Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-27 14:33:11    
Kwa mara ya kwanza nchi sita kujadili mswada wa azimio la vikwazo kwa Iran

cri

Nchi tano wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani, tarehe 26 zilifanya mkutano mjini New York kuujadili mswada wa azimio la kuiwekea vikwazo Iran. Wachambuzi wanaona kuwa huenda mjadala huo utakuwa wa muda mrefu.

Mswada huo ulioandaliwa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani umeamua kuiwekea vikwazo Iran kwa mujibu wa kipengele cha 41 kwenye ibara ya mlango wa saba ua Katiba ya Umoja wa Mataifa, lakini haukutaja kutumia nguvu za kijeshi. Mswada huo unaitaka Iran itekeleze mara moja azimio Nam. 1695 na kusimamisha shughuli za kusafisha uranium na kuzitaka nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zisisaidie Iran vitu vyote vinavyohusika na utengenezaji wa silaha za nyuklia na kuiwekea vikwazo fedha zake na kuwazuia watu husika kusafiri. Mswada umetoa onyo kwamba endapo Iran itaendelea kukataa kusimamisha shughuli za kusafisha uranium, Baraza la Usalama litaichukulia Iran hatua kali zaidi.

Kwa mujibu wa azimio Nam. 1695 lililotolewa mwezi Julai mwaka huu, Iran inapaswa kusimamisha shughuli za kusafisha uranium kabla ya tarehe 31 Agosti mwaka huu. Lakini katika miezi kadhaa iliyopita Iran imekuwa ikiendelea na shughuli hizo, na mazungumzo kati ya Umoja wa Ulaya na Iran pia hayakupata mafanikio yoyote. Zaidi ya hayo, serikali ya Iran tarehe 25 ilithibitisha kwamba imeanzisha kiwanda cha pili cha kusafisha uranium. Hii ina maana ya kuwa shughuli za Iran za kusafisha uranium zimepiga hatua nyingine.

Wakati nchi hizo zinapojadili mswada huo Russia ilijitokeza kuupinga. Waziri wa mambo ya nje wa Russia Sergey Lavrov anaona kwamba mswada huo haulingani na makubaliano ya nchi sita yaliyopatikana hapo mwanzo. Alisema lengo la nchi sita lilikuwa ni kuizuia Iran kupata teknolojia nyeti kabla ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kufanya vilivyo masuala yote husika. Bw. Lavrov alisisitiza kwamba ili kuyafanya mazunguzo yaendelee nchi sita zinapaswa kuwasiliana na Iran na utatuzi wa suala la nyuklia la Iran pia unategemea Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki.

Mbali na Russia, nchi nyingine pia zinatofautiana kuhusu mswada huo, tofauti yao ni kuhusu kutekeleza au kutotekeleza vikwazo hivi sasa dhidi ya Iran. Marekani inataka vikwazo hivyo vitekelezwe mara moja, na inaona kwamba la sivyo hadhi ya Umoja wa Mataifa itashuka. China inaona bado ni mapema kuichukulia hatua Iran. Kwenye mkutano na waandishi wa habari msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Liu Jianchao tarehe 26 alisema, China imo katika kutafiti mswada huo. Na kusema kwamba China siku zote inaunga mkono na kulinda mfumo wa kutoeneza silaha za nyuklia na kuna hali ya wasiwasi kutokea katika Mashariki ya Kati, inatetea kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo, na hatua za Baraza la Usalama zinapaswa kusaidia kutimiza lengo hilo.

Kutokana na tofauti kati ya nchi hizo kuhusu mswada huo, kabla ya mswada huo kuwasilishwa rasmi mbele ya Baraza la Usalama hakika utajadiliwa na kurekebishwa kwa mara kadhaa. Mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Bw. John Bolton baada ya mkutano wa nchi sita alisema, hii ni mara ya kwanza kubadilishana maoni, mjadala huo utaendelea tena wiki ijayo. Mwakilishi wa Russia Vitaly Churkin pia alisema kuna masuala mengi yanayohitaji kujadiliwa.

Idhaa ya kiswahili 2006-10-27