Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-24 17:03:24    
Raia ni waathirika zaidi na vurugu nchini Iraq

cri

Tarehe 23 mashambulizi ya mabomu yalitokea katika mji wa Sadr mashariki ya Baghdad na kusababisha vifo vya watu 150 na wengine 238 kujeruhiwa. Mji wa Sadr ni sehemu wanayoishi waislamu wa madhehebu ya Shia, ambayo inadhibitiwa na "jeshi la Mehdi" linaloongozwa na kiongozi wa madhehebu ya Shia, Bw. Sadr. Mji huo unaoshambuliwa mara kwa mara na vikosi vya madhehebu ya Suni ni sehemu ambayo migongano mingi inatokea kati madhehebu ya kidini. Ni miaka mitatu sasa tangu vita vya Iraq vimalizike, lakini vurugu za kimabavu hazijapungua, raia wengi wa Iraq wamepoteza maisha na kuathiriwa vibaya na vurugu hizo.

Tarehe 22 Umoja wa Mataifa ulitoa ripori ikisema kuwa, katika mwezi wa kumi raia 3,709 wa Iraq walipoteza maisha katika vurugu za kimabavu, huu ni mwezi wenye watu wengi kabisa waliokufa tokea vita vya Iraq vizuke mwaka 2003. Ripoti hiyo pia imesema, tokea mwezi wa pili mwaka huu Wairaq laki 4.2 wamekimbia makazi yao.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, tishio kubwa kwa raia wa Iraq linatokana na migongano kati ya madhehebu ya kidini. Mlipuko uliotokea katika msikiti Ali al-Hadi mwezi wa pili mwaka huu ulisababisha mgongano mkali kati ya madhehebu ya Shia na Suni na kusababisha vifo vingi vya watu waliouawa ovyo kwa uhasama. Habari kutoka kwenye tovuti ya CNN ya Marekani zinasema, katika siku tatu tokea tarehe 20 hadi 22 Novemba polisi wa Iraq waligundua maiti 140 mjini Baghdad na pembezoni mwa mji huo, na miili mingi ilikuwa na majeraha ya kudhalilishwa kutokana na uhasama.

Wachambuzi wanaona kuwa licha ya migogoro kati ya madhehebu ya kidini, majeshi ya nchi za nje yanayoongozwa na Marekani pia ni tishio kwa usalama kwa raia wa Iraq. Polisi ya Iraq tarehe 23 ilitangaza kuwa askari wa Marekani walilifyatulia risasi basi dogo katika mji wa Sadr na kusababisha vifo vya watu wane, na wanane kujeruhiwa. Kadhalika vikosi vya Marekani nchini Iraq ni shabaha ya vikosi vinavyoipinga Marekani, na mashambulizi kwa vikosi hivyo husababisha vifo na majeruhi kwa raia wengi wasio na hatia.

Isitoshe tishio la usalama kwa raia wa Iraq pia linatokana na vikundi vya wahalifu. Serikali ya Iraq inashindwa kudhibiti usalama, wahalifu wanatumia fursa hiyo kufanya maovu. Tarehe 14 mwezi huu watu wenye silaha waliovaa sare za polisi waliwateka nyara maofisa zaidi ya 100 wa wizara ya elimu ya juu, tukio hilo lilistaajabisha dunia. Tokea serikali ya Saddam ipinduliwe mwaka 2003, matukio ya utekaji nyara yanaongezeka siku hadi siku. Kwa mujibu wa takwimu kutoka ubalozi wa Marekani nchini Iraq, hivi sasa kila siku matukio ya kuteka nyara yanatokea mara tano hadi 30, hali hiyo pengine imezidi hali ya nchi za Colimbia, Mexico na Brazil, nchi ambazo zina matukio mengi ya utekaji nyara, watekaji wana shughuli kamili toka kuwatafuta watu watakaotekwa hadi kuwateka, kuwasafirisha na kuwadhibiti na kufanya mazungumzo na jamaa wa mateka.

Wachambuzi wanaona kuwa hali mbaya ya usalama nchini Iraq imewafanya watu wa Iraq waishi kwa wasiwasi, serikali ya Iraq inapaswa kuchukua hatua halisi, kuvunja vikosi vya wanamgambo, kupambana ufisadi na vikundi vya wahalifu, kuimarisha usalama na kutatua tatizo la ugawaji wa maslahi ya mafuta ili kusuluhisha mgongano kati ya vikundi mbalimbali. Hali kadhalika Marekani inapaswa kurekebisha sera zake kuhusu Iraq na kuweka ratiba ya kuondoa jeshi lake kutoka nchini humo kama wanavyotaka watu wa Iraq, na nchi za jirani na nchi nyingine za Kiarabu pamoja na jumuyia ya kimataifa, ziisaidie nchi hiyo ili watu wa Iraq waliozama hatarini wapate usalama mapema iwezekanavyo.

Idhaa ya kiswahili 2006-11-24