Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-08 18:35:20    
China na Umoja wa Ulaya zafikia maoni ya pamoja kuhusu masuala kadhaa, lakini migongano kati yao bado ipo

cri

Waziri wa biashara wa China Bwana Bo Xilai na mjumbe wa Kamati ya biashara ya Umoja wa Ulaya Peter Mandelson tarehe 7 walifikia maoni ya pamoja kuhusu masuala kadha wa kadha kwenye mkutano wa uchumi na biashara wa pande mbili za China na Umoja wa Ulaya uliofanyika hapa Beijing.

Maoni hayo ya pamoja yalifikiwa katika hali isiyofurahisha sana katika uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya pande hizo mbili kwa hivi sasa. Lakini hivi sasa Umoja wa Ulaya umekuwa mwenzi wa kwanza wa biashara kwa China, na China ni mwenzi wa pili wa biashara kwa Umoja wa Ulaya. Mwaka 2005, thamani ya biashara kati ya China na Umoja wa Ulaya ilizidi dola za kimarekani bilioni 200, mambo ya biashara yamekuwa mambo muhimu sana katika maendeleo ya uchumi wa kila upande. Ndiyo maana, ingawa kuna migongano mbalimbali kati ya China na Umoja wa Ulaya kuhusu uchumi na biashara, lakini pande hizo mbili zimetambua umuhimu wa kutumia njia ya mashauriano kwa kuondoa migongano na kudumisha maendeleo ya kawaida ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara. Waziri wa biashara wa China Bwana Bo Xilai alisema:

Pande mbili zetu zinapokutana na matatizo ya biashara hasa mikwaruzano ya kibiashara, tunapaswa kufanya majadiliano mapema iwezekanavyo, ili kujitahidi kadiri tuwezavyo kutatua matatizo baada ya kufanya majadiliano ya kirafiki.

Bwana Peter Mandelson pia alisema uhusiano wa kiuchumi na kibiashara ni injini kubwa ya uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya, Umoja wa Ulaya unatilia maanani sana uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na China, na siku zote unapenda kutatua ipasavyo matatizo ya kibiashara kwa kupitia juhudi za kupanua ufunguaji mlango, kufanya mazungumzo na majadiliano ili kusukuma mbele siku hadi siku maendeleo ya uchumi wa pande hizo mbili.

Kulinda hakimiliki ya ujuzi ni suala muhimu analotaka kulizungumzia Bwana Mandelson katika ziara yake hiyo nchini China. Alipokuwa na mazungumzo na waziri wa biashara wa China alieleza ufuatiliaji wa Umoja wa Ulaya kuhusu kuimarisha utekelezaji wa sera ya kulinda hakimiliki ya ujuzi, na kampuni za China kutoa malipo wakati zinapotumia hataza za nchi za nje. Waziri Bo Xilai alipojibu maswali alijulisha nia imara na hatua za China katika kuimarisha kazi ya kulinda hakimiliki ya ujuzi. Alisema hivi sasa, vituo vya huduma vya utoaji ripoti kuhusu vitendo vya kukiuka hakimiliki ya ujuzi vimeanzishwa katika miji 50 muhimu ikiwemo Beijing na Shanghai. Baada ya mazungumzo hayo pande mbili China na Umoja wa Ulaya zilisaini kumbukumbu za maelewano kuhusu kuimarisha ushirikiano wa kulinda hakimiliki ya ujuzi.

Kuitaka China itekeleze ahadi zake ilizotoa wakati wa kujiunga na shirika la biashara duniani, na kufungua zaidi soko, hili pia ni lengo muhimu la Bwana Mandelson kufanya ziara hii nchini China. Alisema:

Umoja wa Ulaya na mimi mwenyewe tunaona kuwa, tokea China ijiunge na shirika la biashara duniani mwaka 2001, China imeanzisha kazi nyingi ili kutekeleza majukumu yake, na imepata maendeleo halisi, China inafanya mageuzi. Lakini katika sekta muhimu kadha wa kadha, pande zetu mbili bado zina masuala kadhaa ambayo hayajatatuliwa, kama vile vizuizi vya kibiashara na kadhalika. Lakini tunafanya juhudi za pamoja ili kuyatatua.

Waziri wa biashara wa China Bwana Bo Xilai alisema, China imetekeleza kwa makini ahadi zake ilizotoa kwa shirika la biashara duniani, kiwango cha ushuru wa forodha kimepungua kwa kiasi kikubwa, na China imetoa mchango mkubwa katika kufungua soko lake. Amewataka watu wanaotaka China ifungue zaidi soko waweze kuona mafanikio yaliyopatikana nchini China, na waweze kuzingatia kuwa China bado ni mwanachama mpya wa shirika la biashara duniani, na bado ni nchi inayoendelea. Pia ameutaka Umoja wa Ulaya utambue mafanikio halisi ya China na kutambua kwa haki hadhi kamili ya uchumi wa soko huria ya China.