Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-21 15:39:49    
Mazungumzo kati ya Hamas na Fatah kuhusu kuunda serikali ya muungano yakwama tena

cri

Katika kipindi cha karibuni makundi mawili makubwa ya kisiasa ya Palestina, Hamas na Fatah yalikuwa yakifanya mazungumzo kuhusu kuunda serikali ya muungano inayoweza kukubaliwa na jumunyia ya kimataia, lakini tarehe 20 mazungumzo hayo yalikwama tena.

"Nawaambieni kwamba mazungumzo kuhusu kuunda serikali ya muungano yamepata maendeleo makubwa, kwa makadirio yangu pengine mwishoni mwa mwezi huu tutauona mwangaza wa serikali mpya."

Hii ni kauli iliyotolewa na mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina Bw. Mahmoud Abbas siku kumi zilizopita kwenye mkutano wa maadhimisho ya miaka miwili tokea kiongozi wa Palestina Bw. Arafat afariki. Kauli yake iliwafurahisha sana watu wa Palestina. Tokea Hamas ilipoanza kushika madaraka, jumuyia ya kimataifa imesimamisha misaada ya kiuchumi kutokana na serikali yake kukataa kuitambua Israel na kutoacha vitendo vya kijeshi. Hali hiyo ilifanya Palestina ambayo uchumi wake ulikuwa mbaya iwe karibu kufilisika. Watu wa Palestina wanatumai kuwa serikali mpya itaundwa mapema na itakubaliwa na jumuyia ya kimataifa ili Palestina iondolewe vikwazo vya kiuchumi.

Msaidizi wa Bw. Abbas, Bw. Nabil Amr tarehe 20 aliwaambia waandishi wa habari kuwa Fatah na Hamas zinagongana kuhusu nyadhifa za waziri mambo ya ndani na waziri wa fedha, na mazungumzo yamekwama. Bw. Nabil Amri alisema, mafanikio pekee katika mazungumzo hayo ni kuwa na maoni ya pamoja kuhusu wadhifa wa waziri mkuu, lakini hii ni "hatua ya mwanzo tu katika safari ndefu".

Lakini ofisa mmoja wa Hamas alisema, hivi sasa mazungumzo yamekwama tu na hayajasimama kabisa. Kiongozi wa Hamas na waziri mkuu wa serikali ya sasa pia walikataa kusema kuwa mazungumzo yamesimama.

"Mazungumzo bado yanaendelea, mwenyekiti na mimi sote tunahudhuria mazungumzo hayo. Mazungumzo yataendelea."

Vyombo vya habari vinasema, hii si mara ya kwanza kwa kukwama kutokana na mgongano kati ya Hamas na Fatah, Profesa Issa ibu-Zuhairah alisema

"Hamas ina mahusiano ya karibu na nchi za Iran na Syria na Fatah ina mahusiano karibu na nchi za Arabia, Marekani na Ulaya, kwa hiyo mgongano kati ya Hamas na Fatah ni mgongano wa kisiasa wala sio mgongano kuhusu kuundwa kwa serikali mpya."

Wachambuzi wanaona wasiwasi kuhusu kuweza kuundwa kwa serikali ya muungano. Profesa wa Israel Efraim Inbar alisema,

"Sina hakika kwamba serikali ya muungano itafanikiwa kuundwa, kwa sababu mazungumzo yalifanyika kwa miezi kadhaa lakini hayakupata mafanikio yoyote, mgongano kati ya Fatah na Hamas ni mkubwa."

Bw. Issa ibu-Zuhairah alisema makundi ya Fatah na Hamas yana migongano huku yanakabiliwa na tatizo la pamoja, yaani wasiwasi kuhusu taifa la Palestina.

"Makundi hayo mawili lazima yalegeze masharti yao kwani watu wanasubiri yatatue matatizo mengi hasa ya uchumi, na sio nani atakuwa waziri mkuu."

Idhaa ya kiswahili 2006-11-21