Mkutano wa tatu wa baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ulifunguliwa tarehe 29 Novemba huko Geneva. Mkutano huo utajadili kutunga njia za kushughulikia mambo, utaratibu wa baraza hilo na masuala yaliyopo katika sekta ya haki za binadamu duniani. Hivi sasa bado kuna tofauti kubwa kati ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea kuhusu masuala hayo.
Kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mambo ya haki za binadamu Bi. Louise Arbour kwenye ufunguzi wa mkutano huo alisoma barua ya katibu mkuu Kofi Annan. Kwenye barua yake Bw. Annan alieleza matumaini yake kuwa baraza la haki za binadamu litafanya mkutano maalum kuhusu suala la Darfur. Alisema tangu baraza hilo lianzishwe limefanya mkutano maalum kwa mara tatu kuhusu mgogoro kati ya nchi za kiarabu na Israel, mgogoro huo haupaswi kuzuia ufuatiliaji wa masuala mengine. Bi. Arbour alidhihirisha kuwa hali ya kukiuka haki za binadamu kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa inakuwa mbaya siku hadi siku. Amezitaka Palestina na Israel zichukue hatua kupunguza mgogoro kati yao. Mjumbe wa China kwenye hotuba yake alizitaka tena pande husika za mgogoro huo zitekeleze maazimio husika ya Umoja wa Mataifa na kuleta amani na utulivu kwa sehemu ya Palestina na Israel.
Wachunguzi wanaona kuwa, baraza la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa liliundwa kwa muda usiozidi nusu mwaka uliopita, lakini tofauti kati ya nchi zilizoendelea na nchi zinazoendelea zimeanza kuonekana kuhusu masuala kadhaa, kama vile kufanya mkutano maalum. Baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za magharibi vinaona kuwa, baraza la haki za binadamu limefanya mkutano maalum kwa mara tatu kuhusu mgogoro kati ya nchi za kiarabu na Israel, mikutano hiyo iliikosoa Israel ya kukiuka haki za binadamu, lakini linapuuza hali ya kukiuka haki za binadamu nchini Sudan, hali hiyo imeonesha kuwa nchi zinazoendelea hazina usawa kuhusu suala hilo. Lakini nchi zinazoendelea zinasema mgogoro kati ya nchi za kiarabu na Israel na suala la Darfur ni masuala mawili tofauti kabisa. Mgogoro kati ya Israel na Palestina unasababishwa na uvamizi, vitendo vya kijeshi vya Israel vimekiuka vibaya haki za binadamu za watu wa Palestina. Lakini suala la Darfur ni jambo la ndani ya Sudan, jumuiya ya kimataifa inatakiwa kuzihimiza pande mbili ziache mapambano kwa msingi wa kuheshimu mamlaka ya Sudan, na kutatua mgogoro kati yao kwa njia ya majadiliano.
Tofauti ya pili kati ya nchi zinazoendelea na nchi zilizoendelea ni maoni tofauti kuhusu madaraka ya wataalamu wanaojitegemea, vikundi vya kazi na waandishi maalum wa ripoti. Kama inavyojulikana, kulingana na kamati ya haki za binadamu umaalum mkubwa wa baraza la haki za binadamu ni kuweka utaratibu wa kuthibitisha hali ya haki za binadamu ya nchi wanachama wote wa Umoja wa Mataifa kwenye msingi wa kuwa na usawa kila baada ya muda fulani, lakini watu 13 kati ya wataalamu wanaojitegemea, vikundi vya kazi na waandishi maalum wa ripoti walioteuliwa na kamati ya haki za binadamu wanashughulikia hasa masuala ya nchi kadhaa zinazoendelea, kwa hivyo nchi zinazoendelea kwenye mkutano wa pili wa baraza la haki za binadamu zilipitisha uamuzi wa kutaka kusawazisha utaratibu wa vitendo na madaraka ya watu hao kabla hawataondolewa.
Wachambuzi wanadhihirisha kuwa, zamani nchi zilizoendelea zilifanya suala la haki za binadamu kuwa kama ni chombo cha kisiasa cha kutoa shinikizo kwa nchi zinazoendelea, kamati ya haki za binadamu imekuwa mahali pa kufanya mapambano makali ya kisiasa kati ya kusini na kaskazini. Inaonekana kuwa, nchi kadhaa za magharibi bado haziwezi kuacha mawazo na vitendo zilivyofanya, hivyo baraza la haki za binadamu litakabiliwa na matatizo mengi katika mchakato wa mageuzi.
|