Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-29 19:52:27    
Gesi ya kinyesi yaboresha mazingira na maisha ya watu wa mkoa wa Guangxi

cri

 

Gesi ya kinyesi ni nishati safi inayozalishwa kwa takataka. Kwa kiasi kadhaa inaweza kutumiwa badala ya mafuta, gesi ya asili na makaa ya mawe. Watu wanatumia vinyesi na takataka kuzalisha gesi ya kinyesi. Gesi ya kinyesi inaweza kutosheleza mahitaji ya kuleta joto, kuwasha taa na kupika chakula, na masalio ya kuzalisha gesi ya kinyesi yanaweza kutumiwa kama mbolea kwa kupanda miti ya matunda na mimeaa ya nafaka.

Mwandishi wa habari alipotembelea katika mkoa wa Guangxi ulioko kusini mashariki ya China aligundua kuwa, katika sehemu hiyo hewa imekuwa safi zaidi, milima imefunikwa na miti mingi zaidi, na wakulima wamepata faida nyingi zaidi kuliko zamani kutokana na matumizi ya nishati hiyo safi.

Mkurugenzi wa ofisi ya kuwasaidia watu maskini Bw. Hu Decai alisema, serikali imeweka matumizi ya gesi ya kinyesi kwenye mpango wa kuwasaidia wakulima wa huko kujiendeleza. Na matumizi ya gesi ya kinyesi yanahitaji kuendelezwa na kutumiwa zaidi.

"Gesi ya kinyesi ina sifa kadhaa. Kwanza inasaidia kutatua suala la nishati kwa wakulima wa huko, kupunguza uharibifu wa misitu, na kuboresha mazingira. Tena gesi ya kinyesi ni safi, watu wanatumia vinyesi vya ng'ombe na farasi kuzalisha gesi ya kinyesi, na masalio yanaweza kutumiwa kuwa mbolea. Aidha kutumia gesi ya kinyesi kunaweza kuwapunguzia kazi baadhi ya watu hasa wanawake."

Katika kijiji cha Nawo wilayani Qingxiu mjini Nanning, mkulima Lan Hualin na familia yake wanalima hekta 2 za mashamba. Alitumia mapato yake kujenga nyumba ya ghorofa mbili. Nyumbani mwake, mwandishi wa habari hakuona jiko la jadi lenye rangi nyeusi kutokana na moshi, nyumba yake ni safi sana. Mabadiliko hayo yanatokana na matumizi ya gesi ya kinyesi. Mke wake alimwambia mwandishi wa habari akisema,

"Sasa ninapika chakula kwa gesi ya kinyesi, ni rahisi kuitumia. Zamani hatukutumia gesi ya kinyesi, hivyo tulilazimika kukata kuni milimani, na halafu kuzikausha kuni hizo. Sasa hatuna haja ya kukata kuni milimani, tuna wakati mwingi zaidi kufuga ng'ombe na kupanda mahindi na mpunga."

Wilaya inayojiendesha ya kabila la Wayao ya Gongcheng iko kusini mashariki mwa mji wa Guiling, mkoani Guangxi. Katika wilaya hiyo karibu kila nyumba ina shimo la kuzalisha gesi ya kinyesi. Katika kijiji cha Hengshan mwandishi wa habari aliona kuwa, katika kijiji hicho chenye watu zaidi ya mia 2 kuna mashimo 56 ya kuzalisha gesi ya kinyesi, asilimia 96 ya familia zina mashimo ya kuzalisha gesi ya kinyesi. Katika baadhi ya vijiji vya wilaya ya Gongcheng, mashimo makubwa ya kuzalisha gesi ya kinyesi yamejengwa, mabomba ya gesi ya kinyesi yapo kwenye kila nyumba. Uzalishaji na matumizi ya gesi ya kinyesi yamewekwa pamoja, na jambo hilo limepunguza kazi kwa watu na kubana matumizi ya ardhi.

Mkulima Rong Wenxi alimwambia mwandishi wa habari kuwa, kuna watu wanne nyumbani mwake, sasa wanachemsha maji, kupika chakula na kuwasha taa kwa nishati ya gesi ya kinyesi. Si kama tu gesi ya kinyesi ni safi na ni rahisi kutumia, bali pia inaweza kubana matumizi ya pesa. Alisema,

"Bei ya gesi ya kinyesi ni nafuu, tukitumia gesi ya asili tunahitaji kutumia Yuan 92 kwa mwaka, lakini sasa tunatumia gesi ya kinyesi, tunatumia Yuan 32 tu kwa mwaka, yaani theluthi mbili ya pesa zimepunguzwa."

Uzalishaji na matumizi ya gesi ya kinyesi una manufaa mengi. Naibu mkuu wa idara ya misitu ya mji wa Guilin Bw. Jiang Ruohai alisema,

"Mabadiliko ya aina za nishati zinazotumiwa vijijini na uenezi wa matumizi ya gesi ya kinyesi yamesifiwa kuwa ni ukombozi kwenye historia ya maendeleo ya nishati vijijini. Si kama tu wakulima wengi hawana haja ya kufanya kazi kubwa za kukata kuni, bali pia maeneo yanayofunikwa na miti mjini Guilin yameongezeka kuwa asilimia 66.46 kutoka asilimia 37.7 ya mwaka 1980.

Matumizi ya gesi ya kinyesi mkoani Guangxi yamepata maendeleo makubwa, wakulima wa huko wamenufaika na gesi ya kinyesi, pia wamegundua njia mpya ya ujenzi wa vijiji. Watu wengi kutoka nchini na nchi za nje wamekwenda huko kujifunza maarifa yao. Mkoa huo ukiwa ni sehemu muhimu ya kujifunza maarifa ya kuwasaidia watu maskini, umepokea ujumbe wengi wa nchi zinazoendelea zikiwemo nchi za Afrika. Wageni wana hamu kubwa kuhusu uzalishaji na matumizi ya gesi ya kinyesi. Kuhusu mambo hayo, naibu mkurugenzi wa kituo cha usimamizi wa utoaji misaada kwa watu maskini kwa fedha za nje Bw. Li Fangzhen alisema,

"Kama nilivyojua, hali ya hewa ya nchi za Afrika ni joto na inafanana na mkoa wa Guangxi, hivyo inafaa kujenga mashimo ya kuzalisha gesi ya kinyesi barani Afrika. Wageni wa Afrika wana hamu kubwa kuhusu mashimo ya gesi ya kinyesi, wakija kwetu wanawasha moto wenyewe ili kuona matumizi ya gesi ya kinyesi. Waliona kuwa tumebadilisha takataka kuwa vitu vinavyoweza kutumika."

Wasikilizaji wapendwa, kama mtapata fursa ya kuja hapa China, karibuni mkoani Guangxi, mweze kutazama mazingira mazuri mkoani humo, kuchuma matunda yasiyo ya uchafuzi, na kuona mashimo ya gesi ya kinyesi.