Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-14 19:44:16    
Ni kwanini pato linalotokana na uuzaji wa bidhaa nje la China linaongezeka kwa mfululizo?

cri

Takwimu zilizotolewa na forodha ya China zinaonesha kuwa, thamani ya biashara ya nje ya China iliweka rekodi mpya katika mwezi Agosti mwaka huu, ambapo thamani ya usafirishaji bidhaa kwa nchi za nje kwa mara ya kwanza ilizidi dola za kimarekani bilioni 90 na kufikia bilioni 90.77, wakati thamani ya uagizaji bidhaa kutoka nje kwa mara ya kwanza ilizidi dola za kimarekani bilioni 70 na kufikia bilioni 71.97.

Pamoja na ongezeko kubwa la biashara ya nje ya China suala la kukosa uwiano wa biashara ya nje limejitokeza kwa udhahiri. Katika mwezi Juni mwaka huu, thamani ya uuzaji bidhaa kwa nchi za nje ilikuwa kubwa kuliko bidhaa zilizoagizwa kutoka nchi za nje kwa dola za kimarekani bilioni 14.5, mwezi Julai ilikuwa dola za kimarekani bilioni 14.6 na dola za kimarekani bilioni 18.8 katika mwezi Agosti, ambazo zilikuwa rekodi mpya kabisa kwenye historia ya biashara ya nje ya China.

Katika mwaka uliopita, thamani ya bidhaa zilizosafirishwa na China kwa nchi za nje ilikuwa kubwa kuliko thamani ya bidhaa zilizoagizwa na China kutoka nje, ambayo ilizidi dola za kimarekani bilioni 100, na kuwa rekodi mpya kabisa kwenye historia. Tofauti hiyo ya biashara toka mwezi Januari hadi Agosti mwaka huu ilifikia dola za kimarekani bilioni 94.65, ambayo inakaribia ile ya mwaka mzima uliopita. Ofisa husika wa idara biashara ya nje ya wizara ya biashara ya China alisema, hali hiyo huenda itaendelea katika siku za baadaye, na pengine tofauti hiyo itazidi dola za kimarekani bilioni 20 katika mwezi fulani mwaka huu, na tofauti ya thamani ya biashara ya mwaka huu mzima itaweka rekodi mpya katika historia.

Mtaalamu wa ofisi ya takwimu ya idara kuu ya forodha akifanya uchambuzi alisema, moja ya sababu za kuwepo na ongezeko kubwa la usafirishaji wa bidhaa nchi za nje katika miezi michache ya karibuni ni viwanda kuwa na wasiwasi kwamba huenda serikali itapunguza fedha za kodi zinazorudishwa kwa baadhi ya bidhaa zinazosafirishwa nchi za nje, hivyo vinakazana kusafirisha bidhaa zake nje.

Mtaalamu huyo alisema bidhaa zilizozalishwa na baadhi ya sekta kuzidi mahitaji ya nchini ni sababu nyingine iliyochangia ongezeko kubwa la bidhaa zilizosafirishwa nchi za nje. Katika miezi 8 ya mwanzo ya mwaka jana, uagizaji wa vifaa vya chuma cha pua kutoka nje ulikuwa mkubwa zaidi kuliko vifaa hivyo vilivyosafirishwa nchi za nje kwa dola za kimarekani bilioni 7.7, lakini katika miezi 8 ya mwanzo ya mwaka huu, thamani ya usafirishaji wa chuma cha pua ilikuwa kubwa kwa dola bilioni 9.5 kuliko vile vilivyoagizwa kutoka nje, mbali na hayo baadhi ya bidhaa ambazo zingeagizwa kwa wingi kutoka nchi za nje, lakini sasa zinasafirishwa nchi za nje kwa wingi. Kwa mfano China ina upungufu wa madini ya shaba, na inaagiza kwa wingi kutoka nje kila mwaka, lakini kutokana na bei ya shaba nchini China kuwa chini kuliko bei ya soko la kimataifa, limetokea jambo la ajabu kuwa vifaa vingi vya shaba vinasafirishwa kwa nchi za nje.

Habari zinasema ili kuhimiza ulingano wa biashara na kuongeza nguvu ya ushindani ya viwanda, idara husika ya baraza la serikali inafanya utafiti na kutunga sera za kuhimiza sekta muhimu kuagiza zana kutoka nchi za nje.

Msemaji wa wizara ya biashara Bw. Chong Quan alisema, kutokana na tofauti ya vipindi vya maendeleo ya uchumi na mgawanyo wa kazi duniani, si ajabu kukosa uwiano katika biashara ya nje kwa nchi mbalimbali. Tangu kujiunga na WTO, biashara ya nje ya China inapanuka kwa mfululizo na ni yenye ulingano kwa jumla. Aliongeza kuwa hivi sasa China ina akiba kubwa ya fedha za kigeni, na haijali sana kuwa na pato kubwa katika biashara ya nje, bali inajitahidi kuwa na ulingano katika biashara ya nje. Hivi sasa serikali ya China inachukua hatua mwafaka kupanua uagizaji bidhaa kutoka nchi za nje, kwa upande mwingine inatarajia nchi husika kuondoa vikwazo kwa uagizaji wa China wa zana za teknolojia ya kisasa na kuanzisha mazingira kwa China kuongeza uagizaji wa bidhaa kutoka nchi za nje.

Idhaa ya Kiswahili 2006-11-14