Pamoja na nyimbo na ngoma za furaha za kiafrika, mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2006 kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa umefunguliwa tarehe 6 mwezi Novemba kwenye makao makuu ya shirika la mpango wa mazingira la Umoja wa Mataifa yaliyoko Nairobi, mji mkuu wa Kenya. Wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 160 na maofisa wa Umoja wa Mataifa zaidi ya 6,000 wanashiriki kwenye mkutano huo. Katika muda wa mkutano huo, vitafanyika vikao kadhaa kuhusu suala la hali ya hewa ya dunia, ikiwa ni pamoja na mkutano wa 12 wa nchi zilizosaini "mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa" na mkutano wa 2 wa nchi zilizosaini "mapatano ya Kyoto". Suala muhimu linalofuatiliwa na mkutano ni namna ya kuzisaidia nchi za Afrika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa duniani.
Waziri wa mazingira wa Kenya, ambayo ni nchi mwenyekiti wa mkutano na nchi inayoandaa mkutano huo, Bw. Kivutha Kibwana alipotoa hotuba kwenye sherehe ya ufunguzi alisema, hali ya hewa ya dunia kubadilika kuwa joto, itaathiri utekelezaji wa lengo la maendeleo ya jamii kwa watu maskini kabisa barani Afrika, alitoa wito wa kutaka nchi zilizosaini mkataba huo zichukue hatua halisi kutatua suala la hali ya hewa duniani kubadilika kuwa joto.
"Kila nchi ina jukumu lake, lakini iwe nchi iliyoendelea au ni nchi inayoendelea inanufaika kwa pamoja katika shughuli za kukabili uharibifu unaoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa, nchi zote zinatakiwa kutoa ahadi ya pamoja, ambayo ni juu ya msingi wa haki na usawa kwa kulingana na hali halisi ya kila nchi."
Kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa ya dunia, jumuiya ya kimataifa imepitisha "mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya hali ya hewa" na "mapatano ya Kyoto", ambazo zimethibitisha kanuni za kisheria kuhusu ushirikiano wa kimataifa. "Mapatano ya Kyoto" ambayo ilianza kazi mwezi Februari mwaka jana, yanazitaka nchi 36 za viwanda zipunguze utoaji wa hewa ya carbon dioxide kwa 5% nyingine juu ya msingi wa mwaka 1990 katika kipindi cha kwanza cha ahadi zilizotoa kati ya mwaka 2008 na mwaka 2012. Namna ya kupunguza zaidi utoaji carbon dioxide katika kipindi cha pili cha baada ya mwaka 2012, yaani suala la "baada ya Kyoto" ni suala lililowekewa mkazo kwenye mkutano wa mwaka huu kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa. Naibu mkurugenzi wa idara ya mikataba ya wizara ya mambo ya nje ya China Bw. Su Wei alitoa maelezo kuhusu suala hilo, akisema,
"mkutano wa nchi zilizosaini mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa unakusudia kutatua hususan masuala mawili, la kwanza ni namna ya kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa, jambo kubwa zaidi ni kujadili uanzishaji wa mfuko wa fedha unaoendana na mabadiliko ya hali ya hewa ili kutoa msaada wa fedha kwa nchi za Afrika hususan zile zilizoko nyuma kabisa kimaendeleo kuchukua hatua zinazoendana na mabadiliko ya hali ya hewa; Jambo lingine muhimu ni kuhimiza uhamishaji wa teknolojia, kwani teknolojia ya kisasa ni njia ya kimsingi ya kutatua suala la mabadiliko ya hali ya hewa. Nchi zilizoendelea zinawajibika kuruhusu kuhamisha teknolojia za kisasa ili kupunguza utoaji wa hewa inayofanya hewa ya dunia kubadilika kuwa joto."
Mkurugenzi mtendaji wa shirika la mpango wa mazingira la Umoja wa Mataifa Bw. Achim Steiner alisema, kufanya mkutano huo kwenye nchi ya Afrika ni kutaka jumuiya ya mataifa ifuatilie kwa pamoja changamoto zinazoletwa na mabadiliko ya hali ya hewa kwa Afrika.
|