Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-14 15:49:44    
Barua 1112

cri
Leo kwanza tunataka kumshukuru Bwana Mbarouk Msabah Mbarouk wa Duai, nchi za falme za kiarabu ambaye tarehe 5 alasiri alitupigia simu akisema amefurahia mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliokuwa ukifanyika mjini Beijing, alitaka kututumia barua pepe kutoa maoni yake, lakini baadaye hatukupata, labda ni kutokana na anuani yetu iliyobadilika, na yeye alitumia anuani ya zamani, hapa tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu kuwa, anuani yetu ya barua pepe ni swlbj@yahoo.com.cn.

Bwana Mbarouk pia alituuliza kuwa, mbona toleo jipya la jarida dogo la Daraja la urafiki mpaka sasa bado halijachapishwa. Kweli tungeomba radhi kwa wasikilizaji wetu wote, kutokana na kazi nyingi za kila siku, tuliahirisha uchapishaji wa jaridi hili mara kwa mara. Siku hizi tutajitahidi kuandaa vizuri ili kulichapisha.

Na msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff wa Bongoma Kenya alituletea barua pepe hivi karibuni akisema, salamu ziiwafikie huko Beijing China akitumai kuwa tuko wazima na tunaendelea katika pilikapilika kadha wa kadha. Kwanza anafahamu kuwa tulikuwa na shughuli za mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika pamoja na maandalizi ya sherehe ya miaka 65 ya Radio China kimataifa CRI pamoja na matayarisho ya michezo ya olympiki 2008. kwa kweli hizo zote ni kazi ngumu.

Alisema, zaidi ya hayo angependa kutoa maoni yake kuhusu mkutano ulikuwa unaoendelea mjini Beijing. Kwake binafsi amependezwa na maudhui au lengo la mkutano huo. Kwani mkutano huo una juhudi za kuongeza urafiki na maelewano kati ya China na Afrika. Hali kadhalika ni kuunda miundo misingi ya kuimarisha uchumi na ufanisi wa biashara.

Vile vile huu mkutano utazingatia juhudi na jukumu la kuimarisha maendeleo kati ya China na Bara la Afrika katika karne ya 21. Kando na hayo kwa nchi haswa Kenya tukizingatia kwa kilimo itakuwa na bahati ya kipekee ya kupata misaada kwa miradi ya maendeleo ambayo tayari China imeshaonyesha dalili za kuiunga mkono kwa kuwa na mipango ya kufanya maonyesho pamoja na kuimarisha kilimo, utoaji wa mitambo haswa ya utoaji wa mikopo kwa wakulima pamoja na kueneza makampuni mbalimbali katika nchi ya Kenya. Hiyo itaimarisha hali ya maarifa ambayo itaongeza utoaji wa mazao hata utayarishaji wa mazao, hali kadhalika kwa uhifadhi wa mazao.

Bwana Shariff anasema, kwa vile ambavyo anavifahamu, China ina uwezo wa kuzidisha kampuni zake na kuzihusisha katika kilimo na kwa mipango mingine kama vile kuwapa wakulima elimu, mikopo na njia mpya za kitekenolojia, hali kadhalika jambo bora ni kuondolea nchi za kiafrika kama vile Kenya madeni na hilo jambo likizingatiwa litakuwa la busara mno.

Mbali na hayo Afrika inahitaji mipango kama vile kupata huduma ya afya na elimu na kuimarisha uhusiano wa kitamaduni ambayo ilianzishwa miaka hamsini iliyopita na nchi za China na Afrika. Kwa kufanya hivyo nchi za Afrika zitaweza kupata angalao ufanisi kwa vile ikilinganishwa na nchi ya China iko karne nyingi sana nyuma ya China. Hata hivyo hii yote italeta amani kati ya nchi yete uimarishaji wa uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika.

Na sasa hivi ikiwa ni mara ya pili kwa rais Mwai Kibaki wa Kenya kuzuru nchi ya China. Watu wa Kenya wanayo matumaini makubwa kuwa yatakuwa ya manufaa kama anavyofahamu kuwa rafiki ya baba yako au mzazi wako ni rafiki yako pia kwa vile serikali ya Kenya na serikali ya China zimekuwa na urafiki mzuri, hana budi kusema kuwa wakenya sasa ni marafiki wa nchi ya China. Hii inaweza kuthibitishwa kutokana na mambo mbalimbali.

Tunamshukuru sana Bwana Mutanda Ayub Shariff kwa barua yake ya kueleza maoni yake kuhusu mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika.

Na msikilizaji wetu Adson JN Gamba wa Arusha Tanzania ametuandikia barua pepe isimayo: Hongera Rais Hu Jintao wa China na waziri mkuu Wen Jiabao kwa ziara yenu barani Afrika mwaka 2006.

Bwana Gamba alisema, anaunga mkono ziara waliyofanya rais Hu Jintao wa China na waziri mkuu wa China Wen Jiabao kwa kilomita 3500 ya nchi 10 za Afrika. Waliyoianza mapema April na June 2006. Lengo la ziara hiyo ikiwa ni kupanua wigo wa ufunguaji milango ya biashara yenye uwiano wa kunufaishana kati ya pande mbili na kujenga pamoja jamii ya kimataifa yenye mapatano kwa njia ya kidiplomasia hasa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni pia kuhimiza amani ya Dunia yenye unyumbufu na urafiki wa kidugu ili kuleta maendeleo endelevu ya pamoja na uchumi wa jamii duniani.

Bwana Gamba alisema, Ushindi wa wanajeshi na wananchi wa China dhidi ya wavamizi wa Japan, ushindi liliopata jeshi jekundu la chama cha kikomunisti cha China katika mapambano dhidi ya jeshi jeupe la chama cha Guomintang kilichoongozwa na Chang Keishek mwaka 1949, Ushindi huo wa China dhidi ya wavamizi ulikuwa ni ushindi wa Tanzania na bara zima la Afrika kujikomboa na kujitoa kutoka ndani ya minyororo ya mabepari. Ulikuwa ni ushindi ulioleta ustawi wa fikra mpya kwa China na Afrika na kuanza mahusiano ya kindugu ulioanzishwa na waasisi wa pande mbili. Wote wawili walioenga misingi imara kwa kusaidiana na kunufaishana hasa katika nyanja za elimu, uchumi na utamaduni.

Chama cha kikomunisti cha China kilifikia maamuzi ya kilele cha juu na kuanzisha ushirikiano na mahusiano ya vyama vya siasa na Afrika, Lengo la vyama hivyo vilikuwa kama nyezo na mchango wa mchakato ili kusukuma mbele maendeleo ya uwiano na uchumi wa pande mbili.

Tanzania bila kusahau mchango waliotoa wachina ambao ni ndugu zetu. Wachina 96 waliofika Tanzania walijitolea mihanga katika ujenzi wa reli ya TAZARA yenye KM 1860, makaburi yao leo hii ni alama na kielezo cha kudumu cha urafiki na udugu wa damu wa China kuchangia maendeleo ya bara la Afrika.

Pia China iliweka mkakati wa unyumbufu na msukumo imara katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ili lugha ya kiswahili itambuliwe na kuwa lugha ya saba kimataifa, na China ilisaidiwa na Tanzania na nchi nyingine za Afrika kuingia katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na kupata nafasi ya kiti cha uanachama wa kudumu.

Bwana Gamba alisema, anamsifu rais Hu Jintao wa China jwa juhudi zake za kuimarisha urafiki na mahusiano kati ya China na Russia uwe wa mafanikio na kusimama imara ili kukwamua (UN) Umoja wa Mataifa kutoka (UM) unyonyaji wa mataifa makubwa, na kushirikiana na nchi zinazoendelea ili kujenga uchumi wa uwiano na uhusiano wa kuheshimiana duniani.

Bwana Gamba alisema, pia anautakia kheri na amani mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, na mkutano wa 3 wa mawaziri wa baraza hilo, lengo likiwa kufungua ukurasa mpya wa kuhimiza urafiki, uchumi, amani na ushirikiano pia kuharakisha maendeleo ya kimkakati, kiujenzi na kuenzi miaka 50 ya urafiki kati ya China na Afrika.

Kwa kuwa sio rahisi kwake yeye binafsi kwapa Rais Hu Jintao, na waziri mkuu Wen Jiabao.pongezi hizi mkono kwa mkonom, anachukua hatua na azma ya kutumia kiwakilishi chetu cha pande mbili Radio China Kimataifa. Kutokana na umuhimu wa Chombo hiki hana shaka pongezi zake zitawafikia

Zidumu milele China na Afrika.

Tunamshukuru kwa dhati Bwana Adson JN Gamba kwa barua yake ya kupongeza ziara aliyofanya rais Hu Jintao wa China mwezi Aprili nchini Kenya na nchi nyingine za Afrika, na ziara aliyofanya waziri mkuu Wen Jiabao nchini Tanzania, Uganda na nyingine zipatazo zaidi ya 10 barani Afrika, pia tunamshukuru pongezi zake kwa mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika.

Idhaa ya Kiswahili 2006-11-14