Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-10 19:50:39    
Mkahawa wa kiafrika wa Pilipili unaowavutia wachina wengi mjini Beijing

cri

Karibu na daraja la Yansha lililoko Eneo la Chaoyang mjini Beijing, kuna mkahawa mmoja wenye mtindo pekee wa Afrika, mhakawa huo ulipewa jina la kiswahili Pilipili, ambalo linajulikana mjini Beijing, kwani ujenzi wa mkahawa huo pamoja na jina lake vyote vinaonesha umaalum wa Afrika. Paa na kuta za mkahawa huo zimefunikwa kwa manyasi ya artemisia kutoka Afrika ya Kusini. Wateja wakiingia mkahawani, wataona sanaa mbalimbali kutoka Afrika zimewekwa ndani ya mkahawa, ambapo wataburudishwa kwa muziki wa Afrika unaosikika kwenye mkahawa na kuhisi harufu nzito ya usanii wa Afrika.

Mkahawa Pilipili ni mkahawa wa kwanza wa kipekee wenye mtindo wa Afrika mjini Beijing. Imefahamika kuwa mkahawa huo ulianzishwa na Kampuni ya dawa ya Holley-Cotec ya Beijing, ambayo dawa yake ya Cotecxin ilitoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria barani Afrika. Kwa nini Kampuni hiyo inayotengeneza dawa na kufanya biashara za dawa siku zote ilianzisha mkahawa huo? Mwandishi wetu wa habari alikwenda kwenye mkahawa wa Pilipili na kufanya mahojiano na meneja wa kampuni ya uenezi wa utamaduni ya Pilipili ya Beijing Bw. Zhang Lichun.

Bw. Zhang Lichun alisema, katika siku nyingi zilizopita, kampuni hiyo imegundua kwa kupitia biashara yake na nchi mbalimbali za Afrika kuwa, ingawa upo urafiki mkubwa kati ya China na nchi mbalimbali za Afrika, lakini shughuli za kiutamaduni kati ya raia na raia bado hazitoshi. Katika shughuli zake za biashara barani Afrika, Kampuni ya dawa ya Holley-Cotec imekuwa na hisia nyingi za urafiki kwa Afrika, ndiyo maana, kampuni hiyo iliamua kufanya juhudi zake kwa kuhimiza maingiliano ya kiutamaduni kati ya wananchi wa China na Afrika.

Alisema,"Sanaa za Afrika, ngoma na muziki za Afrika pamoja na vyakula vya Afrika vyote ni vyenye umaalum pekee. Kampuni ya dawa ya Holley-Cotec ilianzisha kampuni ya uenezi wa utamaduni ya Pilipili na kuanzisha Mkahawa wa Pilipili chini ya kampuni hiyo, madhumuni yake ni kuwajulisha wachina sanaa za Afrika, na utamaduni wa Afrika, ili wachina waijue zaidi Afrika."

Bw. Zhang Lichun alieleza kuwa katika kipindi cha mwanzo, wateja waliokwenda kwenye mkahawa wa Pilipili wengi walikuwa ni watu wa nchi za nje na wachina waliowahi kufika Afrika, na wachina wengi ambao hawajawahi kufika Afrika hawafahamu vyakula vya Afrika. Kufuatana na ongezeko la mawasiliano ya kiraia kati ya China na Afrika katika miaka kadhaa ya karibuni, wachina wengi zaidi wameanza kulijua zaidi bara la Afrika, ambapo wateja wengi zaidi na zaidi walianza kwenda kwenye mkahawa wa Pilipili.

Mkahawa huo licha ya kupika Ugali, FuFu, nyamachoma, mishikaki ya samaki, kuku wa kukaangwa na vyakula vingine vyenye mtindo wa kipekee wa Afrika, Mkahawa wa Pilipili pia unaendesha mara kwa mara maonesho ya nyimbo na ngoma ya nchi mbalimbali za Afrika. Bw. Zhang Lichun alisema jukumu la mkahawa huo ni kuhimiza maingiliano ya kiutamaduni kati ya wananchi wa China na wa Afrika.

Alisema  "tulishirikiana na balozi za nchi mbalimbali za Afrika nchini China na kuendesha wiki ya utamaduni wa nchi mbalimbali za Afrika mara kwa mara, na kuwajulisha wachina utamaduni na sanaa, mila na desturi, vivutio vya utalii na vyakula vitamu vya nchi mbalimbali za Afrika."

Kwenye Mkahawa wa Pilipili, mwandishi wetu wa habari alikutana na wachoraji wanne wa picha za Tingatinga kutoka Tanzania. Wachoraji hao wanne walikuja Beijing kutokana na mwaliko wa Kampuni ya uenezi wa utamadunih ya Pilipili, na kuonesha picha zao za Tingatinga. Picha za mtindo wa Tingatinga zilivumbuliwa na mchoraji wa Tanzania Bw. Tingatinga, ambazo ni picha zenye mvuto pekee kwenye sehemu ya Afrika ya mashariki.

Mchoraji wa Tanzania Bw. Simon Clement alimwambia mwaandishi wetu wa habari kuwa hii ni mara yake ya kwanza kuja China. Ingawa wachina hawafahamu vizuri picha za Tingatinga, lakini yeye anaona furaha kupata fursa ya kuonesha picha zake kwa marafiki wa China. Vilevile alieleza maoni yake kuhusu mawasiliano ya utamaduni kati ya wananchi wa China na Afrika.

Alisema,  "Wachina wengi wanafanya kazi nchini Tanzania, na wanatusaidia. Na sisi Watanzania wengi pia tumekuja China kueneza utamaduni wa Afrika. Naona waafrika na wachina tunaelewana na kusaidiana kutokana na utamaduni wetu wenye umaalum tofauti. Naona ushirikiano vilivyo kati yetu unatunufaisha kweli. Ni matumaini yangu kuwa ushirikiano huo utaendelea na kuimarishwa siku hadi siku.

Kwenye mkahawa huo mwaandishi wa habari wetu alikutana na wateja wengi wa China, na wengi kati yao ni vijana ambao bado hawajawahi kufika Afrika. Walimwambia mwaandishi wetu wa habari kuwa mwanzoni walikuwa na hamu ya kuonja vyakula vya Afrika, hivyo walikwenda kwenye mkahawa huo wenye mtindo pekee wa Afrika, baadaye waliona kuwa wanapenda vitu vyote kwenye mkahawa huo pamoja na vyakula, na vitu vya sanaa na maonesho ya nyimbo na ngoma vinawavutia zaidi. Bi. Bai alipohojiwa na mwaandishi wetu wa habari alisema,

"Vitu vyote hapa ni vya ajabu, na ninavipenda sana. Utamaduni wa Afrika unanivutia na ninapenda kuufahamu zaidi. Nina matumaini kuwa maingiliano ya kiutamaduni ya aina mbalimbali yatafanyika siku zijazo, ili kuwawezesha wachina wengi zaidi wapate fursa za kujua utamaduni wa Afrika. Naona mustakabali wa maendeleo ya utamaduni wa Afrika nchini China ni mpana sana. "

Kwenye mahojiano hayo, Bw. Zhang Lichun alisema kampuni ya uenezi wa utamaduni ya Pilipili ya Beijing ina imani kubwa kuhusu mustakabali wa maingiliano ya utamaduni kati ya China na Afrika, pia alizungumzia kwa furaha mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika utakaofanyika tarehe 4 hapa Beijing. Alisema,

"Tutafanya maonesho ya utamaduni wa Afrika katika kipindi cha mkutano wa wakuu wa baraza hilo. Kahawa za Ethiopia, vivuitio vya utalii vya Misri, mvinyo na almasi za Afrika ya kusini, pamoja na vivutio vya utalii vya Zimbabwe, vyote vitaoneshwa kwenye maonesho hayo. "

Bw. Zhang Lichun alidokeza kuwa kampuni ya Holley-Cotec imeamua kuimarisha zaidi maingiliano ya utamaduni kati ya wananchi wa China na Afrika. Alieleza imani yake kuwa mkutano wa wakuu wa baraza hilo hakika utaleta "wimbi la Afrika" nchini China, pia utaleta fursa nyingi za maendeleo ya maingiliano ya utamaduni kati ya wananchi wa China na Afrika.