Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-10-27 20:41:37    
Mahojiano kati ya mwandishi wetu wa habari na Balozi wa Tanzania nchini China Bwana Ramadhani Mapuri

cri

Mwandishi: Mhesimiwa balozi, hivi karibuni Mkutano wa wakuu wa Baraza la urafiki kati ya China na Afrika utafanyika hapa Beijing, sijui waafrika wanategemea nini kutoka kwa mkutano huo?

Balozi: Tunategemea ushirikiano kupanuka zaidi. Tumekuwa na ushirikiano wa muda mrefu baina ya China na Afrika, hivi sasa tayari pande zote mbili zimefaidika na ushirikiano huo. Biashara kati ya Afrika na China imeongezeka kwa kiasi kikubwa sana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, imeongezeka kutoka dola za kimarekani bilioni 10 hadi bilioni 40 mpaka sasa, katika kipindi hicho tumeanzisha ushirikiano kati ya Afrika na China, kwa hivyo biashara imeongezeka hasa, kuongezeka kwa biashara hiyo ni kupitia utaratibu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika. China imeweza kuondoa ushuru kwa bidhaa za aina 190 kwa nchi za Afrika, hivyo bidhaa nyingi sasa zinaingia China bila ushuru. Sasa hivi mwelekeo ni kushirikiana katika kukuza utalii, wachina wameingia katika bara la Afrika kama watalii. Lakini tunatarajia kwamba baada ya mkutano huo ambao ajenda kuu ni kupanua ushirikiano hasa kutaka wachina waweze kuwekeza katika nchi zetu katika viwanda hasa vitakavyoongeza thamani ya bidhaa zetu za kilimo, ili badala ya kuagiza bidhaa ambazo hazijasindikwa, tuweze kuuza bidhaa zilizosindikwa, hii itakuwa faida mbili. Kwanza zenyewe zitaongeza thamani ya bidhaa, kuanzisha viwanda, watu wetu wataweza kupata ajira, tunataka wenzetu watuletee teknolojia, wenzetu China wamepiga hatua na kubadilisha kwa haraka maisha ya wananchi na uchumi wao unakuwa kwa haraka, tunatarajia tufaidike na teknolojia hizo hasa zitakazokifanya kilimo chetu kiwe cha tija zaidi kuliko sasa.

Mwandishi wa habari: Watu walisema, China ina urari mzuri na nchi nyingine za Afrika hazina urari mzuri, kuna juhudi zozote za kubadilisha hali hii?

Balozi: Kweli kabisa urari wa Afrika hasa wa zile nchi ambazo hazizalishi mafuta ni mzuri zaidi kwa upande wa China, ndiyo maana nasema lazima kupunguza ushuru wa bidhaa zinazosafirishwa kuja huku, wachina wajitahidi kuleta uwekezaji kuongeza thamani za bidhaa zetu ili bidhaa zitakuwa na thamani zaidi, mapato yetu yatakuwa makubwa zaidi, sisi kweli tunakabiliwa na changamoto, tungewahimiza wafanyabiashara wetu wasielekeze nguvu zao kuagiza vitu vilivyotengenezwa na China, bali kununua vitu vitakavyotumika katika kuzalisha bidhaa nchini Tanzania.

Mwandishi: Uhusiano kati ya Viongozi ni mkubwa zaidi kuliko uhusiano kati ya wananchi wa China na Afrika, je, kuna mambo yoyote ya kurekebisha hali hii?

Balozi: Nadhani mambo yanabadilika. Huko nyuma urafiki wetu ulianza kati ya serikali na viongozi wetu, hivi sasa urafiki huo umeshafika kwa wananchi, ukipata nafasi kwenda Guangzhou utakuta watanzania wengi. Kila kukicha hali inabadilika sasa hivi, hivi sasa watanzania wengi wameanza hata kufika Beijing, hawaishii Guangzhou tu, mchina wa kawaida na mtangazaji kama wewe kawaida wanashirikiana katika biashara, na nyumbani kwetu wachina wamejaa tele, wanakuja wawekezaji, wengine hata wanaofanya biashara ndogondogo ambapo hata wanapigiwa kelele, lakini ndio uhusiano unaanza hapo na utaongezeka changamoto. Tunatakiwa kufanya juhudi kubadilisha mahusiano yawe yanaendelea kukua kwa manufaa ya pande zetu mbili.