Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-12-04 20:08:38    
Jumuiya ya Afrika Mashariki yapiga hatua kubwa

cri

Kwenye mkutano wa 8 wa wakuu uliofanyika tarehe 30 Novemba huko Arusha, Tanzania, wakuu wa nchi tatu wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Tanzania, Kenya na Uganda waliamua kuzipokea Burundi na Rwanda kuwa nchi wanachama wapya wa jumuiya hiyo. Hii ni hatua nyingine kubwa iliyopigwa katika mchakato wa jumuiya hiyo kuleta umoja wa sehemu hiyo.

Jumuiya ya Afrika Mashariki ni umoja wa uchumi wa kusaidiana ulioundwa kutokana na kuwepo kwa desturi za utamaduni wa Kiswahili wa sehemu hiyo. Jumuiya mpya ya Afrika Mashariki itakuwa na nchi wanachama watano yaani Burundi, Kenya, Rwanda?Tanzania na Uganda, eneo la jumuiya hiyo mpya litafikia kilomita za mraba milioni 1.81, idadi ya watu milioni 106, ambapo thamani ya uzalishaji mali ya sehemu hiyo itafikia dola za kimarekani bilioni 50.

Nchi tatu za Kenya, Tanzania na Uganda ziliwahi kuanzisha umoja wa forodha mwaka 1967, baadaye zilifanya majaribio ya kuunda umoja wa uchumi wa kikanda kwa njia mbalimbali kama vile kamati ya ngazi ya juu ya Afrika Mashariki, shirika la kutoa huduma za pamoja la Afrika Mashariki, na jumuiya ya ushirikiano ya Afrika Mashariki. Nchi hizo tatu zilianzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1967, ambayo ilivunjika mwaka 1977 kutokana na kuwepo kwa tofauti za kisiasa na makwaruzano ya kiuchumi.

Tangu Jumuiya mpya ya Afrika Mashariki ianzishwe mwaka 2001, nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda zilijaribu kuondoa tofauti zao katika maendeleo ya kiuchumi, kuanzisha umoja wa ushuru wa forodha wa Afrika Mashariki mwezi Januari mwaka 2005, na mwishoni mwa mwaka 2006, sehemu ya Afrika mashariki imekuwa sehemu ya pamoja ya utalii, na watalii kutoka nchi za nje wakienda katika sehemu hiyo watapewa visa ya pamoja ya Afrika mashariki. Jumuiya ya Afrika Mashariki pia imetunga ratiba ya tumia sarafu ya pamoja na kuunda soko la pamoja ifikapo mwaka 2010, na kuunda shirikisho la kisiasa ifikapo mwaka 2013.

Kuanzia katikati ya mwezi Novemba mwaka huu, nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeanza kuwafahamisha wakazi wa sehemu hiyo mchakato na umuhimu wa kuleta umoja wa kiuchumi na shirikisho la kisiasa, na kukusanya maoni na mapendekezo ya wakazi wa sehemu hiyo kuhusu mwelekeo wa kuleta umoja wa kiuchumi na shirikisho la kisiasa. Jumuiya ya Afrika Mashariki pia imeamua kuongeza nguvu ya kueneza mchakato huo kwa njia ya kuadhimisha siku ya jumuiya hiyo ili kuweka msingi wa kutimiza umoja wa kiuchumi na shirikisho la kisiasa.

Wakati huo huo mkutano wa 8 wa wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulizindua mkakati wa maendeleo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2006 hadi 2010, mambo muhimu yaliyomo ni kuboresha miundo mbinu ya mawasiliano, bandari, viwanja vya ndege na forodha, ili kuweka mazingira mazuri kwa kuanzisha soko la pamoja.

Viongozi wa nchi tano za Burundi, Kenya, Rwanda, Tanzania, na Uganda wamefikia maoni ya kauli moja, yaani kuimarisha maendeleo ya Afrika mashariki kwa kufanya ushirikiano kati ya nchi zilizoko nyuma kimaendeleo, kusaidiana na kupanua soko. Waliona kuwa japokuwa kuna matatizo ya aina mbalimbali, lakini mchakato wa kuleta umoja wa kiuchumi wa Afrika mashariki utasonga mbele kithabiti kwa kufanya juhudi na kufikia maelewano na ushirikiano kati ya nchi wanachama.