Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-11-30 16:24:07    
Akina Bibi waliojikita katika kutunza na kuhifadhi Mto Hanjiang

cri

Mto wa Changjiang ni mto maarufu kwa urefu kwake kuliko mingine ya China. Tawi lake kuu linaitwa mto Hanjiang. Makala hii inahusu kina Bibi wawili wanaoishi kando ya Mto Hanjiang, ambao wamejikita katika shughuli za kueneza elimu ya kutunza na kuhifadhi raslimali ya maji, na kuzuia viwanda kadhaa visitoe maji machafu mtoni.

Kina Bibi hao wawili mmoja anaitwa Yun Jianli, na mwingine anaitwa Ye Fuyi, wote wamestaafu kazi. Wanaishi katika mji wa Xiangfan, mkoani Hubei katikati ya China, ambapo mto Hanjiang wenye urefu wa kilomita 1,500 unapita kwenye mji huo. Baada ya kustaafu wanawake hao wawili wanaishi raha mustarehe kwa kutegemea pensheni zao. Je, ni kitu gani kilichowafanya wafuatilie shughuli za kuhifadhi mazingira?

Mama Yun Jianli mwenye umri wa miaka 60 alieleza kuwa, chanzo ni safari moja aliyofanya ya kuvuka Mto Hanjiang mwanzoni mwa mwaka 2000. Alisema "Nilikuwa navuka Mto Hanjiang kwa basi kwa kupita daraja, ambapo kulikuwa na mtu aliyesema, angalia maji machafu yanatiririshwa mtoni, kuna harufu mbaya! Mwenzake akijibu, hii si harufu mbaya sana! Nenda uangalie tawi lake mto wa Gunhe, maji yake ni machafu zaidi. Maneno hayo yalinipa mshangao mkubwa sana. Nikaamua kuwa ningejikita katika shughuli za kutunza na kuhifadhi mto wa Hanjiang mpaka mwisho wa maisha yangu."

Tangu zamani sana Mto Hanjiang ulikuwa unajulikana kwa maji yake safi. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na maendeleo ya uchumi, maji machafu yanayoletwa na viwanda na wakazi wa mji, yanatiririka kwenda kwenye mto huo. Tangu mwezi Machi mwaka 2000, mama Yun Jianli alianza kuchunguza hali ya mazingira ya matawi matano ya mto huo, akagundua kuwa baadhi ya matawi yalikuwa na hali mbaya kutokana na uchafuzi. Alitoa mapendekezo mara kadhaa kwa serikali ili vyanzo vya kuleta uchafuzi viweze kushughulikiwa kwa haraka iwezekanavyo. Mwezi Agosti mwaka 2002, mama Yun akishirikiana na mama mwingine Ye Fuyi walianzisha shirika lisilo la kiserikali linaloshughulikia uhifadhi wa mazingira, shirika hilo linaloitwa Mto Hanjiang wa kijani, ni la kwanza la namna hiyo mkoani Hubei.

Mama Ye Fuyi ni mshirika mkubwa wa mama Yun Jianli. Mama Ye alieleza kuwa, watu wengi wanakuja kutembelea shirika hilo, wakiwemo waandishi wa habari, watu kutoka mashirika mengine ya uhifadhi wa mazingira, watu wa shule mbalimbali, wanaojitolea na wakazi wa kawaida, ambao wanashauriana jinsi wanavyochangia shughuli za kutunza na kuhifadhi Mto Hanjiang. Mama Ye alisema, "Kazi yetu ni ngumu, hata hivyo tunaifanya kwa furaha. Baadhi ya akina mama wenzetu ambao tunafanya nao pamoja mazoezi ya kujenga mwili, huwa wanatupuuza wakisema, kwa nini mnataka kufanya kazi nyingi bila kulipwa? Huwa najibu kuwa, silipwi lakini nafanya kazi hiyo kwa ajili ya kujiletea furaha tu, kitu ambacho kinafanana na sisi kufanya mazoezi ya kujenga mwili. Zaidi ya hayo, tunafanya mazoezi kwa ajili ya kujenga miili yetu tu, lakini shughuli za kuhifadhi mazingira ni kutoa mchango kwa wengine, kwani kila mtu ananufaika na mazingira safi. Hili ni jambo la maana zaidi."

Kwa maoni ya mama Yun Jianli, kuwaelimisha watu umuhimu wa kuhifadhi mazingira ni muhimu sana kwa hivi sasa. Kwa hiyo kazi hiyo inapewa kipaumbele na shirika hilo. Mpaka hivi sasa shirika hilo limeeneza elimu husika miongoni mwa watu zaidi ya elfu 70 wanaoishi kando ya mtiririko wa mto wa Hanjiang.

Licha ya hayo mama hao wawili wanazingatia sana kuwaelimisha watoto umuhimu wa kutunza mazingira. Wakitembelea sehemu fulani, kwa kuanzia wanakwenda shuleni kueneza elimu ya uhifadhi mazingira. Wametembelea shule zaidi ya 300 za sekondari, shule za msingi na shule za chekechea. Baada ya kusikiliza maelezo waliyotoa, watoto wengi wa shule za msingi walikuwa wanafanya hiari kubadilisha tabia ya kutupa taka ovyo, na kujitokeza kueneza elimu ya kutunza raslimali ya maji miongoni mwa jamaa zao.

Mwanafunzi mmoja wa shule ya msingi Zhai Tingting alisema "Tulipofundishwa na mama Yun tulianza kuchukua hatua. Tukiwakuta watu wengine wanatupa taka ovyo, tunawakosoa na kuwashauri wachukue takataka na kuzitupa ndani ya masanduku ya kukusanyia takataka, vile vile tunawaambia umuhimu wa kutunza mazingira tuliyonayo ili tuweze kuvuta hewa safi."

Katika juhudi za kueneza umuhimu wa kuhifadhi Mto Hanjiang, toka mwezi Aprili mwaka 2003 mpaka mwezi Mei mwaka 2004, wazee hao wawili walianzisha kampeni mbili za kutembea kwa miguu kando ya Mto Hanjiang na tawi lake Mto Tangbai. Kampeni hizo ziliwavutia watu wengi, ambapo mamia ya watu walijitokeza kushiriki kwenye operesheni hizo. Kwenye matembezi hayo walitafuta vyanzo vya maji machafu, kukusanya vipimo vya maji na kueneza elimu ya hifadhi ya mazingira. Kampeni hizo zilifuatiliwa na serikali ya mji wa Xiangfan, ambayo ilichukua hatua za kufunga viwanda kadhaa vya kutengeneza karatasi vilivyoleta uchafuzi mbaya, na viwanda vingine vililazimishwa kufanya marekebisho ndani ya kipindi fulani.

Ili kuongeza ufanisi wa kazi yao, shirika hilo la uhifadhi wa mazingira lilianzisha tovuti kwenye mtandao wa Internet. Hivi sasa majina ya akina Bibi hao wawili pamoja na shirika waliloanzisha yanajulikana kwenye maeneo ya mtiririko wa Mto Hanjiang.

Idhaa ya kiswahili 2006-11-30