Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-09 18:33:17    
Champa Tsondre na shule yake ya kulea watoto

cri

Kabla ya kuingia shule ya kulea watoto ya Caiquan, sauti nyororo za watoto zilikuwa zilisikika, wanafunzi wa shule hiyo walikuwa wakiimba wimbo wa shule hiyo huku wakiwa wameshikana mikono.

Hiyo ni shule maalumu ambayo inawapokea watoto wenye ulemavu na watoto yatima, ambayo ipo mjini Lhasa, mkoa unaojiendesha wa kabila la Watibet. Mkuu wa shule hiyo ni Bw. Champa Tsondre, ambaye pia ni mkuu wa kiwanda cha kazi za mikono cha Kitibet. Bw. Champa Tsondre ni mrefu, ana sura nzuri na kuonekana kuwa mkarimu na mchangamfu. Kama walivyokuwa watoto wengine kutoka kwenye familia zenye umaskini kabla ya Tibet kupata ukombozi mwaka 1951, Champa Tsondre haikupata nafasi ya kwenda shule, badala yake alijifunza kutoka kwenye vitabu vya dini ya kibudhaa kwa miaka ya kadhaa. Baadaye Champa alipokuwa kijana alifanya kazi mbalimbali, zikiwemo useremala, ushonaji viatu, na pia aliwahi kuwa mchezaji. Mwaka 1986 Champa aliteuliwa kuwa mkuu wa kiwanda cha kutengeneza viatu mjini Lhasa.

Alishuhudia hali ngumu ya watoto yatima na watoto wenye ulemavu mitaani ambao walikosa nafasi ya kupata elimu, pamoja na vijana wenye ulemavu wanaoombaomba mitaani kutokana na kukosa ajira, Champa aliamua wa kuwasaidia.

Bw. Champa aligeuza kiwanda chake cha kutengeneza viatu kuwa kiwanda cha ufadhili kinachojihusisha na kazi za mikono za Kitibet. Aliwashirikisha vijana walemavu na watoto yatima zaidi ya 20, kuwapa nafasi ya kusoma, kujifunza ufundi wa uchoraji, uchongaji na utengenezaji viatu, ili waweze kujipatia lishe kwa kutegemea ufundi wa kazi waliopata.

Mwaka 1993 Bw. Champa Tsondre alitoa Yuan zaidi ya laki 4 ambazo ni akiba yake ya miaka mingi, kuanzisha shule ya kulelea watoto yatima na watoto wenye ulemavu ya Caiquan. Ndiyo maana akawa mkuu wa shule hiyo, anawapatia watoto hao chakula na malazi na kuwasomesha, vile vile anawafundisha ufundi mbalimbali wa kabila la Watibet, ili wawe na uwezo wa kujitegemea na kulitumikia taifa. Bw. Champa alisema "Kila jumapili natumia saa mbili kuwaelezea watoto hao jinsi watoto yatima na walemavu walivyodharauliwa na kuishi katika hali ngumu kabla ya ukombozi wa Tibet. Hivi sasa tuna maisha mazuri, tunapaswa kuishukuru jamii mpya na kusoma kwa bidii ili kulitumikia taifa. Kutokana na maelezo yangu, watoto wanatiwa moyo sana na kusoma kwa bidii, watoto wengi waliohitimu shule ya Caiquan waliandikishwa kwenye shule nzuri, na kusifiwa na watu wengine."

Hivi sasa shule hiyo ya Caiquan ina wanafunzi wapatao 145, Bw. Champa anawatunza vizuri watoto hao kama baba yao mzazi. Na watoto hao wanamwita baba badala ya mkuu wa shule.

Droje Tseten ni mmoja kati ya mwanafunzi hao. Baba yake mzazi alifariki dunia alipokuwa mtoto mchanga, mama yake mzazi pia alifariki dunia alipokuwa na umri wa miaka 6. Mtoto huyo alikumbusha akisema (sauti 3) "Kuingia shule ya Caiquan, kwa mara ya kwanza nilipata familia kubwa ya namna hii na ndugu wengi, kwa mara ya kwanza niliweza kula mpaka nikashiba, na ilikuwa mara ya kwanza kwenda darasani, mara ya kwanza kumwona mwalimu na kupewa vitabu vipya vya masomo, vile vile ilikuwa ni mara ya kwanza kufahamu taifa letu linaitwa China. Mimi niliona mambo mengi kwa mara ya kwanza katika shule ya Caiquan. Hivi sasa nimesoma na kuishi hapa shuleni kwa miaka 6, mimi na wenzangu tunaona furaha kuishi hapa, tumepata ujuzi mwingi na kufundishwa tabia njema."

Shule ya Caiquan imepata misaada ya serikali ambayo inampa kila mtoto posho Yuan 200 kwa mwezi, na watoto wakiugua idara za afya zinawatibu kwa wakati. Kitendo cha Bw. Champa kiligusa hisia za watu wengi na kuwavutia walimu kadhaa ambao wanajitoleza kufanya kazi ya ualimu katika shule ya Caiquan. Mwalimu Dekyi Zholma amefanya kazi kwenye shule hiyo kwa mwaka mmoja, alieleza kuwa anafurahia kazi hiyo. Alisema (sauti 4) "Nina uzoefu wa kufanya kazi ya ualimu kwa miaka 10, na nimefanya kazi kwenye shule ya Caiquan kwa zaidi ya mwaka mmoja. Hapa shuleni masomo ni tofauti na yale ya shule nyingine, kwani wanafunzi wa huku ni walemavu, baadhi yao hawawezi kusikia, baadhi yao hawawezi kuona na wengine ni watoto yatima, pia kuna watoto ambao wana umri wa zaidi ya miaka 10 lakini hawajawahi kwenda shule. Hata hivyo watoto hao walikuwa na bidii kubwa katika masomo. Mkuu wa shule yetu anawatunza watoto vizuri na kuchapa kazi kwa ajili yao, naona ni fahari sana kwangu kufanya kazi ya ualimu katika shule ya Caiquan."

Watoto yatima na watoto wenye ulemavu ni kundi maalumu, kwa hiyo ili aweze kuwaelimisha Bw. Champa alijifunza uzoefu na mbinu za kisasa za kuwafundisha watoto zilizotumika katika shule za kuwalea watoto wenye ulemavu zilizopo katika sehemu nyingine za China. Kwa kufuata hali halisi ya Tibet, Bw. Champa alianzisha mpango maalumu wa kuwafundisha watoto hao.

Hivi sasa imetimiza miaka zaidi ya 10 tangu shule ya kuwalelea watoto ya Caiquan ianzishwe. Katika kipindi hicho watoto wengi waliohitimu kwenye shule hiyo walifaulu mitihani ya kujiunga na shule za sekondari na vyuo vikuu. Mafanikio ya watoto hao yanamfurahisha sana Bw. Champa Tsondre, ambaye anaona kuwa jasho lake halikupotea bure.

Idhaa ya kiswahili 2006-11-9