Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-26 15:01:03    
Mkulima aliyejitolea kutunza ukuta mkuu katika miaka 20 iliyopita

cri

Ukuta mkuu uliopo nchini China ni majivuno ya Wachina, ambao pia ni urithi adimu wa binadamu wote. Katika muda wa miaka zaidi ya elfu 2 iliyopita, ukuta mkuu umekuwa ukiharibika vibaya kutokana na vita vya mara vingi na nguvu za maumbile zikiwemo upepo na mvua. Kutokana na hali hiyo, katika miaka ya hivi karibuni Wachina wengi wameanza kujitolea kutunza ukuta mkuu. Bw. Zhang Heshan ndio ni mmojawapo kati yao, mkulima huyo wa kawaida amejishughulisha na shughuli hizo kwa muda wa miaka zaidi ya 20.

Bw. Zhang Heshan anaishi katika kijiji cha Chengziyu, mkoani Hebei katikati ya China. Kijiji hicho kipo karibu na sehemu ya ukuta mkuu uliojengwa kileleni mwa mlima. Kwa mujibu wa kumbukumbu za historia, sehemu hiyo ya ukuta mkuu ilijengwa mwaka 1381. Bwana Zhang alisema mababu wa zamani wa wakazi wa kijiji hicho walikuwa askari wa kulinda ukuta mkuu, ambao baadaye walijipanga huko na hatua kwa hatua kikajitokea kijiji hicho.

Zhang Heshan alizaliwa katika kijiji hicho, kwa maneno yake mwenyewe alikuwa anakua kwenye masimulizi ya hadithi zinazohusu ukuta mkuu. Alisema "Nilipokuwa mtoto mdogo, baba yangu mzazi alinisimulia hadhithi kuhusu ujenzi wa ukuta mkuu, mila na sifa za ujenzi za ukuta mkuu, kila kitu."

Bwana huyo alikumbusha kuwa hali ya sehemu hiyo ya ukuta mkuu iliyopo karibu na kijiji chake ilikuwa nzuri wakati wa utotoni mwake. Lakini uliharibika siku hadi siku kutokana na wenyeji kutofahamu umuhimu wa kuutunza. Hali ambayo ilimpa wasiwasi kubwa, hasa katika miaka ya1980 tukio la kupoteza kwa mnara mmoja uliokuwepo kwenye ukuta mkuu likamgusa sana. Zhang Heshan alikumbusha akisema mnara huo uliotengenezwa kwa jiwe kubwa ulikuwa ukiwekwa ndani ya ngome moja ya ukuta mkuu, na kwenye sura za mnara huo yalichongwa maneno mengi. Alisema  "Mwaka 1978 nilikuta mnara huo ukaanguka ndani ya ngome, lakini haukuvunjika kabisa. Hadi mwaka 1980 nilipokwenda kukagua, mnara huo ulikuwa umepotea. Siku hiyo hiyo nikaamua ni lazima ukuta mkuu utunzwe vizuri, kwani vitu vya kale vikiteketezwa basi havipo tena."

Kuanzia hapo Bw. Zhang Heshan alianza kujikita kwenye shughuli za kuutunza ukuta mkuu, mpaka sasa amefanya hivyo kwa miaka zaidi ya 20, ambacho katika kipindi hiki kila siku anatembea kwa umbali wa kilomita zaidi ya 10 kwa ajili ya kukagua sehemu ya ukuta mkuu iliyopo karibu na kijiji chake. Akiwakuta watu waliochimba matofali ya ukuta mkuu ili kuchuma mimea ya mitishamba au kukamata wadudu, ama watu waliochunga kondoo kwenye ukuta mkuu, anawakataza na kuwashauria waende sehemu zilizo mbali na ukuta mkuu. Akikuta mifereji ya kutoza maji ya mvua ya ukuta mkuu kukwama, anaondoa matope. Akikuta mimea kuotea kati ya matofali ya ukuta mkuu, anaikata ili isiharibu ujenzi huo. Matofali yakianguka, anayaweka vizuri na watalii wakiacha takataka kwenye ukuta mkuu, anazikusanya.

Pamoja na hayo Zhang Heshan pia aliwaelimisha wanakijiji wenzake wajiunge na shughuli za kuutunza ukuta mkuu. Mwanakijiji Li Zhenfang alisema "Awali kwa ujumla wanakijiji hawakufahamu umuhimu wa kuutunza ukuta mkuu, walifanya vitendo vya kuharibu ukuta mkuu. Kutokana na juhudi za mzee Zhang za kueneza ujuzi husika ama jinsi alivyotenda mwenyewe, hivi sasa sisi tumekubali wazo la kuutunza ukuta mkuu."

Mwaka jana mzee Zhang alianza kuvutiwa na kupiga picha. Sasa katika doria anayofanya kila siku kwenye ukuta mkuu, anakwenda na kamera yake na kupiga picha zinazopendeza za ukuta mkuu.

Katika shughuli za utunzaji wa ukuta mkuu, mkulima huyo pia anavutiwa na historia yake na kuanza kujikita katika utafiti kuhusu ujenzi huo. Mpaka sasa insha zake kadhaa zimechapishwa kwenye gazeti la taaluma ya ukuta mkuu la China. Mwaka 2002 Zhang Heshan alikubaliwa na taasisi ya taaluma ya ukuta mkuu ya China ambayo wanachama wake wengi ni wataalamu na wasomi, mzee huyo akawa mkulima wa kwanza aliyepata uanachama wa taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake. Katibu mkuu wa taasisi hiyo Bw. Dong Yaohui alimsifu sana Zhang Heshan akisema "Wakazi wengi wanaoishi kando ya ukuta mkuu wamejitolea kufanya shughuli za kuutunza ukuta mkuu, Bw. Zhang Heshan ni mmojawapo kati yao. Watu hao wanajulikana kama uti wa mgongo wa kuulinda ukuta mkuu."

Hatua ya mzee Zhang Heshan kujitolea kuutunza ukuta mkuu pia imefuatiliwa na watu wa nje ya China. Mpaka hivi sasa wageni zaidi ya elfu 1 kutoka nchi zaidi ya 10 za kigeni zikiwemo Marekani, Sweden na Norway, walimtembelea nyumbani kwake, wakisikiliza masimulizi ya mzee huyu kuhusu ukuta mkuu. Bw. Sebashan Curt Winnen kutoka Ujerumani alisema  "Yeye alitusimulia kwa majivuno jinsi alivyotunza ukuta mkuu. Maelezo yake yalitushangaza sana, kumbe anafuatilia hata kitu kidogokidogo kuhusu utunzaji wa ukuta mkuu. Mimi nimeguswa sana kuwamba kuna Wachina wengi wa kawaida wanaojishughulisha na utunzaji wa ukuta mkuu."

Hivi sasa mzee Zhang Heshan bado anaendelea kufanya doria ya ukaguzi kwenye ukuta mkuu kila siku. Kutokana na mfano wake, mwanae Zhang Xiaoguang amejiunga na baba yake mzazi katika shughuli hizo za kuutunza ukuta mkuu, ambao wana ari ya kuwafahamisha watu wengi zaidi ukuta mkuu wa China na utunzaji wake.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-26