Mwezi Aprili mwaka huu Liberia, ambayo hivi sasa inafanya ujenzi mpya, ilipokea kikundi cha nne kutoka China cha jeshi kulinda amani la China lililoundwa na vikosi vya uhandisi, utibabu na uchukuzi. Hadi hivi sasa miezi zaidi ya 6 imepita tangu kikosi hicho kipelekwe huko, mwandishi wetu wa habari aliyeko nchini Liberia Bw. Zheng Yunfeng alikwenda huko kuwatembelea askari hao na kufanya mahojiano nao.
"Wachina, wema, wachina, wema."
Watoto kutoka shule ya tarafa moja iliyoko kaskazini mwa mashariki ya Liberia waliwalaki hivyo wanajeshi waliotoka China. Mkuu wa shule hiyo Bw. Henry alisema,
"Wanajeshi wa China walitusaidia kusawazisha kiwanja kinachotarajiwa kujengwa shule ya msingi, pia walitusaidia kurekebisha njia, hivi ni vitu muhimu sana."
Habari zinasema wanajeshi anaowashukuru Bw. Henry ni askari wa kikosi cha uhandisi cha jeshi la kulinda amani la China. Kazi zao muhimu ni kujenga barabara na kuzitunza. Barabara nyingi za nchi hiyo zimeharibika vibaya kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mingi. Hivyo kazi za kikosi cha uhandisi ni kubwa na ngumu, mara kwa mara walifanya kazi porini kwa muda wa miezi kadhaa. Naibu kiongozi wa kikosi cha uhandisi Bw. Chen Dajun alisema
"kazi ya kutengeneza barabara za hapa ni ngumu sana, msingi wa barabara hizo una mchanga na udongo mwingi, hivyo mvua ikinyesha, barabara hizo zinakuwa na matope mengi."
Kutokana na juhudi za askari wa kikosi hicho, barabara za zamani, ambazo magari yaliweza kwenda kwa mwendo wa kilomita 30 kwa saa, sasa yanaweza kwenda kwa mwendo wa kilomita 60 hadi 80 kwa saa. Mkuu wa mkoa wa Granda Gedeh, kilipo kikosi cha uhandisi, Bw. Christopher Bailey alipongeza sana mchango waliotoa askari wahandisi wa China kwa ujenzi wa huko. Alisema, "Tunawashukuru sana, uhusiano kati yetu na askari wahandisi wa China ni mzuri, tunawapenda, sisi ni kama watu wa ukoo mmoja."
Vilevile mwandishi wetu wa habari alikwenda kuwatembelea madaktari wa kikosi cha utibabu cha jeshi la kulinda amani la China. Kikosi hicho kina watu 43, lakini kinawahudumia wanajeshi na wakazi karibu elfu 5 wa huko. Mkuu wa kikosi hicho Bw. Sun Tiansheng alisema, madaktari na wauguzi wanafanya kazi kwa zamu kwa saa 24 kila siku, hawaogopi kazi ngumu, kitu kinachotishia usalama wao ni maambukizi ya ukimwi.
Bw. Sun alisema, "72% ya wagonjwa waliolazwa kwenye hospitali yao ni wagonjwa wa ukimwi, wakati kiasi cha 50 ya wagonjwa wanaokwenda kuwaona madaktari ni watu wenye virusi vya ukimwi, lakini vitu vya kinga tunavyotumia dhidi ya maambukizi ya ukimwi si vya kisasa sana."
Siku moja ya mwezi Septemba, askari mmoja kutoka Ethiopia alikwenda kwenye hospitali yao kutibiwa, askari huyo alikuwa ameambukizwa virusi vya ukimwi, na tena alikuwa ni mgonjwa wa kifua kikuu. Mkuu wa wauguzi wa hospitali hiyo Bibi Chen Haihua alitufahamisha kuwa, "siku ya pili baada ya askari huyo kulazwa katika hospitali hiyo, alikohoa damu na kuchafua shuka, sakafu na hata nguo ya mwuguzi. Lakini walichojali ni kuokoa maisha ya mgonjwa huyo. Baada ya kumaliza kazi, niliwaambia wauguzi waende haraka kubadilisha nguo iliyochafuliwa na damu yake na kuoga ili kujiepusha na hatari ya maambukizi ya virusi."
Kikosi cha uchukuzi kimekabidhiwa jukumu la kusafirisha vitu vya mahitaji kwa askari elfu 15 wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa nchini Liberia. Askari wa kikosi hicho wanafanyakazi bila kujali mchana au usiku. Hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu, jeshi hilo la China litamaliza kipindi chake cha kazi cha miezi 8 barani Afrika.
Idhaa ya Kiswahili 2006-11-01
|