Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-28 16:08:35    
Barua 1128

cri
Leo kwanza tunapenda kuwataarifu wasikilizaji wetu kuhusu Kipindi maalum cha chemsha bongo kinachohusu vivutio vya utalii vya "Mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda".

Tukizungumzia Mkoa wa Sichuan, China, labda marafiki zetu wengi hawaujui, lakini kama tukitaja Panda, huenda watu wote wanaweza kufurahia wanyama hao wanaopendeza. Mkoa wa Sichuan, kusini magharibi ya China ndio maskani ya wanyama Panda.

Mkoani Sichuan kuna vivutio vingi vya utalii. Ili wasikilizaji wetu wauelewe zaidi mkoa huo na vivutio vyake, Radio China kimataifa imeanzisha kipindi maalum cha chemsha bongo kuhusu vivutio vya utalii vya "Mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda", na kuanzia tarehe 27 Novemba Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kila Jumatatu kwenye kipindi cha "Safari nchini China" itatangaza makala moja ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya utalii vya "Mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda", na matangazo ya kila makala yatarudiwa katika kipindi cha Sanduku la barua kila wiki, tunawakaribisha wasikilizaji wetu washiriki katika kipindi hiki cha chemsha bongo.

Kama tunavyofanya kila mwaka, kila tukisoma makala moja tutatoa maswali mawili ili wasikilizaji wetu wajibu. Kipindi hiki cha Chemsha bongo kitamalizika tarehe 15 Aprili mwaka 2007, baadaye kamati ya uchaguzi ya Radio China kimataifa itawachagua wasikilizaji washindi wa nafasi za kwanza, pili na tatu na wa nafasi maalum, na washindi watakaopata nafasi maalum wataalikwa kuja China kutembelea mkoani Sichuan. Tunawakaribisha wasikilizaji washiriki kwenye chemsha bongo na tunawatakia mafanikio mema.

Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa S.L.P 161 Bariadi Shinyanga?Tanzania ametuletea barua akituma salamu nyingi za heri na baraka kutoka Nchini Tanzania kwa wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Yeye ni mzima wa afya njema na anaendelea na shughuli za kila siku za ujenzi wa taifa, anasema lengo la barua yake ni kutoa pongezi kwa wafanyakazi wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa kutokana na juhudi kubwa katika kuwahudumia wasikilizaji kwa vipindi vinavyovutia sana ambavyo vinasikika kila siku.

Bwana Kilulu Kulwa anaendelea kusema ni ukweli usiopingika kwamba kutokana na vipindi hivyo vizuri vinavyowajulisha wasikilizaji maoni na uchambuzi wa watu mbalimbali, wakiwemo wasikilizaji wa Radio China kimataifa, imekuwa ni kichocheo kikubwa kabisa kwa yeye kuipenda radio China Kimataifa, watu wa China na taifa la China. Anasema Radio China Kimataifa inawashirikisha wasikilizaji wake moja kwa moja katika kipindi chake cha sanduku la barua na salamu zenu. Aidha mashindano ya ujuzi yanayoandaliwa na Radio China kimataifa kila mwaka yamemsaidia sana kujenga urafiki na undugu baina ya watu wa China na wa mataifa mengine duniani. Hivyo anapenda kuipongeza sana Radio China Kimataifa kwa mikakati na juhudi zake nyingi inazozifanya kuwajulisha wasikilizaji wake hali halisi ya maisha katika Jamhuri ya watu China na hivyo kufuta kabisa propaganda mbaya inayoenezwa kuhusu China, anasema hongera sana Radio China Kimataifa.

Bwana Kulwa anasema katika barua yake nyingine kuwa, ana furaha kutuma waraka mwingine, lengo kuu likiwa ni kutoa shukrani kwa kipindi cha sanduku ka barua cha tarehe 9 mwezi Julai 2006. Anasema siku hiyo pamoja na mengine tuliisoma barua yake aliyokuwa ameambatanisha majibu ya chemsha bongo ya mwaka huu yanayohusu "Mimi na Radio China kimataifa" Hivyo Bwana Kilulu anaamini kuwa majibu yake yalitufikia.

Bwana Kulwa anasema, mwaka 2005 alishiriki kwa juhudi na aliandika makala nzuri kuhusu umuhimu wa Taiwan kurudi nyumbani China. Kwa bahati mbaya hatukuisoma makala yake katika kipindi cha sanduku la barua na wala hatukumjulisha kama tulipokea majibu yake kuhusu chemsha bongo kuhusu ujuzi wa Taiwan. Anasikitika sana, kwani yeye anapenda sana kuiona Taiwan ikiungana na China, ili taifa liwe na nguvu na umoja. Anasema watanzania wanaamini sana dhana ya umoja ni nguvu, na ndio maana Muungano walio nao ni imara sana barani Afrika. Na mwisho anatumai kuwa urafiki wetu utaendelea kuimarika na kustawi siku hadi siku.

Tunamshukuru sana Bwana Kilulu Kulwa kwa barua yake ya kututia moyo na kutuhimiza tuchape kazi zaidi. Bwana Kulwa ni msikilizaji wetu tangu zamani sana, na tena ni rafiki yetu wa dhati sana, tunamshukuru sana juhudi zake za kututumia barua kila mara na kutusaidia kuboresha vipindi, tunamwambia kuwa kila mara tukipata barua yake, au hata ya msikilizaji yeyote tutaisoma hewani bila kusita.

Bw Mutanda Ayub Sharif wa S.L.P 172 Bungoma nchini Kenya anatoa shukrani na pongezi kwa wafanyakazi wa Radio China kimataifa kwa kazi zetu, anatumaini kuwa hivi sasa tunaendelea kuchapa kazi vilivyo. Anasema kwa sasa homa na matarajio makubwa yanalenga wale ambao walishiriki kwenye chemsha bongo. Anasema lengo kubwa la kushiriki kwenye chemsha bongo sio lazima iwe ni kupata ushindi, bali ni kujipatia zaidi ujuzi. Katika mashindano ya mwaka huu ya 2006, washindi watakuwa na mori au jambo la kujivunia kwani itakuwa ya historia kwa vile itakuwa sherehe kubwa sana nchini China kwa kuadhimisha miaka 65 ya Radio China Kimataifa. Kwa sasa wasikilizaji wengi wanaendelea kujiunga na idhaa hii, ana uhakika kuwa katika siku zijazo Radio China Kimataifa itavuma pote duniani.

Tunamshukuru sana Bwana Shariff kwa juhudi zake za kuitangaza Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Mwaka huu Msikilizaji wetu Franz Manco Ngogo wa Tarime Tanzania na Bwana Mutanda Ayub Shariff wa Bongoma Kenya wamechaguliwa kuwa wasikilizaji washindi wa nafasi maalum katika chemsha bongo ya mwaka huu kuhusu "Mimi na Radio China kimataifa, na hivi karibuni watafika Beijing kuhudhuria shughuli za kusherehekea miaka 65 ya Radio China kimataifa", hii ingekuwa ni fahari kwa wasikilizaji wetu wote, kweli kutokana na juhudi zao kubwa wamepata ushindi, na wanastahili kupongezwa, lakini kwa kweli kupata ushindi siyo lengo pekee la shindano la chemsha bongo, lengo kubwa ni kushiriki na kujipatia ujuzi.

Msikilizaji wetu Dennis Ombene wa S.L.P 8 Omogonchoro, Kisii, Kenya ametuletea barua akitoa shukrani kwa kazi nzuri na vilevile anatoa shukrani kwa makala aliyotumiwa na hasa chemsha Bongo ya mwaka huu. Anasema angependa kushauri tuongeze habari zinahusu China, kwani yeye anaona kama ni chache, lakini anafahamu kuwa changamoto kubwa ni muda kwa hiyo kama muda ukiruhusu ni vizuri habari kuhusu China ziongezwe na maelezo muhimu nayo yapewe muda zaidi. Vilevile anasema masafa ya FM huko kwao Kisii hayasikiki, anaomba kama inawezekana matangazo hayo ya FM yaboreshwe na yasikike hadi Kisii, pia wakati wa matangazo anaomba muziki wa kisasa nao ipewe kipaumbele. Na kuhusu mtandao wa Internet anatukumbusha kuwa, huduma ya internet haipatikani vijijini.

Anamaliza kwa kusema hata kuanzisha Klabu vijijini ni vigumu, kwa hiyo angeomba msaada wa fedha ili waweze kuazisha Klabu ya wasikilizaji.

Tunamshukuru sana Bwana Dennis Ombene kwa barua yake na maoni yake mazuri kuhusu kuongeza habari zinazohusu China, na kuhusu ombi la kufikisha matangazo ya FM huko Kisii Kenya. Kuhusu ombi la msaada wa fedha ili aweze kuanzisha klabu ya wasikilizaji, kwa kweli sisi tunashindwa kufanya hivyo. Tunapenda wasikilizaji wetu mkumbuke kuwa Radio China kimataifa ni chombo cha habari, hasa inashughulikia kazi za kurusha matangazo, na fedha za radio yetu zinatolewa na serikali kutokana na bajeti, mambo yote ya fedha ni serikali inayohusika. Tunaomba mtuelewe.

Msikilizaji wetu Dominic Nduku Mishoro wa S.L.P 1920 Kakamega, Kenya ametuandikia barua akisema anapenda kutoa salamu zake nyingi akitarajia kuwa wafanyakazi wote wa Radio China kimataifa ni wazima kwa uwezo wa mwenyezi Mungu. Kwanza anashukuru kwa barua alizotumiwa za chemsha Bongo ya tatu pamoja na kidadisi chenye maswali ya chemsha Bongo kweli kweli.

Mbali na hayo anasema Radio China Kimataifa imewaunganisha kupata marafiki kutoka sehemu mbalimbali duniani na hata ametumiwa zawadi za aina mbalimbali kadiri anavyozidi kuwasiliana na Radio China Kimataifa. Kwa upande wa vipindi, Bwana Dominic anasema kipindi kama cha jifunze kichina, anawaomba wahusika wa kipindi hicho wakiongezee muda wa matangazo na pia kiwe hewani kila siku ili kuwavutia wasikilizaji wengi ambao wana nia ya kujifunza na kuijua lugha ya kichina kupitia Radio China kimataifa. Pia anaomba wahusika wajenge vituo vingine vya mafunzo ya kujifunza lugha ya kichina mbali na kituo cha FM cha Nairobi.

Anasema vilevile Radio China kimataifa imeanza kubadilika sura pole pole, hivyo anaomba wahusika wajenge mitambo zaidi ya kuboresha usikivu wa matangazo kutoka kituo cha Fm cha Radio China Kimataifa Nairobi nchini Kenya kwa miji kama Garissa, Kisumu, Mombasa na Kakamega, na mwisho anawatakia kila la heri wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa kwa kazi zote wanzozifanya katika idhaa ya kiswahili.

Tunamshukuru kwa dhati Bwana Dominic Nduku Mishoro kwa barua yake na maoni na mapendekezo yake mbalimbali, yote aliyotuambia tutajitahidi kuyazingatia kwa makini.

Na mwishoni tunapenda kuwaambia tena wasikilizaji wetu kuwa, kuanzia tarehe 27 Novemba Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kila Jumatatu kwenye kipindi cha "Safari nchini China" itatangaza makala moja ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya utalii vya "Mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda", na matangazo ya kila makala yatarudiwa katika kipindi cha Sanduku la barua kila wiki, tunawakaribisha wasikilizaji wetu washiriki katika kipindi hiki cha chemsha bongo.

Idhaa ya kiswahili 2006-11-28