Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-20 15:07:31    
Msanii wa ngonjera ya kuchekesha, Ma Ji

cri

Ikilinganishwa na lugha zinanzoandikwa kwa herufi za Kilatini, lugha ya Kichina ina mvuo wake pekee ambayo licha ya kuwa na usanii wa maandiko wa mitindo ya aina nyingi pia ina usanii wa kuongea, na ngonjera ya kuchekesha ni usanii mmoja pia. Bw. Ma Ji ni msanii anayefahamika kwa Wachina wengi katika usanii huo.

Mliyosikia ni sehemu ya ngonjera ya kuchekesha iitwayo "Urafiki" iliyozungumwa na Ma Ji na Tang Jiezhong katika miaka ya 70, maudhui yake ni kuusifu urafiki kati ya China na Tanzania uliopatikana katika miaka ya ujenzi wa reli ya Tazara. Usanii wa ngonjera ya kuchekesha ilianzia mbali nchini China, lakini haikuwa usanii halisi hadi ilipofikia mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20. Mambo yanayozungumzwa katika michezo ya ngonjera yanatokana na maisha ya kila siku na yanachekesha kwa kusifu au kudhihaki hali nzuri au mbaya kwenye jamii.

Mchezo wa ngonjera ya "Urafiki" hadi sasa umekuwa na miaka 30, Bw. Ma Ji alipotaja ngonjera hiyo alisema,

"Ngonjera ya 'Urafiki' ilitungwa na mhandisi mmoja aliyeshiriki katika ujenzi wa reli ya Tazara. Baada ya ngonjera hiyo kuoneshwa, mara ilijulikana na watu wengi walifahamu maneno kadhaa ya Kiswahili yaliyotumika katika ngonjera hiyo, hata baadhi ya Waafrika nchini China walipenda kusema maneno hayo wakionesha kufurahia ngonjera hiyo."

"Urafiki" ni moja tu ya ngonjera mia kadhaa za kuchekesha zilizotungwa na Ma Ji.

Bw. Ma Ji alizaliwa mwaka 1934 katika familia maskini. Kutokana na maisha magumu Ma Ji alipokuwa na umri wa miaka 14, alikuwa anafanya kazi katika kiwanda kimoja cha nguo mjini Shanghai. Baada ya China mpya kuasisiwa Ma Ji alikuwa mfanyakazi katika duka moja la vitabu mjini Beijing. Kutokana na tabia yake ya uchangamfu na kuvutiwa na maisha ya wenyeji wa Beijing Ma Ji alionekana mwenye kipaji cha usanii wa ngonjera ya kuchekesha. Kwa mfano, aliweza kuiga jinsi walivyoimba wakati wachuuzi wadogo walipotembeza biashara yao na kuiga lafdhi ya lahaja za sehemu mbalimbali za China.

Mwaka 1956 ulikuwa ni mwaka wenye mabadiliko kwenye maisha yake. Ma Ji alipata nafasi ya kuonesha uhodari wake katika mashindano ya michezo ya sanaa ya wenyeji, na alichaguliwa kuwa mchezaji wa kulipwa katika Kundi la Michezo ya Sanaa ya Kuongea na Kuimba katika Redio ya China, na alianza kufundishwa na kusaidiwa na msanii mkubwa wa ngonjera ya kuchekesha Bw. Hou Baolin. Alipokuwa na umri wa miaka 20 alikuwa anajulikana sana katika nyaja ya ngonjera ya kuchekesha.

Katika miaka 50 iliyopita Ma Ji alionesha na kutunga michezo ya ngonjera zaidi ya 300, na alionesha michezo yake karibu kila pembe ya China, hata watu wenye asili ya China katika Asia ya kusini mashariki wanamfahamu na kupenda sana kusikiliza ngonjera zake. Kutokana na kupenda utamaduni wa China baadhi ya wanafunzi wa nchi za nje nchini China wamekuwa mashabiki wa ngonjera ya kuchekesha, walimwomba awe mwalimu wao. Ma Ji aliwapatia fursa nyingi kwa kuonesha michezo pamoja nao. Alisema,

"Mwaka jana niliandika mchezo mmoja wa ngonjera unaoitwa 'kutafuta mavazi ya chapa maarufu' ukieleza kuwa kutokana na maisha bora Wachina wanazingatia zaidi kuvaa mavazi yenye chapa maarufu. Nilichagua wageni wawili wazungungumze kwenye mchezo huo, mmoja ni Mwafrika mwingine ni Mfaransa, sisi watatu tuliigiza kwenye mchezo huo katika kituo cha redio."

Bw. Ma Ji alisema ameshughulika na ngonjera ya kuchekesha kwa zaidi ya nusu ya maisha yake, anapenda sana mchezo wa sanaa hiyo wa jadi wa Kichina. Lakini kutokana athari ya utamaduni wa nchi za nje, mchezo huo wa sanaa ulififia katika miaka ya 90. Kuanzia miaka miwili iliyopita mchezo wa sanaa hiyo umeanza kufufuka kutokana na kutunzwa na serikali, watu wameanza kuupenda mchezo huo wa sanaa. Mjini Beijing, mchezaji Guo Degang na wachezaji wengine vijana wa ngonjera wameibuka, muda si mrefu uliopita, mashindano ya ngonjera ya kuchekesha yaliyofanyika na kutangazwa katika kituo kikuu cha televisheni cha China yalivutia watazamaji wengi wa sahemu mbalimbali za China. Bw. Ma Ji alisema, atatumia uzoefu wake wa miaka mingi kuwasaidia wachezaji vijana. Alisema,

"Nimekuwa mzee wa miaka 72, nitaondoka jukwaani, kwa kuwa nimeshughulika na mchezo huo kwa maisha yangu yote, nitawasaidia wachezaji vijana kwa uzoefu wangu, na nitaendelea kuandika michezo mingi."

Bw. Ma Ji akiwa msanii mashuhuri, aliwahi kuonesha michezo yake ya usanii katika nchi nyingi na mara nyingi alishiriki katika maingiliano ya kiutamaduni kati ya China na nchi za nje. Mwaka jana alikwenda Afrika na kuonesha michezo kwa kushirikiana na wasanii wenyeji. Mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mjini Bejing unamfurahisha sana. Alisema,

"Huko barani Afrika nilishuhudia ngoma zilizogusa hisia zangu na niliona wanyama pori wengi wanaoishi pamoja na binadamu. Tunaweza kuandika mambo mengi katika michezo ya ngonjera kuhusu utamaduni wa Afrika na namna ya kuhifadhi wanyama na mazingira. Naona tukiona mengi tutaweza kuandika mengi kwa ajili ya kuwahudumia Wachina na Waafrika."

Idhaa ya kiswahili 2006-11-20