Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-23 16:49:51    
Jinsi watu wa kabila la Wakyrghiz wanavyotilia maanani elimu

cri

Kabila la Wakyrghiz ni kabila lenye watu wachache kati ya makabila 55 madogomadogo ya China. Wakyrghiz wengi wanaishi katika wilaya inayojiendesha ya kabila la Wakyrghiz ya mkoa wa Xinjiang Uygur, kaskazini magharibi mwa China. Neno kryghiz katika lugha ya kabila hilo lina maana ya "wafugaji wa milimani". Kabla ya kuasisiwa kwa China mpya mwaka 1949, Wakryghiz walikuwa ni wafugaji wanaohamahama, na asilimia kati ya 80 na 90 ya watu wa kabila hilo walikuwa hawajui kusoma wala kuandika. Hivi sasa zaidi ya nusu karne imeshapita, hivi sasa kabila la Wakryghiz limepata maendeleo makubwa yanayolingana na makabila mengine hapa nchini China. Kutilia maanai elimu ni sababu muhimu ya maendeleo ya kabila hilo. Mwandishi wetu wa habari alitembelea familia moja ya Wakryghiz na kushuhudia jinsi watu wa kabila hilo wanavyotilia maanani elimu.

Familia hiyo ina watu 6: Bw. Abdul Kader, mkewe, mabinti watatu na mwana mmoja. Watoto hao wanne sasa wanasoma katika vyuo vikuu tofauti. Baba mzazi Bw. Abdul Kader alisema "Katika desturi kabila la Wakryghiz ni kabila la wachungaji waliohamahama. Awali kutokana na hali mbaya ya mazingira asili na uwezo mdogo wa kiuchumi, Wakryghiz wachache sana walipata nafasi kusoma shuleni. Babu yangu alikuwa hakupata elimu, lakini alikuwa akifanya kila awezalo kumsomesha baba yangu shuleni ili apate elimu. Wakati huo kulikuwa hakuna barabara hapa kwetu, baba yangu alikuwa akitembea kwa kilomita 80 hadi 90 kwenda kusoma katika shule ya sekondari ya Kashgar. Kwa hiyo tangu utotoni mwangu nilikuwa nafahamu kwamba, kupata elimu ni jambo muhimu sana kwetu."

Baba wa Bw. Abdul alifanya chini juu kumsomesha mwanae mpaka amalize masomo ya chuo cha ualimu, akawa mwalimu.

Mke wa Bw. Abdul, Bibi Kader pia alitoka familia iliyotilia maanai elimu. Wakati huo hata watoto wachache wa kiume walipata nafasi ya kusoma, wazazi wa Bibi Kader walishikilia kumsomesha binti yao shuleni, wakipuuza upinzani wa wengine na kubana matumizi ya familia, mpaka binti huyo ahitimu masomo na kufanya kazi ya ualimu katika shule ya chekechea.

Bw. Abdul Kader alieleza maoni yake kuwa, ama kwa kabila au kwa taifa, sekta ya elimu ni muhimu sana, bila kuendeleza shughuli za elimu sio rahisi kufanikiwa kuondokana na umaskini. Hivi sasa maisha ya watu wa kabila la Wakryghiz yanaboreshwa siku hadi siku, kwa hiyo anadhamiria watoto wake wote wapate elimu ya kiwango cha juu, ili wawe na ujuzi wa kuchangia maendeleo ya Wakryghiz.

Watoto wote wanne kusoma kwenye vyuo vikuu ni jambo la kujivunia, lakini pia linaleta gharama kubwa ambazo ni mzigo kwa Bw. Abdul na mkewe ambao wote ni walimu na hawalipwi vizuri sana. Kwa hiyo walianzisha mfuko wa elimu wa familia hiyo. Bw. Abdul alisema "Mwaka 1982 binti yangu wa kwanza alipozaliwa, nilikuwa na mshahara wa Yuan 58 kwa mwezi. Nilikubaliana na mke wangu kuwa, tunatoa Yuan 30 kila mwezi kuweka benkini zikiwa ni akiba ya elimu kwa watoto. Hata kama maisha yangekuwa magumu ya namna gani, ni lazima tuweke akiba ya fedha hizo kwa wakati kila mwezi. Hivi sasa nalipwa Yuan 2,400 kwa mwezi, kwa hiyo tunachangia Yuan 150 kwa mwezi kwenye mfuko huo wa elimu wa familia yetu."

Mama Kader alisema "Tulikumbwa na shida mbalimbali kwa wakati tunawasomesha watoto wanne shuleni, kiasi kwamba tuliwahi kuomba mikopo kwa benki. Hata hivyo tuna nia kuwa, kwa vyovyote vile ni lazima watoto wapate elimu. Kabila la Wakryghiz linazingatia kuwafundisha watoto wa kike kufanya kazi mbalimbali za nyumbani kama vile kutarizi, lakini sikuwafundisha wala sikuwaacha kazi nyingi za nyumbani. Wakirudi kutoka shuleni, waliendelea kusoma kwa makini, nilifurahia hali hiyo."

Hivi sasa binti yao wa kwanza Bi. Alima ameiga mfano wa wazazi wao na kuanzisha mfuko wa elimu wa familia kwa mwanae, yeye na mume wake wanaweka akiba ya Yuan 300 kwa mwezi kwa ajili ya elimu ya mtoto wao.

Watoto wanne wa Bw. na Bi. Kader si kama tu walifaulu mitihani ya kujiunga na vyuo vikuu, bali pia waliandikishwa na vitengo vinavyowavutia vijana wengi hodari. Bw. Kader alieleza kuwa taaluma zilizochaguliwa na watoto wake ziliamuliwa kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kabila la Wakryghiz na taifa nzima. Alisema "Binti yangu wa kwanza alijifunza lugha ya Kiingereza ili afahamu zaidi dunia hii. Binti wa pili sasa ni mwalimu, kwa sababu mimi na mke wangu ni walimu. Binti wa tatu alijifunza taaluma ya upashanaji habari kwani hivi sasa taifa linahitaji sana watu wanaoshughulikia utafiti wa sayansi na teknolojia. Na mwanangu alichagua taaluma ya udaktari ili ataweza kuwasaidia wengine wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali."

Bwana huyo aliongeza kuwa, "Binti yangu wa kwanza sasa anasoma shahada ya pili. Natumai watoto wengine pia wataweza kusoma shahada ya pili, na baadaye kuendelea na masomo ya shahada ya tatu, mimi na mama yao tutafanya kila tuwezalo kuwasaidia hadi watakapohitimu masomo. Pia natumai watoto wakihitimu watarudi kwetu wilaya inayojiendesha ya kabila la Wakryghiz, kwani kati ya wakazi laki 5.8 wa wilaya yetu, Wakryghiz ni watu laki 1.4, wakirudi watasaidia maendeleo ya shughuli za elimu za Wakryghiz."

Idhaa ya kiswahili 2006-11-23