Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-14 14:54:58    
Makundi yote ya kisiasa yakubaliana Bw. Mohammad Shubair awe waziri mkuu wa serikali mpya nchini Palestina

cri
Makundi ya Hamas na Fatah nchini Palestina tarehe 13 yalikubaliana na pendekezo la kumteua Bw. Mohammad Shubair awe waziri mkuu wa serikali mpya ya serikali ya Palestina. Bw. Mohammad Shubair aliwahi kuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiiislamu cha Gaza. Ofisa mmoja wa ngazi ya juu wa kundi la Hamas alisema Bw. Shubair amekubali kuteuliwa kuwa waziri mkuu. Baada ya mazungumzo na migogoro ya umwagaji damu iliyodumu kwa nusu mwaka, hatimaye makundi hayo yamepiga hatua katika suala la kuunda baraza jipya la mawaziri.

Bw. Shabir alizaliwa mwaka 1946 huko Gaza, na aliwahi kusoma katika chuo kikuu cha matibabu nchini Misri na alipata shahada ya tatu nchini Marekani. Kisha alirudi Gaza na kuanzia mwaka 1993 alikuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gaza na mwaka jana alistaafu.

Bw. Shubair ni mtu mwenye msimamo wa kati kisiasa na ana uhusiano mzuri na makundi ya Hamas na Fatah. Alipokuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Gaza maofisa wengi waandamizi wa Hamas walifundisha katika chuo hicho, na waziri mkuu wa sasa Bw. Ismail Haniyeh pia aliwahi kuwa mkurugenzi wa ofisi ya Shubair. Bw. Shubair pia alikuwa na uhusiano wa karibu na Fatah na alikuwa mgeni wa mara kwa mara nyumbani kwa kiongozi wa zamani wa Palestina Arafat. Baada ya Arafat kufariki dunia Shubair aliendelea na maingiliano na Bw. Abbas aliyechukua nafasi ya Bw. Arafat. Shubair hakuwahi kuonesha msimamo wake hadharani kuhusu Israel, lakini alipohojiwa na waandishi wa habari wa gazeti la Haaretz la Israel alisema, akiteuliwa kuwa waziri mkuu atachukua "hatua halisi".

Ofisa mmoja wa Palestina alidokeza kuwa, kama Bw. Shubair akichaguliwa kuwa waziri mkuu, ataongoza baraza litakaloundwa na watu huru. Hivi sasa makundi ya Hamas na Fatah yanajadiliana kuhusu uchaguzi wa mawaziri na ugawaji wa madaraka. Habari zinasema kundi la Hamas litapendekeza mawaziri kumi, na kundi la Fatah litapendekeza mawaziri watano. Mtaalamu wa kiuchumi anayeheshimiwa sana Bw. Salam Fayyad atakuwa waziri wa fedha, Bw. Ziad Abu Amr atakuwa waziri wa mambo ya nje, na watu hao wawili wote ni watu huru. Waziri wa mambo ya ndani na waziri wa habari bado hawajaamuliwa.

Bw. Shabi akichaguliwa kuwa waziri mkuu atakabiliwa na changamoto ambayo serikali yake licha ya kukubaliwa na makundi mbalimbali ya kisiasa, ni lazima ikidhi matakwa ya jumuyia ya kimataifa ili kuendelea kupata misaada ya fedha iliyokatwa kwa zaidi ya nusu mwaka. Watu wa Palestina wana matumaini makubwa kuwa serikali mpya itaweza kuondoa migogoro kati ya makundi na kupata utulivu wa taifa.

Kutokana na hali ya hivi sasa Israel na nchi za Ulaya zinaunga mkono kuundwa kwa serikali ya muungano wa Palestina, lakini zinatetea kuwa ni lazima serikali hiyo ikidhi matakwa yao matatu, yaani kuitambua Israel, kuacha vitendo vya kijeshi na kutambua mikataba yote iliyosainiwa kati ya Palestina na Israel. Waziri mkuu wa Israel alisema, mradi tu kundi la Hamas likiridhia matakwa hayo matatu atakubali kufanya mazungumzo na serikali mpya ikiwa ni pamoja na wajumbe wa Hamas.

Hivi sasa serikali ya Palestina bado haijatangaza rasmi uteuzi wa waziri mkuu, na Bw. Shubair pia alisema hajapata taarifa yoyote rasmi ya kuteuliwa. Kuweza au kutoweza kutimiza umoja wa kitaifa bado ni kitandawili, lakini pande zote zina matumaini makubwa na serikali mpya. Waziri mkuu wa Zamani Ahmed Qurie alisema katika siku za karibuni hali ya siasa nchini Palestina itabadilika na itaingia katika kipindi kipya.

Idhaa ya Kiswahili 2006-11-14