Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-15 17:18:57    
Hospitali za kiserikali za kunufaisha umma mjini Beijing

cri

Gharama kubwa za matibabu zinazoongezeka siku hadi siku limekuwa ni suala linalowakabili watu wa China. Ripoti ya uchunguzi wa tatu wa taifa kuhusu hudumu za afya iliyotangazwa mwaka 2005 na wizara ya afya ya China imeonesha kuwa, zaidi ya nusu ya wananchi wa China wakipatwa na magonjwa, hawaendi kuonana na madaktari, na asilimia 30 ya wananchi wa China wanakataa kulazwa hospitalini kama inavyopaswa.

Serikali za ngazi mbalimbali za China zinafanya utafiti kwa ajili ya kutatua suala hilo. Mwaka 2005, serikali ya eneo la Haidian la mji wa Beijing ilijenga hospitali moja ya kunufaisha umma yaani hospitali ya Shangdi, ili kuboresha hali ya matibabu ya watu wenye pato la wastani na la chini wa huko. Katika mwaka mmoja uliopita, hospitali hiyo imekaribishwa na wakazi wa huko.

Bi. Ge Mingyan kutoka sehemu ya vijijini ya mji wa Chongqing alikuja mjini Beijing kufanya kazi za vibarua miaka mitano iliyopita, hivi karibuni aligunduliwa kuwa na saratani ya damu. Gharama za matibabu ya ugonjwa huo zilizokadiriwa na hosptali zilimtia wasiwasi mkubwa. Bi. Ge Mingyan alisema:

"nilimuliza daktari kuwa gharama za matibabu ni kiasi gani, alinijibu kuwa matibabu yatahitaji yuan elfu 8, niliposikia nilishtuka na nikagutushwa na machozi yalianza kunitoka mara moja."

Baada ya hapo, Bi. Ge Mingyan hakutaka kuenda tena hospitali, alikuwa anakaa nyumbani na kusoma vitabu kuhusu ugonjwa huo. Baada ya miaka miwili, hali ya ugonjwa wake ikawa mbaya zaidi. Hivyo alilazimika kwenda hospitali, lakini gharama za matibabu zikawa zimeongezeka zaidi. Alisema:

"daktari aliniambia niandae yuan elfu 30 na kusema ni lazima nilazwe hospitalini. Baada ya kusikia hivyo nilisema kuwa tuache na turudi nyumbani basi, gharama kubwa namna hii nitalipa vipi?"

Kutokana na hali hiyo, hali ya ugonjwa wa Bi. Ge Mingyan ilizidi kuwa mbaya. Ni kwa njia ya oparesheni ya kuhamisha uboho wa uti wa mgongo tu ndipo maisha yake yangeweza kunusurika. Lakini gharama za matibabu ya oparesheni hiyo ziliongezeka kwa kiasi kikubwa na kufikia yuan laki nne hadi tano.

Kama ilivyo kwa Bi. Ge Mingyan, watu wengi hawaendi hospitali wakati ugonjwa wao ukiwa katika hatua ya mwanzo, mpaka hali inapozidi kuwa mbaya, na hatimaye wanalazimika kutibiwa kwa gharama kubwa. Ni kwa vipi tunaweza kuepusha mambo kama hayo yasiendelee kutokea? Bw. Yu Xiaoqian akiwa ni mmoja wa waanzilishi wa hospitali ya Shangdi alisema, hospitali ya kiserikali ya kunufaisha umma inalenga kutoa huduma za kimsingi za afya kwa wakazi na kuwawezesha watu wenye matatizo ya kiuchumi wapate matibabu kwenye hospitali. Bw. Yu Xiaoqian alisema,

"hospitali hizo zinahakikisha kuwa kama watu hao wakipatwa na magonjwa, wanaweza kupata matibabu."

Kutokana na lengo hilo, mwaka 2005 mkurugenzi wa wakati huo wa idara ya afya wa wilaya ya Haidian Bw. Yu Xiaoqian na wengine alianzisha ujenzi wa hospitali ya kwanza ya kunufaisha umma yaani hospitali ya Shangdi. Hospitali hiyo iko kwenye eneo la Haidian lenye raslimali nyingi za matibabu. Hospitali nyingi kwenye eneo hilo zinakaribia kiwango cha kimataifa, lakini kutokana na gharama kubwa za matibabu ni vigumu kwa wakulima zaidi ya laki moja na wakazi zaidi ya elfu kumi wenye matatizo ya kiuchumi wa huko kulipia matibabu.

Mtizamo wa uendeshaji wa hospitali hiyo ni tofauti na hospitali za kiserikali za kawaida. Kwa kawaida, uwekezaji wa kiserikali kwa hospitali za kiserikali ni mdogo, asilimia 90 ya matumizi lazima ipatikane kutoka kwa wagonjwa, hivyo uendeshaji wa hospitali pia unapaswa kufuata kanuni ya soko. Lakini hospitali ya Shangdi inajaribu kufuata njia tofauti. Katika hospitali hiyo mpya, si kama tu mishahara ya madaktari inalipwa moja kwa moja na serikali, bali pia gharama mbalimbali za uendeshaji wa hospitali hiyo zote zinalipwa na serikali.

Kutokana na ruzuku za kiserikali, gharama za matibabu katika hospitali hiyo ni nafuu zaidi kuliko hospitali nyingine. Katika miezi minne tangu kufunguliwa kwa hospitali hiyo, idadi ya vitanda imekuwa havitoshi, kwa kuwa wagonjwa wengi zaidi walikwenda kwenye hospitali hiyo, na wengi wao walihama kutoka kwenye hospitali nyingine maarufu.

Serikali ya wilaya ya Haidian mjini Beijing imeamua kuwa, kama hospitali hiyo inaendelea vizuri, eneo la Haidian litafuata utaratibu mpya na kujenga hospitali mbili nyingine za kunufaisha umma. Hatua hiyo inakubaliwa na kuungwa mkono na wizara ya afya ya China. Sehemu mbalimbali za China zimeanza kujenga hospitali kama hizo.

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa wanaokwenda kwenye hospitali ya Shangdi, baadhi ya watu wana wasiwasi kuwa hospitali hizo hazipati faida kutoka kwa wagonjwa, zitaendelea vipi na kwa muda gani. Kuhusu wasiwasi huo, mkuu wa hospitali hiyo Bi. Wang Ling alisema, kwa kuwa gharama za uendeshaji wa hospitali hiyo zinalipwa na serikali, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa, mizigo ya hospitali hiyo inapungua.

"hospitali hiyo inaweza kumudu matumizi mbalimbali wakati idadi ya wagonjwa wanaokuja hospitali hiyo ikifikia 1000 hadi 1500 kila siku."

Imefahamika kuwa, hivi sasa hospitali ya Shangdi bado ni ya ngazi ya pili, haina uwezo wa kutibu magonjwa makubwa, lakini katika siku za baadaye, kutakuwa na hospitali za kunufaisha umma za ngazi ya tatu, na serikali itawekeza zaidi katika huduma za afya kwa watu wenye matatizo ya kiuchumi.