Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-20 16:52:51    
Kijiji cha kale cha Liukeng mkoani Jiangxi, China

cri

Kijiji cha kale cha Liukeng kinasifiwa na wataalamu wa China kuwa ni Kijiji cha kale cha kwanza cha China, ambacho kiko katika Wilaya ya Lean, mjini Wuzhou mkoani Jiangxi. Kijiji hicho kilianzishwa katika karne ya 10, na sasa kimekuwa na historia ya zaidi ya miaka 1000. Eneo la kijiji hicho ni kilomita 4 hivi, ambapo kuna majengo zaidi ya 500 yaliyojengwa katika enzi mbalimbali.

Wakazi wa kijiji hicho wanasema, katika kijiji hicho kuna njia 7 zinazoelekea mashariki hadi magharibi, na njia moja inayoelekea kusini hadi kaskazini, ambayo inakutana na njia zile 7 kwenye sehemu ya ncha ya magharibi, ambapo zinapitana, na katikati kuna vichochoro vingi vidogo vidogo. Na katika sehemu ya mwanzo na mwisho wa njia hizo zilijengwa ngome za uangalizi.

Kwenye sehemu ya magharibi ya kijiji hicho kuna Jengo moja la wasomi waliofaulu mtihani wa kifalme wa kuchagua maofisa katika zama za kale, jengo hilo lilijengwa wakati wa Enzi ya Song ya kusini miaka 800 iliyopita, kuta za mbao na meza za kuwekea sadaka za jengo hilo zinaonekana na hali ya umakini ya zama za kale. Hivi sasa ndani ya jengo hilo wanakaa raia wa kawaida. Jina la ukoo la wakazi wengi wa kijiji cha kale cha Liukeng ni Dong, mwanakijiji Dong Yongsheng amekaa katika jengo hilo kwa zaidi ya miaka 40. Alipokuwa na umri wa miaka 13, alijifunza kutengeneza vitu vya sanaa, kama vile kofia za wasomi waliofaulu mtihani wa kifalme katika zama za kale.

Kusuka kofia moja kunahitaji wiki moja, lakini kila kofia inaweza kuuzwa kwa Yuan 200, watalii wakitembelea kijiji hicho wanapenda kuvaa kofia kama hiyo kwa kupiga picha. Bwana Dong Yongsheng alisema:.

Nilisuka kofia ya aina hiyo kwa ajili ya watalii waweze kupiga picha, ili wapate kumbukumbu kuhusu Kijiji cha Liukeng, kwani ni kijiji chetu tu kina kofia kama hiyo inayoweza kuwapatia watalii kumbukumbu. Mwanzoni nilisuka kofia nyingi za aina hiyo, watalii wengi kutoka Taiwan na Hong Kong walinunua kofia hizo, walisema kofia hizo ni kama maandishi ya kale yanayohusu mambo ya zama za kale.

Njia zote kijijini humo zilitandikwa kwa mawe yenye umbo la mviringo, kando mbili za njia hizo ni majengo makubwa ya kale. Majengo hayo yote yana kuta ndefu zenye mapambo ya vichwa vya farasi. Katika kijiji hicho kuna vituo vingi vya masomo, huu ni umaalum mwingine wa kijiji hicho. Vituo hivyo vya masomo vimetapakaa katika kijiji hicho, hata katika kipindi fulani vituo hivyo viliwahi kufikia 37, ambavyo vimeonesha kuwa wakazi wa zama za kale wa kijiji hicho walitilia maanani sana utamaduni na elimu. Miongoni mwa vituo hivyo vya masomo, Wuguifang ni maarufu zaidi, kituo hicho cha masomo kilijengwa kwa ajili ya kuwakumbuka wasomi watano wa ukoo wa Dong waliofaulu kwa pamoja mtihani wa kifalme wa kuchagua maofisa katika zama za kale. Mkazi wa kijiji hicho Bwana Dong Shanzhi alisema:

Wakati wa utawala wa mfalme Song Renzong mwaka 1034, katika kijiji chetu, Dong Zhu, Dong Shidao, Dong Shide, Dong Ting na Dong Yi walikuwa ni watu wa ukoo mmoja, uhusiano kati ya watu hao watano ni baba mzazi na mtoto wake, ndugu, baba mdogo na mtoto wa kaka, watu hao watano walifaulu mtihani wa kifalme kwa wakati mmoja, katika ukoo mmoja watu watano kufanikiwa kwa pamoja katika mtihani wa kifalme wa kuchagua maofisa, lilikuwa ni jambo lenye thamani lililowashangaza sana watu wa nchi nzima.

Katika Kijiji cha kale cha Liukeng, pia kuna msikiti mmoja mkubwa wa ukoo wa Dong uliosifiwa kuwa kama ni bustani ya kifalme ya Yuanmingyuan ya Beijing. Eneo la msikiti huo ni mita za mraba 7,000, ambao umekuwa na historia zaidi ya miaka 360, lakini msikiti huo uliteketezwa mwaka 1927, mpaka sasa zimebaki nguzo kubwa tano za mawe, jozi moja ya simba wa mawe wenye sura ya heshima.

Hivi sasa kama watu wakitaka kuelewa zaidi kuhusu msikiti mkubwa wa ukoo wa Dong, wanaweza tu kusoma kumbukumbu za kale zilizohifadhiwa. Kumbukumbu hizo kuhusu ukoo wa Dong zilielezwa vilivyo kwenye ramani ya Kijiji cha Liukeng, mpangilio wa kijiji hicho, majina ya wakazi waliokuwa maofisa na matajiri wa kijiji hicho, majina ya watu mashuhuri waliokufa pamoja na maandiko ya kichina ya watu mashuhuri, kumbukumbu hizo zinastahiki kusifiwa kuwa ni kitabu cha ensaiklopidia kuhusu mambo yote ya Kijiji cha Liukeng. Utungaji wa kumbukumbu hizo ni mzuri sana ambazo zimehifadhiwa kikamilifu. Wakazi wote wa kijiji hicho wanaheshimu sana kumbukumbu hizo. Mkazi wa Kijiji cha Liukeng Bwana Dong Zhiming alisema:

Kumbukumbu hizo zimeandikwa kila kitu katika historia ya Ukoo wa Dong, kutokana na kumbukumbu hizo tunaweza kuona kuwa mababu zetu walikuwa wa enzi gani, walipata mafanikio gani au walifanya mambo gani mapya, na ni yapi yanastahili kusifiwa na watu wa vizazi vya baadaye. Kuhifadhi kumbukumbu hizo kunatokana na juhudi zilizofanywa na wazee wengi, na kuwepo kwa kumbukumbu hizo kunasaidia kuunganisha nguvu za ukoo huo.

Katika Kijiji cha Liukeng, hata mto, njia, vichochoro na majengo yote yanaonekana kuwa na hali ya zama za kale, na maisha ya wakazi wa Kijiji cha Liukeng pia yanaonekana kuwa na harufu nzito ya zama za kale. Katika kijiji hicho watu wanaweza kukutana mara kwa mara na akina Bibi wazee kadhaa ambao wakizunguka na kuchezea sarafu za shaba, watu wanne wanachezea sarafu 60 za shaba, huu ni mchezo unaofanyika katika ukoo wa Dong tangu kuanzishwa kwa Kijiji cha Liukeng.

Wakazi wa Kijiji cha Liukeng wanapenda kuonesha upendo wao kwa mtindo wa zama za kale hata katika chakula na vitu vya matumizi yao. Katika kijiji hicho vitu vingi vya matumizi ya kawaida vinatengenezwa na wanakijiji wenyewe. Bi Kizee mmoja mwenye umri karibu miaka 70 ni hodari wa kutengeneza chakula cha Toufugan kwa maharage, chakula hicho kinafurahiwa sana na wakazi wa huko. Na mishumaa iliyotengenezwa na mkazi wa huko Xie Shaoying, pia inapendwa sana na kutumiwa na wakazi wa huko kila wakati wa sikukuu, siku za kuzaliwa na siku za harusi. Na hali kadhalika chakula cha samaki chumvi kilichotengenezwa na wakazi wa kijiji hicho ambacho hata kinajulikana sana katika sehemu ya kijiji hicho, inasemekana kuwa chakula hicho cha samaki chumvi kilijulikana hata kwenye kasri la kifalme.

Idhaa ya kiswahili 2006-11-20