Nigeria ni nchi kubwa katika sehemu ya Afrika ya magharibi yenye watu milioni 130, nchi hiyo ina maliasili nyingi, na ni mhusika muhimu katika muundo wa kisiasa wa sehemu hiyo. Katika miaka mingi iliyopita, China inatilia maanani sana kuendeleza uhusiano kati yake na Nigeria. Balozi wa China nchini Nigeria Bwana Xu Jianguo hivi karibuni alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema mustakabali wa ushirikiano kati ya China na Nigeria ni mpana.
Balozi Xu alisema China na Nigeria zilianzisha uhusiano wa kibalozi mwaka 1971, tangu hapo uhusiano wa kisiasa kati ya nchi hizo mbili siku zote unaendelea katika hali ya utulivu sana. Alisema:
Tangu uhusiano wa kibalozi uanzishwe kati ya China na Nigeria mpaka sasa, uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea katika hali ya utulivu kwa miaka mingi iliyoita. Hasa katika miaka kadhaa ya hivi karibuni, viongozi kati ya nchi hizo mbili walitembeleana mara kwa mara, takriban kila baada ya miaka miwili ujumbe wa ngazi ya juu wa serikali ya China unafanya ziara nchini Nigeria. Maofisa wakuu wa Nigeria hasa rais Obasanjo wana hisia nyingi za urafiki kwa China.
Balozi Xu alisema, China na Nigeria zote ni nchi zenye idadi kubwa ya watu na zote ni nchi zinazoendelea, ambazo zinakabiliwa na jukumu la kuendeleza uchumi, na nchi hizo mbili zina maoni ya pamoja kuhusu masuala mengi ya kimataifa. Alisema:
Kwa mfano China na Nigeria zina maoni ya pamoja kuhusu kulinda haki za binadamu, tunaona kwanza lazima kuhakikisha haki za kuishi na haki za maendeleo, na lazima kuondoa umaskini na kuendeleza uchumi. Kuhusu mambo ya kisiasa, uaminifu wa kisiasa kati ya nchi zetu mbili unaongezeka siku hadi siku, na uhusiano kati ya nchi hizo mbili unaendelea vizuri.
Balozi Xu aliona kuwa kutokana na uaminifu wa kisiasa unavyoongezeka siku hadi siku kati ya China na Nigeria, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwenye sekta ya uchumi nao pia unapanuka siku hadi siku. Mwaka jana thamani ya biashara kati ya China na Nigeria ilifikia dola za kimarekani bilioni 3. Balozi Xu alisema:
Makampuni kadha wa kadha ya China yameingia kwenye soko la Nigeria. Kwa mfano "Kampuni ya Zhongdi ya ng'ambo" ya China inashughulikia kazi ya kuchimba visima nchini Nigeria katika miaka mingi iliyopita, na imesifiwa na serikali ya Nigeria na wananchi wake. Na makampuni mengine ya China yanashughulikia ujenzi wa miradi mbalimbali nchini Nigeria.
Balozi Xu alisema mafanikio mengi yamepatikana katika ushirikiano kati ya China na Nigeria kwenye sekta za sayansi, elimu na utamaduni. Kampuni ya Changcheng ya China iliiuzia Nigeria satlaiti moja ya mawasiliano ya Dongfanghong No.4, hii ni mara ya kwanza kwa kampuni hiyo ya China kuuza satlaiti kwa nchi ya nje, satlaiti hiyo itarushwa mwezi Machi mwaka kesho. Alisema:
Satlaiti hiyo ya mawasiliano ni ya kwanza inayomilikiwa na wananchi wa Nigeria yaani wananchi wa Afrika, ambayo itasaidia Nigeria kuboresha hali ya mawasiliano ya habari na matangazo ya radio, pia itasaidia kuisaidia eneo zima la kusini mwa Sahara barani Afrika, hasa eneo la magharibi mwa Afrika.
Kutokana na jinsi mawasiliano kati ya China na Nigeria yanavyoongezeka, wanigeria wengi zaidi wanakuja China kufanya biashara, na nchini Nigeria watu wengi wanajifunza Kichina. Balozi Xu alisema hivi sasa vyuo vikuu vinne vya Nigeria vinawasiliano na ubalozi wa China nchini Nigeria kueleza matumaini ya kuanzishwa kwa vituo vya kutoa mafunzo ya lugha ya Kichina.
Alipozungumzia mustakabali wa maendeleo ya ushirikiano kati ya China na Nigeria, Balozi Xu alisema kutokana na jinsi uhusiano kati ya China na Nigeria unavyoendelea siku hadi siku, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta za uchumi na biashara, sayansi na teknolojia, utamaduni na elimu hakika utapata maendeleo makubwa zaidi.
|