Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-27 19:18:00    
Bi. Zhu Mingying msanii anayechangia kuendeleza urafiki kati ya China na Afrika

cri

Mliosikia ni wimbo wa Afrika uitwao "Yiyaya Leo" alioimba mwimbaji mashuhuri wa China Bi. Zhu Mingying. Watazamaji wanavutiwa sana kutokana na jinsi anavyoimba na huku akicheza ngoma. Tokea mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita aliimba nyimbo nyingi za Asia, Afrika na Latin Amerika, watazamaji wanaona kwamba yeye ni msanii anayechangia kuendeleza urafiki kati ya China na Afrika.

Bi. Zhu Mingying alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Dansi cha Beijing mwaka 1966 na kuanza kufanya kazi katika Kundi la Nyimbo na Dansi la Mashariki la China mjini Beijing. Katika miaka kumi ya mwanzoni baada ya yeye kujiunga na kundi hilo, wachezaji wa kundi hilo walikuwa hawana nafasi nyingi za kuonesha michezo jukwaani kutoka na uendeshaji mbaya wa kundi hilo. Bi. Zhu Mingying alipata umaarufu alipokuwa tu katika maonesho ya kundi hilo mwaka 1979. Katika maonesho hayo Zhu Mingying akiwa amepaka rangi nyeusi kote mwilini na kuvaa mavazi ya Kiafrika wakati aliimba nyimbo za Afrika huku akisakata kiuno. Kwa sababu alikuwa amejifunza kucheza ngoma za Afrika kwa miaka mingi maonesho yake yalivutia na kushangiliwa sana na watazamaji. Licha ya maonesho yake licha kumpatia umaarufu yeye mwenyewe pia yalilipatia sifa kubwa kundi lake. Hivi karibuni waandishi wetu wa habari walizungumza naye, alisema,

"Ingawa umri wangu umekuwa mkubwa, lakini mimi ni mwepesi wa kujifunza nyimbo na ngoma za Afrika kutokana na msingi wangu imara wa sanaa. Niligundua kwamba watazamaji wanafurahia maonesho yangu kutokana na nyimbo nzuri za Kiafrika na ngoma zao, mtindo huo wa kuunganisha yote pamoja unawafurahisha watazamaji."

Bi. Zhu Mingying alisema, alipojiunga na kundi la nyimbo na ngoma la Mashariki nafasi za kuonesha michezo zilikuwa chache. Baadaye alihamasishwa na hayati waziri mkuu Zhou Enlai ambaye aliwashauri wajifunze lugha za kigeni, kwa sababu, alisema, wao licha ya kuwa wasanii pia ni lazima wawe wanadiplomasia katika mambo ya sanaa, wanaweza kuzidisha maingiliano ya kiutamaduni na urafiki kati ya China, Afrika na Latin Amerika. Bi. Zhu Mingying aligundua kwamba michezo ya sanaa ya Asia, Afrika na Latin Amerika ni kuimba na kucheza kwa pamoja, na katika kundi la nyimbo na dansi la Mashariki kulikuwa hakuna wachezaji wenye uwezo wa yote mawili, aliona anaweza kutumia uwezo wake huo kujaza nafasi hiyo. Kwa hiyo aliamua kujifunza lugha za kigeni. Katika wakati huo watu waliofahamu lugha za nchi za Afrika wengi walikuwa katika Redio China Kimataifa, alikuja kwenye kituo cha redio hii na kujifunza lugha ya Kiswahili.

Ufanisi wa maonesho ya nyimbo na ngoma kwa pamoja ulimtilia moyo kujifunza lugha za kigeni. Tokea hapo katika muda wa miaka mitano aliimba nyimbo zaidi ya mia moja kwa lugha zaidi ya ishirini. Siku moja kwenye maonesho mara aliimba na kucheza ngoma za Kihindi mara aliimba nyimbo na kucheza ngoza za Kiafrika kwa kupakwa rangi nyeusi mwili mzima. Alifanya maonesho karibu kote nchini China na mara nyingi alifanya maonesho katika nchi za Asia, Afrika na Latin Amerika.

Zhu Mingyingi alikaribishwa sana katika nchi za nje kutokana na kuimba kwa lugha za kienyeji. Alisema anakumbuka sana alipoimba wimbo uitwao "Baisbusa" nchini Misri. Alisema,

  

"Huko Misri nilipomaliza wimbo huo nilikuwa siwezi kushuka jukwaani kwani watazamaji walinirudisha jukwaani kwa kupiga makofi hata mara 32, nilipokuwa naimba sikuweza kusikia sauti yangu kwa sababu sauti ya watazamaji ilikuwa kubwa zaidi. Baada ya kushuka jukwaani nilizawadiwa kwa pesa nyingi na keki moja kubwa mfano wa meza."

Jinsi aivyovutiwa na watazamaji hao ilimfahamisha kwa kina zaidi umuhimu wa kazi yake. Kila wimbo alioimba unaonesha heshima kwa utamaduni wa Afrika. Hata hivyo alihisi kwamba ufahamu wake kuhusu utamaduni wa Afrika bado mdogo, anatumai atapata fursa nyingi zaidi za kujifunza muziki na ngoma za Afrika. Bi. Zhu Mingying alipopata habari kwamba huko Marekani kuna shule za muziki na ngoma za Afrika bila kusitasita alijiuzulu kazi ya kundi lake na kwenda Marekani.

Mwaka 1985 alijiunga na Chuo cha Muziki cha Berkley, alichagua kozi ya muziki na historia ya muziki wa Afrika. Mwanzoni alikuwa na matatizo ya lugha, baada ya darasa alitumia muda mwingi kuelewa aliyofundishwa. Alisema,

"Afrika ni chanzo cha sanaa duniani, sanaa zake ni tofauti kabisa na sehemu nyingine, ninatamai kuunganisha muziki wa Afrika na wa China, muziki kama huo hakika utakuwa na aina yake na utavutia sana, nasubiri siku hiyo."

Baada ya kuhitimu masomo yake nchini Marekani Zhu Mingying alirudi nchini China, alianzisha chuo cha sanaa za kimataifa na kuanza kufanya utafiti sanaa za Afrika. Alisema,

"Chuo changu kinafanya utafiti wa sanaa za Afrika, sanaa za kila nchi ya Afrika, nitakwenda barani Afrika kujifunza sanaa na kuonesha baadaye, nitawaonesha Wachina sifa zote za Afrika."

Akiwa msanii anayeshughulikia sanaa za Afrika Zhu Mingying mara kwa mara anakwenda barani Afrika, alisema hivi sasa kuna Wachina wengi barani humo, na pia kuna mikahawa mingi ya Kichina, hivi sasa uhusiano kati ya China na Afrika upo katika kipindi kizuri kabisa cha kihistoria. Kuhusu mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika Bi. Zhu Mingying alisema,

"Nilishiriki kwenye mikutano mingi ya baraza hilo, kwa kweli nilifundishwa sana. Nimegundua kwamba China inazingatia pande mbalimbali za Afrika katika mambo ya diplomasia, ushirikiano kwenye miradi, mambo ya siasa, nyanja za sanaa na elimu. Nina hakika kwamba urafiki na ushirikiano kati ya pande mbili utakuwa mkubwa zaidi."

Idhaa ya Kiswahili 2006-11-27