Baraza kuu la 61 la Umoja wa Mataifa tarehe 27 lilifanya mkutano maalum wa maendeleo ili kutathmini hali ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia, kujadili kuongeza ushirikiano wa kimataifa, na kuharakisha utekelezaji wa mkakati wa maendeleo. Waliohudhuria mkutano huo wameona kuwa katika miaka kadhaa iliyopita, hali ya utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya milenia imepata maendeleo mazuri, lakini kwa upande mwingine jumla ya utimizaji wa malengo yaliyowekwa bado hauwezi kuwafurahisha watu. Hivyo jumuiya ya kimataifa inapaswa kufanya ushirikiano, kushughulikia na kutekeleza vizuri ahadi zao kuhusu suala la maendeleo, ama sivyo malengo ya maendeleo ya milenia hayataweza kutimizwa.
Malengo ya maendeleo ya milenia yalitolewa na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan, na kuthibitishwa kwenye mkutano wa wakuu wa duniani wa mwaka 2000. Malengo hayo ni malengo yatakayotimizwa na nchi mbalimbali duniani kabla ya mwaka 2015 katika sekta nane ambazo ni pamoja na kupunguza umaskini, kueneza elimu ya msingi, kuwa na usawa kati ya wanaume na wanawake na hifadhi ya mazingira.
Kwenye mkutano huo Bw. Annan alisisitiza kuwa, nia hasa ya kuweka malengo ya milenia ya maendeleo ni kuzihimiza nchi zinazoendelea ziweke mkakati kamili wa kujiendeleza, nchi zilizoendelea kuzisaidia nchi zinazoendelea, ili kuzisaidia nchi maskini zilete maendeleo yasiyoweza kutimizwa kwa kutegemea rasilimali zao tu. Kwa hivyo, malengo ya maendeleo ya milenia kwa kweli yamekuwa mkataba kwa nchi zote zilizoendelea na zinazoendelea. Lakini hadi leo nchi nyingi zilizoendelea bado hazijatekeleza mkataba huo.
Bw. Annan alidhihirisha kuwa linalosikitisha ni kwamba, kukuza uhusiano wa kiwenzi katika maendeleo duniani bado ni maneno yanayotamkwa tu katika sekta ya biashara. Bw. Annan alisema mazungumzo ya biashara ya duru la Doha yanapaswa kurejeshwa na kupata mafanikio, hili ni sharti la lazima katika kutimiza malengo ya milenia ya maendeleo.
Mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Mataifa Bi. Haya Rashed Al Khalifa alisema, japokuwa kutimiza malengo ya milenia ya maendeleo kunakabiliwa na changamoto kubwa, lakini jumuiya ya kimataifa imepata maendeleo makubwa. Alisema katika miaka 40 iliyopita, wastani wa maisha ya watu waishio katika nchi zinazoendelea umeongezeka kwa robo, katika miaka 30 iliyopita, idadi ya watu wasiojua kuandika wala kusoma duniani imepungua kwa nusu, katika miaka 20 iliyopita, watu milioni 400 duniani wameondokana na hali ya maskini. Bi. Khalifa alidhihirisha kuwa, mwaka jana thamani ya misaada ya maendeleo ya kiserikali duniani kwa mara ya kwanza ilizidi dola za kimarekani bilioni 100, binadamu hatimaye imetokomeza ugonjwa wa ndui, na kutazamiwa kutokomeza polio muda si mfupi baadaye. Mafanikio hayo yameonesha kuwa, kwa jumla malengo ya kupunguza umaskini duniani yatatimizwa kwa wakati.
Wakati huohuo Bi. Khalifa alisema hali ya maendeleo duniani bado si ya kufurahisha. Katika baadhi ya nchi, kwa wastani kila dakika mjamzito mmoja anakufa wakati wa kujifungua, kila mwaka watoto wachanga milioni 4 wanakufa kabla hawajatimiza umri wa mwezi mmoja, asilimia 3 ya watoto hawawezi kupata matibabu, watu milioni moja wanakufa kutokana na malaria, ambapo watu milioni 2 wanakufa kutokana na kifua kikuu na wengine milioni 3 wanakufa kutokana na ugonjwa wa ukimwi.
Kwenye mkutano huo hotuba iliyotolewa na mkuu wa benki ya maendeleo ya kiislam Bwana Ahmed Mohamed Ali ilifuatiliwa na watu wengi. Alitangaza kuwa bodi ya wakurugenzi ya benki hiyo imependekeza kuunda mfuko wa kupunguza umaskini, mfuko huo utakaoanza na mtaji wa dola za kimarekani bilioni 10 utazinduliwa rasmi mwaka kesho, nia yake hasa ni kuzisaidia nchi zilizoko nyuma kabisa kimaendeleo barani Afrika.
|