Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-13 16:48:49    
Waziri mkuu wa Israel afanya ziara nchini Marekani

cri
Waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert tarehe 12 aliwasili huko Washington na kuanza ziara yake ya pili nchini Marekani tangu ashike madaraka. Suala la nyuklia la Iran na hali ya Palestina na Israel ni masuala muhimu yatakayojadiliwa wakati wa ziara hiyo. Bw. Olmert anafanya ziara hiyo wakati uchaguzi wa Marekani wa kipindi cha katikati umemalizika hivi karibuni, hivyo Bw. Olmert anatumai kupata mwelekeo wa sera za Marekani kuhusu Mashariki ya Kati baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo.

Katika ziara hiyo Bw. Olmert alikuwa na mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bibi Condoleezza Rice tarehe 12 baada kuwasili nchini Marekani, na tarehe 13 atakuwa na mazungumzo na rais George Bush wa Marekani kwa saa moja. Pia atakutana na maofisa waandamizi wa serikali ya Marekani, na kwenda Los Angeles kuhudhuria Mkutano wa wayahudi.

Bw. Olmert alipoulizwa kuhusu suala la nyuklia la Iran kabla ya kuanza ziara hiyo alisema, Israel inaunga mkono "Pendekezo la kusalimu amri" lililotolewa na jumuiya ya kimataifa kwa ajili ya kuzuia Iran kuendeleaza silaha za nyuklia, lakini alisema Iran haitakubali pendekezo hilo kama pendekezo hilo halitaifanya Iran iwe na wasiwasi kutokana na matokeo mabaya yanayoweza kuipata baada ya kuendeleza mpango wake wa nyuklia. Alisema kanuni ya Israel ni kuifanya serikali ya Iran na wananchi wake watambue kuwa, watapata hasara kubwa kama hawatafanya ushirikiano na jumuiya ya kimataifa.

Maneno hayo ya Bw. Olmert yanachukuliwa ni kauli kali zaidi ya Israel kuhusu suala la Iran. Ofisa wa serikali ya Israel alidokeza kuwa, Bw. Olmert atajadiliana na rais Bush kuhusu kuunda muungano wa kimataifa wa kukabiliana na Iran, na kufikia mapatano kuhusu suala la nyuklia la Iran.

Kuhusu suala la Palestina na Israel, wachambuzi wanafuatilia msimamo wa Bw. Olmert kuhusu mpango wake wa kuondoa jeshi la Israel kutoka kando ya magharibi ya mto Jordan alioutoa wakati alipofanya ziara nchini Marekani wakati uliopita. Kwani baada ya askari wa jeshi la Israel kutekwa nyara mwaka huu na kutokea kwa vita vya Lebanon, Bw. Olmert alitangaza waziwazi kuwa kuendelea na majadiliano kuhusu mpango wa kuondoa jeshi la Israel hakulingani na hali ilivyo ya hivi sasa. Aidha kutokana na nia ya kuimarisha hadhi yake ya kisiasa, Bw. Olmert alikiingiza chama cha mrengo wa kulia cha Israel "Yisrael Beitenu" kwenye serikali yake mwezi uliopita, hali ambayo inakwamisha hatua ya utekelezaji wa mpango huo.

Ili kuondoa wasiwasi ya watu kuhusu suala hilo, Bw. Olmert alisema kabla ya kuanza ziara nchini Marekani kuwa, hajabadilisha maoni ya kuondoa jeshi kutoka kando ya magharibi ya mto Jordan, na amejiandaa kutoa idhini katika suala la ardhi. Pia alisema anapenda kuwaachia huru wapalestina wengi wanaofungwa na Israel, na kufanya juhudi za kuimarisha hadhi ya mwenyekiti wa Mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas. Bw. Olmert pia ameahidi kuwa, atashikilia njia ya kufanya mazungumzo na Palestina kutokana na hali yoyote.

Lakini serikali ya Israel na wachambuzi hawana matumaini makubwa na ziara hiyo ya Bw. Olmert. Baada ya uchaguzi wa kipindi cha katikati wa Marekani, chama cha Republican cha Bush kimepoteza udhibiti wa baraza la juu na la chini la bunge kutokana na vita dhidi ya Iraq. Aidha Rais Bush amemchagua waziri mpya wa ulinzi, hali ambayo inaonesha kuwa sera ya Marekani kuhusu Mashariki ya Kati inaweza kubadilika, na Bw. Olmert anataka kujua Marekani itachukua hatua gani mpya. Maofisa kadhaa wa Israel wanasema kuwa, kutokana na hali hiyo lengo la ziara ya Bw. Olmert ni kufahamu tu mwelekeo wa sera za Marekani kuhusu Mashariki ya Kati.

Idhaa ya Kiswahili 2006-11-13