Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-21 15:50:43    
Barua 1119

cri
 Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52484 Dubai Falme za Kiarabu hivi karibuni ametutumia barua pepe akisema, kwanza kabisa angependa kuchukua nafasi hii kutoa pongezi zake za dhati kwa kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofunguliwa rasmi mjini Beijing mnamo tarehe 4 Novemba mwaka huu wa 2006 na kuhudhuriwa na viongozi kutoka nchi zaidi ya 40 za Afrika.

Kwa kweli tukio hilo ni lenye umuhimu mkubwa kabisa kwa bara la Afrika kwa wakati huu, ambapo viongozi wa Afrika wanahitaji sana njia mpya za kuboresha miundo mbinu pamoja na kutumia raslimali katika kuboresha uchumi na maendeleo ya mamilioni ya waafrika, ambao bado wanaishi katika hali duni kabisa.

Anasema kwa maoni yake binafsi Jamhuri ya Watu wa China ni mfano mzuri kabisa kwa viongozi wetu wa kiafrika na mataifa mengine yanayoinukia juu ya kujifunza mengi kuhusu mapinduzi ya kiviwanda na kutumia raslimali walizonazo ili kuboresha uchumi na maendeleo ya nchi zao.

Pia anasema katika ulimwengu wa leo hakuna asiyefahamu ni jinsi gani Jamhuri ya Watu wa China inavyozidi kunawiri kiuchumi na kimaendeleo kila kukicha, chini ya viongozi shupavu waliojitolea kujifunga mkaja kuendeleza miundo mbinu ya nchi hiyo kwa kutekeleza sera za mageuzi pamoja na kutumia nguvu kubwa ya umma wa China katika kuifanya nchi hiyo kuwa moja kati ya mataifa makubwa kabisa yaliyoendelea kiviwanda katika ulimwengu wetu huu wa leo.

Bila shaka yoyote Jamhuri ya Watu wa china imejitolea kusambaza matunda yake ya maendeleo kwa mataifa mengine duniani yanayohitaji njia na mbinu mpya za kujikwamua kiuchumi, kama vile nchi za kiafrika, jambo ambalo anasema yeye binafsi limemfurahisha na kumtia moyo sana.

Mkutano huu wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika pia unaonesha jinsi gani mafungamano makubwa ya kisiasa na kihistoria yaliyopo kati ya pande mbili, pamoja na kuudhihirishia ulimwengu kwamba Jamhuri ya watu wa China kamwe haiwezi kulitupa mkono bara la Afrika lenye matatizo mengi na nchi hiyo ipo tayari kujitolea kulisaidia bara hilo bila kinyongo wala uchoyo.

Anakamilisha barua yake kwa kusema ni matumaini yake kuwa mkutano huu utafungua ukurasa mpya wa mashirikiano mazuri kati ya China na Afrika katika karne hii mpya ya 21, pamoja na kulisaidia bara la Afrika kujikwamua kiuchumi na kuwapatia mamilioni ya wakazi wake maendeleo ya kweli ya kisasa katika ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia chini ya maazimio yaliyopitishwa na viongozi wa China na Afrika.

Tunamshukuru sana Bwana Mbarouk Msabaha kwa barua yake ya kuelezea maoni yake kuhusu Mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, kila mara tunavutiwa na moyo dhati na upendo alio nao kwa wananchi wa China na Radio China kimataifa, ni wasikilizaji wetu wengi akiwemo Bwana Mbarouk wanaotuhimiza tuchape kazi zaidi ili kuwafurahisha.

Na msikilizaji wetu Epafara Stanley Deteba ametuletea barua pepe akisema, marafiki zangu wapendwa ninapenda kuwafahamisha kuwa kwa sasa niko Russia kwa ajili ya masomo ambapo ninatarajia kuchukua shahada ya kwanza ya uandishi wa habari katika Chuo kikuu cha Nizhny Novgorod, anasema anapenda kutoa salamu zake kwa watangazaji na wasikilizaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Tunamshukuru sana msikilizaji Epafara Stanley Deteba kwa barua pepe yake, kweli siku nyingi zilizopita hatukupata barua yake, kumbe anasoma nchini Russia. Hapa tunamtakia mafanikio katika masomo yake huko, ni matumaini yetu kuwa atatuletea barua kutuelezea hali ya masomo yake, na pia tunamtakia kila la heri katika masomo yake.

Na msikilizaji wetu Fikiri Joseph Chongela wa S.L.B Lamadi, Magu, Mwanza nchini Tanzania, anasema katika barua yake kuwa yeye ni kijana wa kiume kutoka nchini Tanzania. Aliwahi kusikiliza Radio China kimataifa siku moja tu kupitia masafa mafupi. Alifurahishwa sana na kipindi alichokikuta hewani siku hiyo, na tokea siku hiyo hajawahi kusikiliza tena kutokana na tatizo la mawimbi ya sauti. Ila kwa kupitia mawimbi ya nchini Kenya inasikika kwa nadra sana nchini Tanzania.

Anasema baada ya kusikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa aliifurahia sana kiwango cha matangazo, ubora na ubunifu wa vipindi ambavyo alivisikiliza kwa siku hiyo. Anasema toka siku hiyo aliamua kuandika barua hii ili aweze kutoa pongezi zake. Sasa hivi yeye ni mwanachama msikilizaji wa matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio china kimataifa kupitia mawimbi ya masafa mafupi sanasana wakati wa usiku kwa majira ya Tanzania, kwani wakati huo ndio inasikika vizuri.

Tunamshukuru msikilizaji Fikiri Joseph Chongela kwa barua yake, ni matumaini yetu kuwa atasikiliza vipinvi vyetu na kutoa maoni na mapendekezo yake.

Anaamini kabisa kuwa ataendelea kuisikiliza Radio China Kimataifa kwa hamu kubwa na kwa kiwango cha juu sana pale anapokuwa na radio yake karibu. Mwisho anawatakia wafanyakazi wote wa CRI kazi njema na yeye ataendelea daima kusikiliza matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio Chinakimataifa.

Bw Philip Mchuki, wa klabu ya wasikilizaji wa CRI ya kijiji cha Nyankware S.L.B 646 Kisii Nchini Kenya, ametuandikia barua kwanza anaanza kwa kutusalimu. Anasema lengo la barua yake ni kutoa pongezi kwa wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwa kazi nzuri za siku hadi siku, anasema kwa kweli idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa inazidi kupata umaarufu nchini Kenya. Anasema tangu tuanzishe kituo cha FM Nairobi wasikilizaji wengi wamezidi kuvutiwa na matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Wengi wa wasikilizaji wanapenda kufungulia radio zao kwa masafa ya FM na kuburudika na vipindi vya Radio China kimataifa.

Mwezi Agosti mwaka huu alipata likizo na alitembelea jijini Nairobi ili kupata uhakika kuhusu hali ya usikivu wa kituo cha FM cha Radio China kimataifa. Alitumia muda mwingi kutembelea mitaa ya Nairobi na kwa kweli jambo aliloliona ni kwamba wakazi wengi wa Nairobi wanapenda kusikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa. Tatizo ambalo wengi wanalipata wakati wa kusikiliza kipindi cha jifunze Kichina ni kutokuwa na kitabu cha kichina ambacho watakuwa wanakitumia kufanyia mazoezi.

Anasema kuwa wasikilizaji pia wanafurahishwa sana na watangazaji wetu wa kituo cha Nairobi, ambao mara kwa mara wanawatembelea kuchukua maoni yao na kuyashughulikia kikamilifu. Anasema yeye aliporejea Kisii amewahamasisha wanachama wa kijiji cha Nyankware kusikiliza matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya radio zao na kuitegea sikio Radio China kimataifa kwani ni idhaa ambayo huwatangazia wasikilizaji habari kikamilifu, na ina vipindi vya kuburudisha na kuelemisha.

Anasema, katika sehemu anayosoma kuna wanafunzi wafuatao wanapenda kuwa wanachama wa Radio China Kimataifa na wanaomba watumiwe bahasha na majarida ya Radio China Kimataifa, nao ni Nicolas Orony, Betty Okioma,Jacklyne Nalianya, Dorris Taffy Gesami, David Menge, Jared Otiso, Nancy Orina, George Orwenyo, Nivian Omwenga.

Hapa tunawakaribisha kuwa wanachama wa Radio China kimataifa, ni matumaini yetu kuwa watasikiliza matangazo yetu ya idhaa ya kiswahili na kutoa maoni na mapendekezo yao ili kutusaidia kuboresha vipindi. Na tunamshukuru Bwana Philip Mchuki kwa barua yake ya kutuelezea usikivu wa FM Nairobi Kenya ambao umetutia moyo sana, na mapendekezo yake tutazingatia kwa makini.

Bw Pascal Mjomba, Shule ya Upili Mwandango, S.L.B 161-80305, Mwayaye nchini Kenya, ametuletea barua akisema, kwanza anatoa shukrani za dhati kwa watangazaji wote wa idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa. Anasema ana furaha isiyo kifani kwani amepokea barua tuliyomwandikia, ingawa aliipokea ikiwa imechelewa, anashukuru sana kwa vyote vilivyokuwa ndani ya barua hiyo vikiwa ni pamoja na kadi za salamu, bahasha iliyokwishalipiwa gharama za stempu na picha nzuri inayofurahisha. Picha hiyo ameiweka katika kivaranda cha nyumba yao na mgeni yoyote akiingia tu mlangoni, basi macho yake yataifurahia picha hiyo.

Msikilizaji huyu anasema yeye ni kijana kwa sasa na yupo katika kidato cha nne. Wakati akiwa shule huwa anasikiliza matangazo ya Radio China Kimataifa mara mbili kwa wiki, siku hizo ni ijumaa na jumamosi, lakini wakati wa likizo husikiliza kwa wiki nzima akishirikiana na nyanya yake pamoja na ndugu zake.

Kwa hakika kabisa anaomba kukaribishwa kuwa msikilizaji. Zaidi ya hayo yeye hupendelea sana vipindi vya Safari nchini China, pamoja na klabu ya utamaduni, halikadhilika burudani za muziki, maana vinanda vya kichina vilivyomo katika muziki huo vinamfurahisha sana.

Lakini pia anapendekeza kuwa ingekuwa ni vizuri kama idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa ingekuwa na matangazo au kipindi cha michezo kutoka nchi za Afrika, au matangazo ya ligi za Ulaya ili kuweza kupata wasikilizaji wengi. Pili, katika shindano la Chemsha Bongo liwe na washindi zaidi watakaopewa nafasi ya kuzuru China kushuhudia sherehe za kuadhimisha miaka 65 tangu kuanzishwa kwa Radio China Kimataifa, na pia kuwe na mpango wa kufungua vituo vya matangazo vya idhaa ya kiswahili ya Radio China Kimataifa kwenye sehemu nyingi zaidi. Anakamilisha barua yake kwa kusema anatumai kuwa atazidi kuwasiliana nasi na kutoa mapendekezo yake mbalimbali.

Tunamshukuru sana Pascal Mjomba kwa barua yake na mapendekezo yake, kweli mambo mengi tunataka kuyafanya, na tunajitahidi kuyafanya ili vipindi vyetu vinaweza kukidhi mahitaji ya wasikilizaji wetu.

Idhaa ya kiswahili 2006-11-21