Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-28 16:44:52    
Uvumbuzi waleta mali

cri

Hivi sasa uvumbuzi unaambatana na maisha na kazi za watu. Uvumbuzi unaweza kuleta mali nyingi kwa watu, hivi sasa sekta ya uvumbuzi imekuwa sekta moja mpya inayofuatiliwa sana nchini China. Kampuni ya GOGO time iliyoanzishwa mwaka 2005 kwenye eneo la ustawishaji wa teknolojia la Zhongguancun, hivi sasa imekuwa mfano wa kuigwa kwa kampuni za wastani na ndogo za uvumbuzi mjini Beijing. Kampuni hiyo imefanya maajabu katika sekta ya majarida ya multimedia kwa uvumbuzi wa teknolojia ya kitarakimu, na katika muda wa miezi 8 tu ilikuwa na faida ya Yuan milioni 20. Naibu mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Bw. Xiong Lai alisema, mafanikio ya kampuni hiyo yanatokana na mtizamo wa uvumbuzi wa kuunganisha majarida ya multimedia na uenezi wa shughuli za kampuni. Alisema,

"Tunaona kuwa majarida ya multimedia yana nafasi kubwa ya maendeleo katika siku za baadaye, tukawa na mtizamo wa kuunganisha teknolojia ya multimedia na teknolojia ya kitarakimu, kitu ambacho kinaweza kuonesha vizuri zaidi mahitaji ya shughuli za kibiashara za kampuni na kutoa huduma nyingi zaidi za kujionesha kwa kampuni. Sasa baadhi ya kampuni kubwa zikiwemo shirika la utalii la Shennongjia, kampuni ya simu za mkononi za Bird na kampuni ya Skyworth, zinatumia teknolojia yetu."

Majarida ya multimedia yakiwa pamoja na flash, vipande vidogo vya video, muziki wa mazingira (background) na teknolojia ya 3D vinapendwa sana na watu. Licha ya kuweza kusoma majarida yetu kwenye Internet, watu wanaweza kuyasoma kwenye simu za mkononi na kompyuta za mkononi. Bw. Xiong Lai alisema kampuni ya GOGO time inatoa uwanja wa kujionesha kwa kampuni na kuonesha bidhaa zao, ambao ni mzuri sana ukilinganishwa na magazeti na majarida ya karatasi.

Ili kutoa huduma nyingi za kujitangaza kwa kampuni na kwa bidhaa zake, kampuni ya GOGO time imevumbua software ya kazi hiyo. Kampuni zinaweza kuonesha taarifa zake, tathmini za vipindi, ombi la uidhinishaji wa miradi, mapendekezo ya mipango na ufahamu kuhusu kampuni kwa kutumia software hiyo. Kampuni ya GOGO time inakidhi mahitaji ya kampuni mbalimbali, hivyo imekuwa na wateja wa baadhi ya kampuni maarufu zikiwemo mashirika ya utalii ya Shennongjia na Lijiang, bia ya Qingdao, sigara ya Hongtashan na kampuni ya magari ya Audi.

Chanzo cha mafanikio ya kampuni ya GOGO time, ambayo ni mfanyabiashara anayetoa huduma ya teknolojia ya kitarakimu ya multimedia, ni kutokana na kufanya juhudi kubwa katika uvumbuzi wa teknolojia. Naibu mkurugenzi wa kampuni Bw. Xiong Lai alisema,

"Mafanikio ya uvumbuzi wowote wa teknolojia yanaamuliwa na kuendana na mahitaji ya masoko kwa uvumbuzi huo, Ninaona kuwa chanzo kikubwa cha mafanikio ya uvumbuzi wetu wa teknolojia ni kuwa sisi tunasisitiza uvumbuzi wa teknolojia na matumizi ya uvumbuzi mpya, ambapo mahitaji ya wateja yamekuwa nguvu inayohimiza uvumbuzi wetu wa teknolojia."

Uwekezaji wetu kwenye uvumbuzi wa teknolojia umeleta faida, bidhaa tuliyozalisha ya "Shennongjia" ya tarakimu ya multimedia kwa ajili ya shirika la utalii wa "Shennongjia" mkoani Hubei, ambao ni sehemu maarufu ya utalii nchini China, imethibitishwa na idara husika ya serikali kuwa imefikia kiwango cha kisasa duniani. Mradi wa teknolojia ya tarakimu ya multimedia, waliyojenga kwa ajili ya kampuni ya bia ya Qingdao, ni mradi wa kwanza ambao watu wanaweza kushiriki moja kwa moja, watu wanashuhudia mchakato mzima wa uzalishaji bia toka kuchipuka kwa shayiri hadi bia inapowekwa ndani ya Chupa. Hivi karibuni kampuni ya GOGO time imewekezwa dola za kimarekani milioni 20 na Softbank Asia kutokana na kuvutiwa na maendeleo yake.

Kuhusu maendeleo ya kampuni hiyo katika siku za baadaye Bw. Xiong Lai alisema, kampuni ya GOGO time itajenga mtandao wa "multimedia wa China" ikitaka mikoa yote ya China iweze kuonesha bidhaa zake maarufu kwenye mtandao huo. Licha ya hayo kampuni yao itatafuta kazi duniani za kuonesha bidhaa na shughuli za biashara, ili kuongeza sifa za kampuni na kupanua uwezo wa kupata faida. Bw. Xiong Lai alisema, lengo la mauzo ya kampuni yao kwa mwaka huu ni Yuan milioni 200, na kuwa na ongezeko la 100% kwa mwaka katika miaka 3 ijayo.

Kampuni ya GOGO time ni moja tu ya kampuni nyingi za uvumbuzi zilizojitokeza katika miaka ya hivi karibuni mjini Beijing. Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya uvumbuzi imekuwa na nguvu muhimu ya maendeleo, thamani ya uvumbuzi wa kiutamaduni kwa mwaka jana ilifikia Yuan bilioni zaidi ya 96 ikichukua 14% ya pato la mji wa Beijing. Naibu kiongozi wa idara ya uchumi ya taasisi ya sayansi ya jamii ya Beijing Bw. Zhao Hong alisema, Beijing ina msingi imara wa teknolojia na uzoefu wa uzalishaji mali uliopatikana kwa miaka mingi katika maeneo ya utamaduni, elimu, rasilimali ya nguvukazi, software, mtandao wa internet na mawasiliano ya habari, ambao unachangia maendeleo ya kampuni za uvumbuzi kama ya GOGO time.

"Mji wa Beijing uliojengwa miaka zaidi ya elfu 3 iliyopita, kuwa mji mkuu wa China kwa miaka zaidi ya 850 na wenye msingi imara wa utamaduni, ni chimbuko la uvumbuzi, na kwa upande mwingine Beijing ni mji maarufu duniani, ambao shughuli za maingiliano ya kiutamaduni hufanyika mara kwa mara, jambo ambalo linaleta mtizamo wa uvumbuzi mpya unaoendana na mambo ya dunia."

Wataalamu wengi na uwezo mkubwa wa uvumbuzi wa sayansi na teknolojia, unatoa uungaji mkono mkubwa kwa sekta ya uvumbuzi wa utamaduni wa Beijing. Beijing ina watafiti wa sayansi zaidi ya laki 3, vyuo vikuu zaidi ya 70 pamoja na kampuni za uvumbuzi zikiwemo za usanifu wa kazi za viwanda, nguo na matangazo ya biashara zaidi ya elfu 20.

Naibu kiongozi wa idara ya utafiti wa uchumi ya taasisi ya sayansi ya jamii ya Beijing Bw. Zhao Hong alisema, katika miaka michache ijayo nguvu ya maendeleo ya sekta ya uvumbuzi ya Beijing itaendelea kuimarika, hususan ni kuwa serikali ya Beijing kuichukulia sekta ya uvumbuzi wa kiutamaduni kuwa sekta ya kimkakati ya Beijing katika miaka mitano ijayo, nguvu ya kimasoko na uhimizaji wa serikali vitaleta mustakabali mzuri kwa maendeleo ya sekta ya uvumbuzi ya Beijing.

Idhaa ya kiswahili 2006-11-28