wa Bw. Mu Guangming, dada Mu Jinhua alieleza kuvutiwa na vipindi vya televisheni. Alisema "Nafurahia kutizama vipindi vya televisheni, kwani naweza kupata ujuzi mwingi kupitia vipindi hivyo ambao haupo kwenye vitabu vya masomo, pia naweza kupata habari kuhusu sehemu nyingine nje ya kijiji chetu."

Msichana huyo na kaka yake mdogo, wanasoma kwenye shule ya sekondari iliyopo chini ya mlima. Wanakaa kwenye mabweni ya shule na kurudi nyumbani katika siku za mapumziko.

Familia hiyo inafuga nguruwe watano na kuku kadhaa, hata hivyo chanzo kikuu cha kipato ni kuchuma mimea inayokua mlimani inayotumika kutengeneza dawa za mitishamba, na kuiuza kwenye soko lililopo chini ya mlima. Mapato cha familia hiyo ni Yuan zaidi ya elfu moja hivi kwa mwaka. Fedha hizo si nyingi, lakini maisha yao yanaboreka hatua kwa hatua, hususan tangu miaka miwili iliyopita serikali ilipoanza kutekeleza sera mpya ya elimu, ambayo watoto wa makabila yenye watu wachache sana mfano wa kabila la Wadulong wanaotimiza umri wa kwenda shuleni, wanasahemewa ada na karo za masomo, pamoja na hayo wanapewa ruzuku ya kiasi fulani cha fedha ili kusaidia maisha ya familia yao.

Mwandishi wetu wa habari alipoaga familia hiyo usiku ulianguka, watu wanne wa familia hiyo walikuwa wanakaa kuzunguka moto, wakaanza kutazama vipindi vya televisheni.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-26