Tokea pande tatu za China, Korea ya kaskazini na Marekani kukubali kwa kauli moja kuanzisha tena mazungumzo ya pande 6 katika kipindi cha hivi karibuni kinachozifaa pande 6, siku hizi nchi zinazohusika zinafanya juhudi za kidiplomasia bila kusita.
Tarehe 9 Oktoba Korea ya kaskazini ilitangaza kuwa imefanya majaribio ya nyuklia chini ya ardhi, baadaye China na pande nyingine zinazohusika zilifanya juhudi za kuzungumza na upande wa Korea ya kaskazini. Kutokana na pendekezo la upande wa China, viongozi wa ujumbe wa nchi za China, Korea ya kaskazini na Marekani zinazoshiriki kwenye mazungumzo ya pande 6 walifanya mkutano usio wa rasmi tarehe 31 Oktoba hapa Beijing, ambapo walijadili kuhusu lini mazungumzo ya pande 6 yatarudishwa, namna yatakavyofanyika na kujadili masuala gani. Lengo la kimsingi la mazungumzo hayo ni kuzitaka pande mbalimbali zitekeleze kihalisi ahadi zilizotoa katika taarifa ya pamoja iliyofikiwa kwenye duru la 4 la mazungumzo hayo mwezi Septemba mwaka jana. Katika taarifa hiyo ya pamoja, upande wa Korea ya kaskazini uliahidi kuacha silaha zote za nyuklia na mpango wa nyuklia wa hivi sasa, na kurudi mapema kwenye "Mkataba wa kutoeneza silaha za nyuklia"; upande wa Marekani ulithibitisha kuwa, Marekani haina silaha za nyuklia kwenye peninsula ya Korea, na haina nia ya kuchukua silaha za nyuklia au silaha za kawaida kuishambulia Korea ya kaskazini; Na Korea ya kaskazini ilitoa taarifa ikisema ina haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani, ambapo pande nyingine mbalimbali zilieleza kuheshimu hayo.
Tarehe 5 mwezi huu Marekani iliwatuma manaibu mawaziri wa mambo ya nje kwenda sehemu ya Asia ya kaskazini mashariki kufanya ziara ya muda mfupi, hatua kama hii ni nadra kuchukuliwa na Marekani. Hao ni manaibu mawaziri wa mambo ya nje hao wanaoshughulikia mambo ya siasa na mambo ya udhibiti wa silaha na usalama wa kimataifa. Walifanya ziara nchini Japan nakufika mji mkuu wa Korea kusini Seoul. Wizara ya mambo ya nje na biashara ya Korea ya kusini ilitangaza kuwa, manaibu mawaziri hao wa mambo ya nje wa Marekani watakuja pia Beijing. Na baada ya kufanya ziara nchini China, Japan na Korea ya kusini, pia watakwenda Russia kwa ziara. Na waziri wa mambo ya nje na biashara wa Korea ya kusini Bwana Pan Kimoh alifanya ziara nchini Japan kuanzia tarehe 5 hadi 6, na kubadilishana maoni na wahusika wa Japan kuhusu kuhimiza yaanzishwe tena mazungumzo ya pande 6 na kuhimiza Korea ya kaskazini iache mpango wa nyuklia. Tarehe 6 maofisa wa Russia na Korea ya kusini walifanya mazungumzo kuhusu mambo ya ulinzi huko Moscow. Habari nyingine zinasema, viongozi wa ujumbe wa Korea ya kusini, Marekani na Japan watakaohudhuria mazungumzo ya pande 6 watafanya mkutano mwanzoni mwa wiki ijayo ili kujadili mbinu za pande hizo tatu baada ya mazungumzo ya pande 6 kuanzishwa tena.
Katika mwaka mmoja uliopita Marekani iliiwekea vikwazo Korea ya kaskazini kwa kisingizio cha Korea ya kaskazini kurudufu kiharamu dola za kimarekani, ndiyo maana Korea ya kaskazini ilisusia mazungumzo ya pande 6, na kuweka sharti la kwanza la kuitaka Marekani iondoe vikwazo vya kifedha, halafu ndipo itaweza kurudi tena kwenye mazungumzo hayo; Korea ya kaskazini pia imedai kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani. Lakini Marekani inasema vikwazo hivyo havihusiani na mazungumzo ya pande 6, tena imekataa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Korea ya kaskazini, pande hizo mbili siku zote zilivutana sana. Habari zinasema, Korea ya kaskazini na Marekani zilipokutana kwenye mkutano usio rasmi wa pande tatu za China, Korea ya kaskazini na Marekani, zilionesha unyumbufu wa kiasi fulani kuhusu suala la fedha, na kufikia maelewano kuhusu kutatua suala hilo ndani ya mazungumzo ya pande 6.
Kutatua suala la nyuklia ya peninsula ya Korea kwa njia ya majadiliano na mazungumzo ili kuifanya sehemu ya peninsula ya Korea iwe sehemu isiyo na nyuklia, ni maoni ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa. Kazi ya dharura ni kuwa lazima yaanzishwe mapema mazungumzo ya pande 6, pande husika zinapaswa kuwa na udhati na unyumbufu ili kuendelea na juhudi za kuyawezesha mazungumzo hayo yaanzishwe tena mapema.
|