Kutokana na maendeleo ya haraka ya uchumi wa China, India na nchi nyingine za Asia, nchi kadhaa za Afrika kama vile Zimbabwe, Kenya na Namibia zinafanya juhudi kutetea kutekeleza sera ya "kuelekea mashariki", hasa zinatilia maanani kujifunza mfano wa China kuhusu maendeleo, ambapo zinatarajia kutimiza lengo la kujiendeleza baada ya kuiga maarifa ya China katika ujenzi wake wa uchumi.
Zimbabwe ni nchi ya kwanza ya Afrika iliyotoa na kuanza kutekeleza sera ya "kuelekea mashariki". Mwaka 2002, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alitetea kutupia macho nchi za Asia ambazo China ikiwa mwakilishi wao. Kutokana na kuelekezwa na sera hiyo, China imekuwa nchi inayowekeza vitega uchumi vingi zaidi nchini Zimbabwe, ambapo pande hizo mbili zinapanua siku hadi siku ushirikiano katika sekta mbalimbali.
Waziri wa mambo ya nje wa Kenya Raphael Tuju amedhihirisha wazi kuwa, China imekuwa nchi muhimu katika sera ya Kenya ya "kuelekea mashariki". Mwezi Aprili mwaka huu, kabla ya rais Hu Jintao wa China kufanya ziara nchini Kenya, Ikulu ya Kenya ilitoa taarifa ikisema kuwa, serikali ya Kenya inafuatilia kwa hamu kubwa nchi za mashariki ya dunia, hasa maendeleo ya China, kwani nchi hizo zinaweza kutoa fursa za kiuchumi katika sekta mbalimbali. Msemaji wa serikali ya Kenya Bwana Alfred Mutua alisema, serikali ya Kenya itafanya juhudi kubwa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na China.
Rais Hifikepunye Pohamba wa Namibia alipohojiwa na mwandishi wa habari wa Shirika la habari la China Xinhua alisema, nchi za Afrika si kama tu zinataka kujifunza kutoka kwa nchi zilizoendelea kama vile Japan, bali pia zinapaswa kujifunza kutoka kwa nchi zinazoendelea kama China na India. Katika kipindi cha hivi sasa, hasa zinapaswa kutupia macho kwa China, kwani maarifa ya China ni yenye umuhimu zaidi wa kuzingatiwa na kuigwa.
Sera hiyo ya nchi za Afrika imeonesha kuwa, njia ya maendeleo ya China inakaribishwa zaidi na nchi za Afrika. Viongozi wengi wa Afrika wanaona kuwa, kuendeleza urafiki wa jadi kati ya China na Afrika kumewekwa mkazo zaidi katika mambo ya kidiplomasia ya China. Ni tofauti na nchi kadhaa za magharibi, China haiingilii hata kidogo mambo ya ndani ya Afrika, wala haisemi hii au ile kuelekeza nchi yoyote ya Afrika, bali inazielewa na kuheshimu vilivyo nchi za Afrika.
Viongozi wa nchi za Afrika pia wamedhihirisha kuwa, misaada ya China kwa nchi za Afrika inatolewa bila kinyongo wala uchoyo, na bila kuweka masharti yoyote ya kisiasa. China inaweza kuzisaidia nchi za Afrika kujenga maboma, barabara na madaraja kwa mwendo kasi zaidi na bila gharama kubwa. Katika siku chache zijazo China inatazamiwa kuwa nchi inayoagiza mazao ya kilimo kutoka nchi za Afrika. Na shughuli za matengenezo na ujenzi za China barani Afrika zimehimiza nchi za Afrika zianzishe viwanda vidogo na vikubwa kiasi, ambavyo vimekuwa njia kuu ya kutoa nafasi nyingi za ajira katika nchi mbalimbali za Afrika.
Mwezi Juni mwaka huu, kwenye Mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika wa Baraza la uchumi wa dunia uliofanyika huko Cape Town, sera ya "kuelekea mashariki" ilikuwa suala lililozungumzwa sana na wajumbe waliohudhuria mkutano huo. Mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka huu, Mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ulifanyika kwa mafanikio mjini Beijing, ambapo viongozi wa nchi nyingi za Afrika walieleza kuwa watajifunza kwa makini uzoefu na maarifa ya China ili kuzisaidia nchi za Afrika zitafute njia ya maendeleo inayozifaa, walisema siku ya leo ya China ndiyo siku ya kesho ya Afrika.
Idhaa ya Kiswahili 2006-11-27
|