Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-27 16:43:49    
Kipindi maalumu cha chemsha bongo-"Kutembelea pepo ya dunia"

cri

Makala 1

Mkoani Sichuan kuna vivutio vingi vya utalii, ambapo kuna Bonde la Jiuzhaigou yaani bonde la vijiji 9 vya kabila la watibet na sehemu yenye mandhari nzuri ya Huanglong, hizi ni sehemu mbili zenye vivutio vingi vya utalii, sehemu hizo mbili zina tofauti gani, na kwanini wachina wanazisifu kuwa ni pepo ya dunia?

Katika kipindi hiki maalum cha chemsha bongo kuhusu vivutio vya utalii vya "Mkoa wa Sichuan, Maskani ya Panda" leo tunawaletea makala ya kwanza kuhusu Vivutio vya Bonde la Jiuzhaigou, na Sehemu yenye mandhari nzuri ya Huanglong. Kabla ya kusoma makala hii, kwanza tunatoa maswali mawili. La kwanza, Bonde la Jiuzhaigou lilipewa jina hilo kutokana na eneo hilo kuna vijiji 9 vya kabila la watibet? Bonde la Jiuzhaigou na Sehemu yenye mandhari nzuri ya Huanglong zimeorodheshwa kuwa mali ya urithi wa maumbile duniani? Sikilizeni kwa makini makala tutakayowasomea, mtapata majibu kwa urahisi.

Bonde la Jiuzhaiguo liko kwenye tarafa inayojiendesha ya kabila la watibet na waqiang ya Abe magharibi ya Mkoa wa Sichuan, China. Bonde hilo ni bonde lenye umbo wa herufi Y, urefu wake ni zaidi ya kilomita 40.?Kwa kuwa kwenye bonde hilo kuna vijiji 9 vya kabila la watibet, ndiyo maana bonde hilo linaitwa Bonde la Jiuzhaiguo yaani bonde la vijiji 9.

Bwana Nerohem Yam kutoka Israel anapenda sana kutembelea sehemu mbalimbali nchini China, katika miaka kadhaa iliyopita alitembelea Beijing, Shanghai, mikoani Zhejiang na Shanxi, amepata ufahamu kuhusu mila na desturi za sehemu mbalimbali nchini China na vivutio vya utalii nchini China, lakini baada ya kufika Bonde la Jiuzhaiguo, alikuwa hawezi kujizuia kusifu sehemu hiyo yenye vivutio vya kumshangaza, alisema:

Hii ni sehemu nzuri kabisa nchini China, sijawahi kuona sehemu nyingine duniani inayopendeza namna hii, vivutio vyake ni tofauti kabisa na vile vya sehemu nyingine.

Maajabu ya Bonde la Jiuzhaiguo yanatokana na maji ya huko, maji ni roho ya bonde hilo, kwenye ukanda wa bonde la mto la Jiuzhaiguo, kuna maziwa makubwa na madogo zaidi ya 100 ambayo maji yake ni ya rangi mbalimbali, watibet wanaoishi huko wanayaita maziwa hayo kuwa ni "Haizhi", maana hiyo ya kichina ni watoto wa bahari.

Maji ya maziwa hayo ni safi sana, watalii wanaweza kuangalia kwa urahisi mawe, majani na matawi ya miti yaliyokauka yaliyoko chini ya maziwa; rangi za maji ya maziwa hayo zinabadilika kila mara, maji ya baadhi ya maziwa ni ya kibuluu, maji ya maziwa mengine ni ya kijani sana ikichanganyika na rangi ya kimanjano. Kwa mfano Ziwa kubwa kabisa ndani ya Bonde la Jiuzhaiguo liitwalo Changhai, ukiangalia karibu na ziwa unaweza kuona maji ya ziwa ni ya rangi ya kijani, ambayo ni safi sana, lakini ukiangalia kutoka mbali utaona kuwa maji ya ziwa hilo ni ya kibuluu, na vivuli vya milima ya kando mbili za ziwa vinaonekana wazi ndani ya ziwa, mandhari yake ni nzuri sana kama picha iliyochorwa na watu.

Bwana Morishita Sadamasa kutoka Japan alipotazama ziwa hilo alilisifu sana akisema:

Nilipokuwa Japan niliwahi kutazama video kuhusu mandhari ya Bonde la Jiuzhaiguo, lakini nikifika sehemu hiyo na kushuhudia hali halisi, naona mandhari ya huko ni nzuri zaidi kuliko ile iliyopigwa kwenye video. Nchini Japan pia kuna maziwa mengi, lakini maziwa ya Bonde la Jiuzhaiguo yanawavutia watu zaidi.

Maji ya maziwa kwenye bonde la Jiuzhaiguo ni ya rangi mbalimbali, ambayo ni maumbile ya asili, kwani Bonde la Jiuzhaiguo lina umaalum wa sura ya kijografia ya kikarst, ndani ya ziwa kuna madini ya chokaa, mangnesium na kadhalika, ambayo yanaweza kutoa mionzi ya rangi ya kibuluu na kijani, na ndani ya maziwa kuna majani zaidi ya aina 200 zenye rangi mbalimbali tofauti, hivyo rangi za maji zinabadilikabadilika.

Maji ya maziwa kwenye Bonde la Jiuzhaigou huwa ni shwari, lakini wakati maji hayo yanapoporomoka chini kutoka kwenye miamba mirefu palipositawi miti mingi yanabwaga chini kwa kasi sana, kuna maporomoko ya maji 17 kwenye Bonde la Jiuzhaiguo, hivyo watalii wanaweza kuona maporomoko hayo ni mapana ambayo yanafunika upande mzima wa miamba. Miongoni mwa maporomoko hayo, Maporomoko ya Norilang yanaonekana ni mapana kabisa nchini China, maji yanaporomoka kutoka miamba yenye upana wa zaidi ya mita mia moja mithili ya pazia la maji, na chini ya mwangaza wa jua maporomoko hayo yanaweza kuonekana kuwa ni upinde wa mvua, mandhari nzuri hiyo na inawavutia sana watu.

Hilo ndilo Bonde la Jiuzhaiguo ambalo linasifiwa na wachina kuwa ni sehemu ya peponi. Mwaka 1992 Bonde la Jiuzhaiguo liliorodheshwa na Shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO kuwa ni mali ya urithi wa maumbile duniani. Na wakazi wa huko ambao ni watu wa kabila la watibet wanaona kuwa milima, maji, misitu na mawe kila kitu cha Bonde la Jiuzhaiguo walizawadiwa na Mungu. Msichana wa kabila la watibet Inamanhong alisema, tangu alipokuwa mtoto alifundishwa na baba na mama yake kuwa anapaswa kutunza vizuri majani na miti, na kila kitu cha bonde hilo. Alisema:

Sisi wakazi watibet tunaamini kuwa kila kitu duniani kina roho yake, milima, maji na miti yote tulizawadiwa na Mungu, binadamu wanapaswa kuitunza, tusifanye uharibifu hata kidogo. Na wazee wetu mara kwa mara wanawaambia watoto wao kwamba wasiende kufua nguo kwenye ziwa na wasichafue mazingira.

Msichana mtibet Yinamanhong na wengine wa kabila lake mpaka sasa wanaishi kwenye Bonde la Jiuzhaigou, nao ni waumini wa dini ya kibuddha ya kitibet, wanaishi maisha kwa kufuata mila na desturi za kitibet, wanaonekana ni wachangamfu na wakarimu sana, watalii wakifika Bonde la Jiuzhaiguo, baada ya kutembelea huwa wanaweza kuingia nyumbani kwa wakazi watibet, kuonja chai yenye maziwa na vinywaji vya Qingke vilivyotengenezwa na watibet na kuburudishwa na nyimbo na ngoma zenye mtindo pekee wa kitibet, wanaona furaha kweli.

Baada ya kutembelea Bonde la Jiuzhaiguo, watalii wanaweza kupanda basi kwenda sehemu yenye mandhari nzuri ya Huanglong, kuendelea kutembea kwenye "pepo ya dunia". Sehemu ya Huanglong iko kwenye umbali wa kilomita 130 kutoka Bonde la Jiuzhaiguo. Sehemu ya Huanglong ni sawa na Bonde la Jiuzhaiguo lilivyo, iliorodheshwa na UNESCO kuwa mali ya urithi wa maumbile duniani mwaka 1992. Na maji ya mito ya sehemu hiyo pia ni vivutio pekee vya sehemu hiyo.

Watalii wakitembelea kwenye bonde la sehemu ya Huanglong wataona mwinuko wa rangi ya kimanjano wa chokaa wenye urefu wa kilomita 4 unaotambaa ndani ya misitu na milima yenye theluji kama dragon mwenye rangi ya dhahabu. Kwenye mwinuko huo kuna madimbwi makubwa na madogo zaidi ya 3000 yaliyoko kwenye bonde lenye ngazi mbalimbali, chini ya mwangaza wa jua, maziwa hayo yanameremeta na kupendeza sana. Na madimbwi yaliyoko kwenye ngazi ya juu yanaitwa ni "madimbwi ya rangi tano", madimbwi hayo yapatayo mia 7 hivi yaliyoko chini ya mwangaza wa jua yanaonekana ni ya rangi mbalimbali tofauti, uzuri wake unawashangaza sana watalii.

Lakini madimbwi ya rangi tano yako kwenye mwinuko wa zaidi ya mita 4000 kutoka usawa wa bahari, siyo kila mtu ana nguvu ya kuweza kutembea kwa miguu na kupanda juu. Ofisa wa Sehemu yenye mandhari nzuri ya Huanglong Bwana Kou Yahui alisema, wamepata njia ya kushinda taabu na kupanda juu ya mwinuko huo. Alisema:

Mwaka huu tutakamilisha ujenzi wa njia ya kebo ili watalii waweze kupanda mwinuko huo kuangalia madimbwi ya rangi tano. Aidha tumeweka vituo vitano vya kutoa hewa ya oxygen bila malipo kwenye njia ya milimani, na tutaongeza vituo vingine viwili ili watalii wanaotaka kupanda kwa miguu milima waweze kutumia hewa ya oxygen .

Wasikilizaji wapendwa, kabla ya kuhitimisha makala ya kwanza ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya "Mkoa wa Sichuan, Maskani ya Panda", tunarudia tena maswali. La kwanza, Bonde la Jiuzhaigou lilipewa jina hilo kutokana na eneo hilo kuna vijiji 9 vya kabila la watibet? Bonde la Jiuzhaigou na Sehemu yenye mandhari nzuri ya Huanglong zimeorodheshwa kuwa mali ya urithi wa maumbile duniani? Wiki ijayo wakati kama huu tutawaletea makala ya pili ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya "Mkoa wa Sichuan, Maskani ya Panda". Msikose kutusikiliza, kwa herini.

Idhaa ya kiswahili 2006-11-27